KWA WALICHOKIFANYA CHINA… NDOA YA LULU UTATA TUPU!

DAR ES SALAAM: Wakati wakiwa nchini China msimu wa Sikukuu za Krismasi na mwaka mpya kwa ajili ya kula bata kama lote, ile ndoa kabambe ya malkia wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mmliki wa Radio EFM, Francis Siza ‘Majizo’ iliyokuwa ikisubiriwa kwa shauku kubwa imeibua utata mzito, Gazeti la Amani limedokezwa.  

 

Baada ya kutolewa mahari na Majizo, Septemba, mwaka jana, ndoa ya Lulu ilitarajiwa kufungwa mwezi uliopita wa Desemba kabla ya kuingia mwaka 2019. Sasa basi, wakati wawili hao wakifanya yao China, ghafla, mapema wiki hii ziliibuka habari zenye utata mkubwa kuwa walifunga ndoa hiyo kwa siri nchini humo kabla ya kuingia mwaka 2019 kama walivyokuwa wamedhamiria. Ilidaiwa kuwa baada ya ndoa hiyo kufungwa huko ughaibuni, shughuli kabambe itafuata Bongo hivi karibuni.

 

MAKONDA ATHIBITISHA

Wakati taarifa hizo zikiwa hazina chanzo cha kuthibitisha, ghafla aliibuka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kuzidisha utata zaidi baada ya kuthibitisha tukio hilo la ndoa ya Lulu na Majizo kupitia ukurasa wake wa Instagram. Makonda alifunguka hayo alipokuwa akitoa pongezi kwa mchekeshaji wa Bongo, Emmanuel Mathias ‘MC Pilipili’ aliyemvisha pete ya uchumba mchumba’ke wa muda mrefu, Philomena Thadei ‘Mena’ wikiendi iliyopita.

 

Aliandika; “…heri Majizo ameamua kufungia China, sasa tunasubiri send-off huku (Bongo)…” Kama itakumbukwa, Makonda ndiye aliyetangaza kuwa mwenyekiti wa kamati ya harusi ya Lulu na Majizo hivyo taarifa yake ilionekana kuwa mashiko, lakini bado maswali yakawa palepale kwamba kwa nini waliamua kufunga kwa siri nchini humo hivyo kuwachanganya ndugu wa maharusi.

 

MSHTUKO

Katika kusaka ukweli wa jambo hilo, kama kweli ndoa hiyo imefungwa, Gazeti la Amani lilizungumza na mtu wa karibu wa Majizo ambaye alionesha kushtushwa na habari za kufungwa kwa ndoa hiyo nchini China.

 

“Haiwezekani ikafungwa kimyakimya kwa staili hiyo. Hakuna kitu kama hicho kwani lazima ningejua,” alisema mtu huyo na kuongeza: “Hayo ni mambo ya mitandaoni na kama kweli imefungwa hakuna ndugu wa upande wowote amehusika. Kama unataka kuamini mpigie ndugu yeyote wa Lulu au Majizo umuulize kama kuna ishu kama hiyo.”

 

MASTAA WENZAKE

Baada ya kumsikia mtu huyo wa karibu, gazeti hili lilizungumza na ndugu wa upande wa Lulu na waigizaji wenzake ambao walishtushwa kusikia kufungwa kwa ndoa hiyo. “Kama ni kweli, basi hakuna msanii aliyealikwa na ndiyo maana tunaona kama ni jambo la uzushi tu, Lulu hawezi kufunga ndoa halafu tusijue au asiwaalike wasanii wenzake,” alisema mmoja wa waigizaji wakubwa wa sinema za Kibongo akiomba asinukuliwe kwani siyo msemaji wa tasnia hiyo.

KWA MAMA LULU

Hata hivyo, Amani lilipiga hodi nyumbani kwa mama mzazi wa Lulu, Lucresia Karugila maeneo ya Mbweni jijini Dar ili kuthibitisha habari hizo ambapo hata majirani walishangaa kusikia ndoa hiyo ilifungwa China. “Mama Lulu ametoka maana ndiye angeweza kututhibitishia. Hapa mmetushtua maana tulikuwa tunasubiri tu cherekochereko.

 

“Kwa kweli hatujasikia kama hiyo ndoa imeshafungwa kama mnavyosema. Sisi ndiyo kwanza tunasikia habari hizi kutoka kwenu waandishi,” alisema mmoja wa majirani wa mama Lulu aliyejitambulisha kwa jina moja la Juma. Baada ya kumkosa mama Lulu nyumbani hapo, Amani lilimtafuta kupitia kilongalonga chake cha kiganjani, lakini kiliita kwa muda mrefu bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi (SMS) hakujibu.

 

LULU ATOA OFA

Wakati mjadala wa ndoa yake ukipamba moto, mapema wiki hii Lulu alitoa ofa kwa mashabiki wake kwa kutaka kugawa nguo zake nyingi zilizopo kabatini huku akiwataka watu mbalimbali kumtumia picha ya nguo waliyowahi kumuona nazo akiwa amevaa na kupendeza kisha yeye kuipenda ili aweze kugawa nguo hizo. Kupitia ukurasa wake wa Snapchat, Lulu aliandika; “Kuna nguo yoyote uliwahi kuipenda na ukatamani kuwa nayo…okey 2019 nitaanza kusafisha kabati langu…who si ready…”

 

LULU NA MAJIZO

Taarifa za Lulu kufunga ndoa na Majizo zilianza kuzagaa tangu mwaka juzi. Hata hivyo, haikufanyika. Sababu kubwa ikitajwa ni ile kesi iliyokuwa ikimkabili Lulu ya kumuua bila kukusudia mwigizaji mwenzake aliyekuwa mwandani wake, Steven Kanumba.

 

Lakini kabla ya hapo, habari za Lulu kutaka kufunga ndoa zilianza tangu mwaka 2012. Mwaka huo kulikuwa na taarifa za Lulu kuvishwa pete ya uchumba na Kanumba. Hata baada ya kifo cha Kanumba, habari za Lulu kutaka kuolewa hazijawahi kukoma kwani mwaka 2013 alidaiwa kupata mchumba wa kuziba pengo la Kanumba, lakini kwa bahati mbaya, mwanaume huyo alidaiwa kufariki dunia.

 

Ulipoingia mwaka 2015 zilianza kusikika tena habari za Lulu kupata mchumba. Katika mitandao ya kijamii umbeya ulisema kuna mfanyabiashara alitaka kufunga ndoa na Lulu. Mwaka 2016, iligundulika kuwa mfanyabiashara huyo ni Majizo aliyetoka kuachana na mwanamitindo Hamisa Mobeto na uhusiano wao ulianza tangu mwaka 2015.

Loading...

Toa comment