The House of Favourite Newspapers

Kwa Nini Wanaume Wanapendazaidi Kuchepuka?

0

ALHAMISI nyingine Mungu ametupa zawadi ya uhai. Tunakutana kwa pamoja kuzungumza yahusuyo mahusiano na maisha kwa ujumla.

 

Hakuna ambaye anatamani kuishi kwenye maisha ya mahusiano yenye matatizo, lengo letu hapa siku zote ni kuhakikisha tunapeana mafundisho mbalimbali ya mambo ya kufanya ili ukiwa kwenye mahusiano, uwe salama.Unapokuwa na amani kwenye mahusiano, hata maendeleo yako utayaona.

 

Unapokuwa kwenye migogoro, hata ustawi wa maendeleo yako unaweza kupungua. Ndiyo maana nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara, hakikisha sana unaitafuta amani ya moyo kwa gharama yoyote.

 

Wewe na mwenza wako muamue kweli kusaidiana kutafuta amani ya moyo. Msaidiane kuishi vizuri, kila mmoja ambebe mwenzake katika udhaifu wake. Mtiane moyo pale mnapokutana na magumu, hakika mtafanikiwa.

⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP: ⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8 ⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx

Kama mada ya leo inavyojieleza hapo juu, miongoni mwa changamoto kubwa kwenye mahusiano inayowaandama watu wengi kwenye mahusiano, ni suala zima la kuchepuka. Japo wapo wanawake wanaopenda tabia hiyo lakini zaidi suala hili limeshamiri kwa wanaume.

 

Hii inatokana na kiasili au kimaumbile, wanaume ni watu ambao hawawezi sana kujizuia na matamanio ya tendo la ndoa kuliko wanawake. Yaani mwanamke angalau anaweza kukaa bila kufanya tendo la ndoa lakini mwanaume inakuwa vigumu.

 

Wanaume wana tamaa zaidi kwenye tendo hilo. Wanajiendekeza, hawaridhiki na hivyo kujikuta hata kama wapo na mahusiano ya kudumu, bado wanaweza kuwa na michepuko nje.

Mwanaume anakuwa na mke wake ambaye kwa macho ya kibanadamu kila mtu anamtamani lakini anakwenda kutembea na mhudumu wa baa Si kwamba anakuwa amempenda sana huyo mhudumu wa baa, bali anapatwa na tamaa za muda mfupi ambazo zinachanganyika na ‘pepo wa kiume’ hivyo kujikuta amefanya maamuzi ambayo hata kesho yake anaweza kuyajutia.Mbali na hilo, kitu kingine kinachochangia mwanaume achepuke zaidi ni utulivu wa mwanamke wake.

⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP: ⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8 ⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx

Mwanamke akiwa na ‘kelele’ nyingi ndani, anapokuwa mkorofi wakati mwingine wanaume huamua kuusaka utulivu nje.Anaamua tu kutumia muda wake mwingi kujiburudisha huko nje sababu anajua akirudi ndani kutakuwa na kelele. Mbali na kuzungumza masuala ya kifamilia, hata lile tendo la ndoa linakuwa limepoteza ladha kwa mke, hivyo haoni sababu hata ya kulifanya.

 

Anajua anapokuwa na kiu ya tendo, bora aende nje akapewe huduma na ‘mafundi’ wanaojua kutoa huduma nzuri na kuvutia. Watu ambao wanatoa huduma huku wakitoa lugha nzuri na tamu, lugha rafiki na yenye kubembeleza.Mke anabaki kuwa mke jina lakini raha ya tendo inapatikana nje.

Hivyo atamuacha mkewe ndani, anakuwa na chimbo lake la kumpa amani. Kingine pia kinachowafanya wanaume wachepuke ni kwa sababu ya kutopata mtoto.

 

Wapo wanaume ambao wakiona hawapati mtoto ndani ya nyumba, huamua kujaribu nje. Mara nyingi wanaamini kwamba wao wako sawa ila wenza wao ndiyo wenye matatizo ya uzazi. Wanakwenda nje ili kutafuta watoto.Ndugu zangu, maisha ya kuchepuka hayafai.

 

Changamoto zote nilizozitaja kama sababu ya kuchepuka, zinatibika kama tu mwanaume mwenyewe ataamua. Acha tamaa za kijinga, tafuta mtu mmoja na uridhike naye.

 

Inapotokea kuna migogoro au mtu wako anapenda kelele ndani ya nyumba, muelimishe na usimkimbie au kutaka kumkomoa kwa kutoka nje.

 

Ukifanya hivyo si tu ni hatari wa usalama wako, lakini pia naye anaweza kulipizia kwa kuchepuka halafu mkapoteza kabisa uelekeo wa maisha.Kama kuna changamoto ya uzazi, waoneni wataalam wa afya watawapa suluhu ya changamoto yenu kwani siku hizi hakuna kinachoshindikana kama kweli lengo lenu ni kupata mtoto.Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!

⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP: ⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8 ⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx

Instagram na Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.

Leave A Reply