The House of Favourite Newspapers

LEBO 7 ZA KIBABE ZINAZOTIKISA AFRIKA

WCB

ENZI zile wakati muziki wa Bongo Fleva unakua, miongoni mwa lebo zilizokuwa zinasimamia kazi za wanamuziki na kutengeneza kazi bora ni pamoja na Bongo Records, MJ Records, Mawingu Studio, Sound Crafters, Empty Souls, Akili Records na G Records.

Hizo ni miongoni mwa lebo zilizoandaa kazi bora. Hata hivyo, pamoja na utitiri huo wa lebo, bado kuna baadhi ya lebo za kibabe ambazo kila mwanamuziki alipenda kufanyia kazi na kama asipopita huko basi aliona kuna kitu kinakosekana kwenye muziki wake. Mfano Lebo ya Bongo Records. Wanamuziki wengi wamekuwa wakiweka wazi kwamba pamoja na kufanya kazi zilizopata umaarufu katika studio mbalimbali enzi hizo, bila kufanya kazi na prodyuza P Funk wa Bongo Records, waliona kuna deni wanalo kwenye muziki.

Unaweza kujiuliza ni kwa nini wanamuziki walipenda kufanya kazi kwenye lebo hii? Jibu lipo wazi kwamba ni kutokana na namna lebo hii ilivyojipatia jina kutokana na kutengeneza kazi bora na kusimamia vyema wasanii mpaka wanafika kwenye ‘main stream’. Sasa kama ilivyokuwa zamani, hata kwa sasa mambo ni vilevile. Kuna lebo kibao Afrika lakini hapa nakudondoshea 7 za kibabe ambazo wanamuziki wengi wangependa kusainiwa ili kufika  mbali zaidi kimuziki.

Wasafi Classic Baby (WCB) ni miongoni mwa lebo za kibabe kwa sasa Afrika. Inatengeneza kazi bora na inasimamia wanamuziki bora wenye hadhi ya kimataifa. Lebo hii inamilikiwa na mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na baadhi ya wanamuziki iliyowasainisha ni pamoja na Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Queen Darleen na Rich Mavoko.

Sarkcess Music

Ukienda nchini Ghana leo hii ukamuuliza mtu yeyote anayefuatilia muziki akutajie lebo kali nchini humo bila shaka jina la kwanza litakuwa ni Sarkcess Music. Sarkcess ni lebo iliyofanikiwa kuvuna jina kubwa ukanda wa Afrika Magharibi kutokana na kutengeneza kazi bora. Inamilikiwa na rapa Sarkodie ambaye anaipeperusha vyema bendera ya Afrika katika gemu la muziki kimataifa na amewahi kufanya kazi na wanamuziki wa kimataifa akiwemo Ace Hood katika wimbo uitwao New Guy. Lebo hii pia inamsimamia mwanamuziki mwingine aitwaye Strongman.

Ambitious Entertainment

Hii ndiyo lebo kubwa nchini Afrika Kusini ambayo wanamuziki wengi wangependa kufanya nayo kazi. Ukisikiliza kazi za wanamuziki wanaosimamiwa na lebo hii ambao ni pamoja na Emtee, Saudi na Sjava utakubaliana nami kwamba hii ni lebo ya kibabe. Ambitious ilianzishwa mwaka 2015 na mfanyabiashara maarufu nchini humo, Kgosi Mahumapelo.

Family Tree

Ukitaja wanamuziki bora kwa sasa Afrika, huwezi kuacha kumtaja  Cassper Nyovest. Jamaa kiukweli anajua na anaipeperusha vyema bendera ya Afrika katika gemu la muziki wa Hip Hop. Cassper ambaye amewahi kufanya kazi na wanamuziki kutoka hapa Bongo, Diamond Platnumz na Vee Money, ndiye mmiliki wa lebo hii ambayo inaifukuza kwa kasi Lebo ya Ambitious. Katika lebo hii mbali na Cassper mwenyewe wanamuziki wengine ambao wanasimamiwa kazi zao ni pamoja na Nadia Nakai, Tshego ma Carpo.

Mavin Records

Kwa sasa Afrika ni vigumu sana kwa mfuatiliaji wa muziki asiifahamu Lebo ya Mavin. Hii ni lebo ambayo ilianzishwa na prodyuza ambaye pia ni mwanamuziki, Don Jazzy akishirikiana na mwanamuziki ‘icon’ D’Banj.

Lebo hii ilianzishwa mwaka 2011 na mwaka 2012, iliongezewa pia jina na kuitwa Supreme Mavin Dynasty. Kwa hiyo inajulikana kwa majina yote mawili ingawa jina la kwanza ndilo maarufu zaidi. Mwanamuziki Tiwa Savage ni miongoni mwa wanamuziki wanaosimamiwa na lebo hii ambapo wanamuziki wengine chini ya hii lebo ni pamoja na Iyanya, Korede Bello, Di’Ja, D’Prince, Dr Sid, Reekado Banks, Johnny Drille, Poe na DNA Twins.

StarBoy Entertainment

Akionyesha kwamba hataki kuachwa nyuma, kutokana na mafanikio aliyoyapata kwenye gemu la muziki, Wizkid mwaka 2013, aliamua kuanzisha lebo yake hii ya StarBoy Entertainment. Hii ilikuwa ni baada ya kujiengua katika lebo iitwayo Empire Mates Entertainment (EME), iliyokuwa inamilikiwa na jamaa aliyemta-mbulisha kwenye muziki, Banky W ambaye ni mwanamuziki na prodyuza pia.

 HKN

Kwenye kitu chochote kama hakuna ushindani basi kuna ladha inapungua pia. Ushindani unaamshaamsha zake aisee! Sasa huku Wizkid akiamua kuanzisha lebo yake, hasimu wake mkubwa kwenye muziki Davido naye hakuwa nyuma, aliamua naye kuanzisha Lebo iitwayo HKN (Honourable Kings of New- School), ili waumane vizuri.

Ingawa ilianza kama utani lakini kwa sasa ni miongoni mwa lebo za kibabe Afrika. Inasimamia wanamuziki wengi maarufu Afrika ambao ni pamoja na Davido, B-red, Shina Rambo, Mayourkun, Dremo, Danagog na Deekay.Lakini pia hivi karibuni Davido ameanzisha lebo nyingine iitwayo DMW (David Music Worldwide), ambapo katika lebo hiyo amewavuta Dremo na Mayourkun.

Comments are closed.