The House of Favourite Newspapers

Lema Akata Tamaa ya Rufaa ya Dhamana, Adai Yuko Tayari Kusota Rumande, Kesi Yake Kutajwa Februari Mwakani

lema

NA MWANDISHI WETU, ARUSHA: Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) leo Desemba 2, 2016, amewataka mawakili wake kutokukata rufaa tena huku akiwaeleza kuwa, kwa sasa yupo tayari kuendelea kukaa rumande hadi pale atakapoachiliwa huru.

Akisoma uamuzi  mdogo wa Jaji Fatuma Masengi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Angero Rumisha, alisema kuwa Mahakama imeifuta Rufaa hiyo, kutokana na wakata rufaa kuikata nje ya muda.

Rumisha amesema waomba rufaa walitakiwa kuonesha kusudio  la kukata rufaa ndani ya siku kumi tangu maamuzi ya maombi ya marejeo kutupwa na Mahakama Kuu, yaliokuwa mbele ya  Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Sekela Moshi Novemba 11.

“Hivyo Mwomba rufaa hii Lema kupitia Mawakili wake alitakiwa kuonyesha kusudio au kutoa notisi  kuonesha Mahakama sababu ya kukata rufaa na Novemba  21 walipaswa kukata rufaa lakini wao wamekata Novemba 22 nje ya muda wa kukata rufaa,” alisema.

Amesema kutokana na hivyo, Mahakama imekubaliana na upande wa Pingamizi lililowekwa na upande wa serikali kupitia Wakili Paul Kadushi akishirikiana na Martenus Marandu kuwa Rufaa hiyo haikufuata misingi ya kisheria kuikata sababu hakuna kusuidi la kukata rufaa na kuiomba Mahakama hiyo itupilie mbali rufaa hiyo.

Rumisha alisema baada ya pingamizi hilo kutolewa na upande wa Lema kuomba Mahakama ilitupilie mbali pingamizi hilo kwani rufaa yao ipo ndani ya muda na imewasilishwa kwa hati ya dharura, Rumisha alisema Mahakama ilivyopitia hoja za pande zote mbili imeona rufaa hiyo imeletwa Mahakamani hapo nje ya muda unaotakiwa.

Aidha alisema mbali na nje ya muda pia wakata rufaa hawakuzingatia sheria inavyotaka kuwa ukikata rufaa lazima uanze na kutoa siku kumi za kusudio la kukata rufaa, jambo ambalo wanaifutilia mbali rufaa hiyo.

Nje ya Chumba cha Mahakama

Wakili wake Lema, John Mallya akizungumza na waandisi wa  Habari, amesema wamezungumza na mteja wao mara baada ya maamuzi ya Mahakama hiyo naye amewaomba kutojishughulisha na suala lolote la kukata rufaa, ingawa wao kama Mawakili wanaona bado kuna njia za kufanya hivyo Mahakama za juu.

Lema ambaye alikamatwa Novemba 3 mwaka huu akiwa mjini Dodoma na kusafirishwa hadi Arusha, anashikiliwa katika mahabusu ya Magereza ya Kisongo mjini Arusha, anakabiliwa na tuhuma ya kutoa lugha ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

Mahakama Kuu Arusha imemnyima dhamana Mbunge Godbless Lema, kwa maelezo kuwa mawakili wake walipaswa kuonesha kusudio la kukata rufaa ndani ya siku 10 kabla ya kukata rufaa, hivyo lema amerudishwa tena rumande na kesi hiyo itatajwa tena februari 2, mwakani (2.Feb.2017).

lemaMke wa Mbunge Godbless Lema akimpungia mumewe alipokuwa akirudishwa rumande baada ya kukosa dhamana.

Familia ya Mbunge mbunge huyo (mke wake na watoto) walikuwepo mahakamani hapo na wameonekana wenye hudhuni kubwa wakati wakimuaga baba yao baada ya kukosa dhamana tena leo na kurudishwa mahabusu.

Mke wa Lema Neema Lema akiwa na watoto wake wawili amesema;

“Nashukuru watu wote waliojitokez akuja katika kesi hii, licha ya usumbufu mwingi waliokutana nao ila hawakukata tama, ila kama familia na nilipoongea na mume wangu Lema tumeona kuwa katika kesi hii kuna mtu  anataka Mahakama ifuate maagizo yake, hivyo nasi tumeona aachwe huyo mtu yafuatwe maagizo yake na afanye atakalo, mume wake atakaa Kisongo,”alisema Neema Lema.

Alisema wamekubaliana kutofungua kesi yoyote mpaka hapo huyo mtu atakapoona inafaa kuacha au la, ila wanachofahamu Tanzania hakuna mwenye hati miliki, iwe kiongozi yoyote mwenye cheo chochote watapita tu tawala zao na maisha yataendelea.

Rufaa iliyokatwa na mawakili wanaomwakilisha Lema mahakamani hapo, iliwekewa pingamizi na upande wa wakili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo leo Novemba 2, 2016 maamuzi yake yamefanyika na pingamizi la Mawakili wa serikali limeshinda, kwa hiyo Rufaa ya Lema imetupiliwa mbali.

lema

Wananchi waliojitokeza mahakamani kufwatilia mwenendo wa kesi ya Mbunge Lema walifukuzwa katika maeneo ya mahakama.

Lema hatasherehekea pamoja na familia familia yake sikukuu za Krismasi na mwaka mpya, atakuwa rumande huku familia yake ikiwa na upweke kwa kumkosa baba yao kwenye sherehe za sikukuu hiyo.

halotel-strip-1-1

Comments are closed.