The House of Favourite Newspapers

Lema, Zitto Waishauri Serikali Mkataba DP World “Hatupingi Uwekezaji Bandari”- Video

0

SERIKALI ya Tanzania, imeshauriwa kurekebisha baadhi ya vifungu vinavyolalamikiwa na wananchi katika mkataba wa ushirikiano wa kuendesha bandari ya Dar es Salaam, kati yake na Kampuni ya Dubai Port World (DP World).
Ushauri huo umetolewa Juni 19, 2023, katika mjadala wa kulinda na kuendeleza umoja wa kitaifa wakati wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mjadala huo ulioandaliwa na Kapuni ya Media Brains, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Godbless Lema, amesema nchi inahitaji uwekezaji lakini Serikali inapaswa irekebishe vifungu hivyo, kisha itoke kwa wananchi kueleza maboresho yaliyofanyika.
“Si dhambi kuleta mwekezaji, katika nchi huwezi kukwepa suala la uwekezaji. Dunia yote inafanya kazi kwa ushirikiano. Nchi inahitaji mwekezaji zaidi ya bandarini, kimsingi uwekezaji hakuna mtu anaukataa na hakuna namna Tanzania inaweza kuishi bila nchi nyingine,” amesema Lema na kuongeza:

“Kwenye ibara ya 4(2) ya makubaliano hayo imeeleza vizuri kwamba Tanzania ikitaka ku-adress jambo lolote la uwekezaji kuhusu bandari hawatamwambia mtu yeyote kwanza isipokuwa Dubai. Sasa mkirekebisha haya mambo halafu mkaja mkawaelewesha watu, mkaondoa vitu vyenye mashaka na watu wa kuwaambia wananchi ni wale wenye uweledi…msitume wale wanaocheza sarakasi bungeni watawaharibia,” amesema.

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameishauri Serikali ianzishe kampuni ya ubia kati yake na DP Wolrd, itakayoendesha bandari hiyo badala ya kuiachia kampuni hiyo ya kigeni pekee.

“Hao Dubai Wolrd wao ni public company iko own na state yao ya Dubai, hamuoni kwamba ni vizuri mamlaka ya bandari au taasisi ya bandari iunde port corporate company iingie ubia na DP 50/50 kuwekeza pamoja na kama tunahitaji kina Rostam waweke hela zao hisa ziwekwe DSE wanunue,” amesema Zitto.

Mwanasiasa huyo ameeleza kuwa, si kweli kwamba bandari imeuzwa bali Serikali imeleta mwekezaji kwa ajili ya kuboresha utendaji wa sekta hiyo muhimu katika uchumi wa nchi, utakaosaidia kukuza mapato ya taifa.

“Tumeelezwa kwamba makusanyo yanatarajiwa kutoka Sh. 7 trilioni mpaka 26 trilioni na hayo ni ya wateja tu idara ya forodha, lakini pili hatujaweza kuutumia vizuri uchumi wetu wa jiografia. Sasa hivi tuna fedha za kigeni tunazopata kwenye biashara ya usafirishaji ni Dola 1.9 bilioni na uwezo wetu ni Dola 12 bilioni, inaweza ikakapatikana kwa kuongeza ufanisi bandarini,” amesema Zitto.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Charles Kitima ameunga mkono ushauri wa Zitto akisema “penda usipende, hii bandari ni yetu tunataka kuona tunafanya biashara hata kama tutaonekana hatuna uwezo. Iundwe kampuni itakayokuwa na ubia kama ilivyofanyika katika maeneo mengine ikiwemo NMB.”

Katika hatua nyingine, Kitima ameishauri Serikali kufanyia kazi maoni ya wananchi yaliyotolewa ili kuuboresha mkataba huo kwa maslahi ya taifa.

Naye Mwanahabari mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu, ameshauri wawekezaji wazawa wapewe nafasi katika uwekezaji huo, huku akihimiza uwepo wa uwazi katika utekelezaji wake.

“Suala la Dubai Port na mashirika mengine kutoka nje yanawekeza ndani, sio suala la kukataa au kukubali. Dhana ya kuingiza nguvu, nishati na mitaji ya wawekezaji kutoka sekta binafsi ni aina gani ya uwekezaji. Ningependa ingekuwa na mashirika ya ndani ingekuwa rahisi sana tunajua hawa watanzania hawawezi wakaondoka,” amesema Ulimwengu.

Leave A Reply