The House of Favourite Newspapers

Lipuli wajiandaa kwa mziki wa Kindoki

 

KOCHA wa Lipuli FC, Seleman Matola amejigamba kwamba hawaogopi uwepo wa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kwenye mechi yao watakapokutana kutokana na wao kujiandaa kwa ajili ya kushinda.

 

Lipuli FC watakutana na Yanga katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) ambayo itapigwa Uwanja wa Samora mkoani Iringa. Kabla ya timu hizo kukutana kwenye kombe hilo zilikutana kwenye ligi ambapo Lipuli FC iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Zahera hakuwepo katika mechi hiyo kutokana na kubaki Dar es Salaam. Matola amesema kwamba hata uwepo wa Zahera kwenye mechi hiyo na kipa Klaus Kindoki hauwatishi kwa sababu Yanga inabaki ileile ambayo walicheza nayo katika mechi ya ligi na kitu kikubwa wao wanajiandaa vilivyo kushinda mechi hiyo.

 

Kindoki ndiye aliyepangua penalti za Alliance na kuivusha Yanga kwenye michuano hiyo.

 

“Hii ni mechi ngumu na tunaichukulia kwa uzito mkubwa sana kwa sababu mshindi ndiye anapita kwenda fainali. Hivyo haitakuwa rahisi hata kidogo kwani Yanga watakuja na nguvu kubwa baada ya kuwachapa katika ligi.

 

“Siwezi kusema kwamba uwepo wa Zahera kwenye mechi hi ndiyo utatufanya sisi tuogope kwani Yanga ni ileile tu. Sisi tunaichukulia kwa uzito mechi hii na tutafanya tuwezalo hili tushinde na tusonge mbele,” alisema Matola mchezaji wa zamani wa Simba na Supersport ya Afrika Kusini.

Comments are closed.