The House of Favourite Newspapers

Leo Ndiyo Leo Droo Ndogo Ya Shinda Nyumba Mwinjuma Mwananyamala

0

LEO ndiyo leo katika Viwanja vya CCM Mwinjuma Mwananyamala jijini Dar es Salaam, wakati watu tisa, ambao ni wasomaji wa magazeti ya Global Publishers watakapoibuka kidedea, miongoni mwa maelfu ya waliokata na kujaza kuponi za Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili, ambapo itachezeshwa droo ndogo ya nne.

Mtu mwenye bahati zaidi kuliko wote leo ataondoka akiwa na pikipiki mpya kabisa, ambayo ndiyo zawadi kubwa ya droo hiyo, huku watu wengine nane nao wakibadili maisha yao kwa kutwaa zawadi nono, ambazo ni simu moja ya kisasa, dinner set, seti moja ya televisheni kubwa flat screen na ving’amuzi vitano vya Ting.

Wakati kuponi zote zilizotumwa Makao Makuu ya Global Publishers kutoka kila pembe ya nchi zitaingizwa kwenye droo hiyo ndogo ili kila msomaji aliyejaza kuponi ajaribu bahati yake, kwa wale watakaofika katika Viwanja vya CCM Mwinjuma, watapata upendeleo maalum kwa kuwepo kwa zawadi kibao za sapraizi, zikiwemo fulana za shinda nyumba.

Mr Shinda Nyumba, yule kijana mwenye urefu wa aina yake atakuwepo katika shoo hiyo akitoa maelekezo kadha wa kadha kwa wasomaji watakaojitokeza ya jinsi ya kushiriki bahati nasibu hiyo ambayo imekuwa gumzo nchini.

Akizungumzia droo hiyo itakayoambatana na burudani kutoka kwa wasanii wanenguaji na muziki mkubwa, Yohana Mkanda, ambaye ni Afisa Masoko wa Global Publishers, aliwataka wasomaji kuendelea kukata kuponi kwa vile hakuna ajuaye ni ipi itanyakua zawadi.

“Niwahimize wasomaji wetu kuendelea kusoma Magazeti ya Ijumaa, Uwazi, Championi, Risasi, Amani na Ijumaa Wikienda, kwani kadiri wanavyokata kuponi zao, nafasi ya ushindi inazidi kuwa karibu yao.

“Kama mnavyojua, hii ni bahati nasibu, lolote linaweza kutokea, hampaswi kudharau kwa sababu shilingi mia tano tu inaweza kubadili maisha yako, ni rahisi sana kushiriki mchezo huu.

“Katika magazeti yetu yote, kwenye kurasa za pili zipo kuponi zenye maelekezo ya namna ya kufanya, wakishamaliza kujaza, wanaweza kuzituma kwetu kupitia kwa mawakala wetu waliopo nchi nzima au wale wa Dar es Salaam wanaweza kuja ofisini kwetu, Bamaga Mwenge na kuziweka kwenye ndoo ya kukusanyia kuponi,” alisema Mkanda.

Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili imedhaminiwa na Kampuni ya Tecno Mobile, King’amuzi cha Ting, British School na Kilimanjaro Institute of Technology.

Leave A Reply