The House of Favourite Newspapers

UGONJWA WA KIPINDUPINDU (CHOLERA) KIPINDI HIKI CHA MVUA

KIPINDI hiki cha mvua ni vema watu wakafahamu kwa undani ugonjwa wa kipindupindu ili kujikinga.  Mojawapo kati ya magonjwa yanayohusishwa na umaskini na uchafu wa kupindukia ni ugonjwa wa huu wa kipindupindu. Kipingupindu ni miongoni mwa magonjwa ambayo huathiri jamii maskini zaidi kwa kiasi kikubwa hasa hasa kwenye nchi zinazoendelea.

Mojawapo ya changamoto zinazokabili nchi zinazoendelea ni jamii kutokuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama, pamoja na kutokuwa na mazingira safi kwa ujumla. Ndio maana mpaka leo nchi zinazoendelea ndizo zinazokumbwa na mlipuko wa kipundupindu au huwa katika hatari ya mlipuko wa ugonjwa huo kwani wengi hunywa maji ya kisimani.

Ugonjwa huu hutokana na maambukizi katika utumbo mdogo wa binadamu uletwao na vimelea vya bakteria vijulikanavyo kitaalamu kama Vibrio cholerae. Kwa kawaida vimelea hawa hupendelea kuishi katika kinyesi cha binadamu. Mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa huu kwa kunywa maji ama chakula kilichochafuliwa na kinyesi chenye vimelea hivi vya kipindupindu.

Mara baada kula chakula au kunywa maji yaliyochafuliwa, baadhi ya vimelea hivi huuawa kwa tindikali iliyopo kwenye tumbo (stomach) pindi chakula au maji haya yanapoingia tumboni. Hata hivyo, baadhi ya vimelea hawa hufanikiwa kukwepa ukali wa hii tindikali na hivyo kuendelea kuishi kwenye utumbo.

Vimelea waliofanikiwa kuepukali tindikali ya tumbo la binadamu, hujongea kwenda kwenye ukuta wa utumbo mdogo. Wawapo kwenye ukuta wa utumbo mdogo Vibrio cholerae hutoa sumu iitwayo CTX au CT (cholera Toxin) ambayo husababisha mtu kuharisha choo chenye majimaji, papo hapo  huzaliana na vimelea hao hutoka nje kwa njia ya haja kubwa. Iwapo choo hicho cha mtu aliyeambukizwa kipindupindu kitachanganyika na chanzo cha maji au chakula, watu wengine wakila au kunywa maji hayo huambikizwa kirahisi.

Hali kadhalika iwapo ni kwenye choo ambacho hakipo kwenye mazingira ya usafi kuna hatari ya choo cha mwambukizwa kuchanganyika na chanzo cha maji au chakula na hivyo kusababisha watu wengi zaidi kuambukizwa ugonjwa huu. Dalili za kipindupindu

Dalili za mwanzo kabisa za kipindupindu ni: Kuanza kuharisha ghafla choo chenye majimaji ambacho rangi yake ni kama maji ya mchele na chenye harufu mbaya kama shombo ya samaki, na kutapika. Aidha mgonjwa wa kipindupindu huonesha dalili zakupungukiwa maji mwilini kama vile, ngozi huwa kavu, midomo kukauka, mgonjwa kuhisi kiu kikali, machozi kutoweza kutoka, kupata mkojo kidogo sana, kuishiwa nguvu na kujisikia mchovu sana na macho kutumbukia ndani hasa kwa watoto.

Kwa kawaida kipindupindu huweza kugunduliwa na kutambuliwa kwa kutumia dalili hizo. Hata hivyo, ili kuthibitisha kuwa mlipuko uliotokea ni kweli kipindupindu, vipimo vifuatavyo huweza kufanyika.

Kupima damu kwa ajili ya kuotesha vimelea vya kipindupindu maabara, kuchunguza choo kwa kutumia darubini (dark field microscope) ambapo vimelea hivi vya V. cholerae huweza kuonekana.

Tiba ya Kipindupindu Lengo kuu katika kutibu kipindupindu ni kurejesha maji na madini mwilini mwa mgonjwa kwa kumpatia maji maalum yenye madini hayo kwa kumpa anywe au kwa njia ya mshipa wa damu ambayo kitaalamu huitwa intravenously (i.v)

Maji ORS yanaweza kutengeneza nyumbani kwa kadiri ya muongozo kwa kuchanganya lita moja ya maji safi na salama na vijiko vidogo vinane vya sukari, kisha ongeza kijiko kidogo kimoja cha chumvi. Aidha, unaweza kuongeza nusu glasi ya juice ya machungwa au nusu ya ndizi (tunda) lilipondwapondwa kwa kila lita, ili kuongeza madini ya potassium na pia kuboresha ladha.

Kwa wagonjwa wenye hali mbaya na wale wasioweza kunywa wenyewe, daktari atawapa maji yenye madini mbambali kwa njia ya mshipa wa damu. Maji haya huitwa kitaalamu Ringer’s Lactate. Baadhi ya dawa ambazo hutumika katika matibabu ya ugonjwa huu ni Azithromycin naTetracycline.

USHAURI

Matumizi ya dawa (antibayotiki) husaidia tu kufupisha muda wa kuwatoa wadudu na wala isitumike kama tiba kuu ya ugonjwa huu. Ni vema kunywa maji yatokayo kwenye bomba yaliyochemshwa kipindi hiki cha mvua.

Comments are closed.