The House of Favourite Newspapers

Lissu: Hakuna Mwenye Mamlaka ya Kunivua Utanganyika

BAADA ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai,  kusema Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amepoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge, mwanasiasa huyo ambaye anaendelea kuuguza majeraha ya risasi ughaibuni amesema atakwenda mahakamani kupinga uamuzi huo.

 

Lissu akiwa Ubelgiji, amesisitiza kuwa, tangu aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa Area D jijini Dodoma Septemba 7, 2019,  amekuwa akipata matibabu nje ya nchi.

 

Amesema kwa hatua ya sasa, “Nitawasiliana na wanasheria wangu haraka iwezekanavyo ili kuona cha kufanya lakini Septemba 7 (mwaka huu) ambayo nilikwisha kusema nitarudi sitabadili, nitarudi na alichokifanya Ndugai ni kukoleza mjadala.”

 

Jana Ijumaa, Spika Ndugai aliliambia Bunge hilo kuwa amemwandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kumjulisha kuwa kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kipo wazi.

 

Amesema hatua hiyo inatokana na Lissu kutojaza taarifa za mali na madeni na sababu ya pili kutotoa taarifa kwa Spika mahali alipo.

 

Mara baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, mwaka 2017, jijini Dodoma, mwanasiasa huyo alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na usiku wa siku hiyo akahamishiwa hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambapo alipatiwa matibabu hadi Januari 6, mwaka jana na kisha kuhamishiwa nchini Ubelgiji hadi leo.

 

“Kuna siku nilisema hao wanaoitwa ‘watu wasiojulikana’ waliotaka kuniua watajidhihirisha tu. Sasa maneno hayo yametimia. 

Kwa maneno yake mwenyewe, Spika Ndugai alisema atakuja kuniangalia hospitalini Nairobi au kokote nitakapokuwa nimehamishiwa. Hakuja hospitalini Nairobi au Ubelgiji, lakini alikuwa anajua niko wapi kwa muda wote ambao nimekuwa nje ya Bunge. 

Mwezi Machi mwaka jana, Katibu wa Bunge alimwandikia barua kaka yangu, Wakili Alute Múghwai, kuhusu matibabu yangu. Barua hiyo ilinakiliwa kwangu nikiwa nimelazwa hospitalini UZ Leuven, na pia kwa Spika Ndugai. Kama Katibu wa Bunge alikuwa anajua niliko, Spika wa Bunge anawezaje kusema hajui niliko???

 

Nimelipwa mshahara na posho za kibunge tangu September 7 mpaka sasa, mwaka mmoja na miezi tisa. Sijawahi kuhudhuria kikao hata kimoja au mkutano mmoja wa Bunge katika kipindi hicho.

Je, Bunge na Spika Ndugai walikuwa wananilipa mshahara na posho za kibunge bila kufahamu nilipo na sababu gani nipo huko???

Kweli???

 

Nikiwa hospitalini Nairobi nilitembelewa na Makamu wa Rais, Samia Suluh Hassan, aliyesema ametumwa na Rais Magufuli kuja kunijulia hali. Baada ya kuhamishiwa Ubelgiji nilitembelewa na Balozi wa Tanzania Ubelgiji. Kama, baada ya yote haya, Spika Ndugai bado hajui niliko basi ni shida kubwa.

 

Lakini anachokisema Spika Ndugai sio cha ajabu. Hii ndiyo Tanzania ya Magufuli. Magufuli alimwambia Spika Ndugai atufukuze bungeni ili tushughulikiwe nje ya Bunge. Huu ndio utekelezaji wa maagizo ya Dikteta Uchwara. 
Nitarudi nyumbani September 7 kumkabili Dikteta Uchwara.

 

Mimi ni Mtanzania na ni Mtanganyika. Hakuna mwenye mamlaka ya kunivua Utanganyika na Utanzania wangu. Nitarudi nyumbani September 7, regardless of what these cowards decide!!!,” AMEANDIKA TUNDU LISSU.

 

BREAKING: TUNDU LISSU Avuliwa UBUNGE, SPIKA Atangaza-” Jimbo Liko Wazi”

Comments are closed.