The House of Favourite Newspapers

NEC: Walioko Nje Ya Nchi Hawataweza Kupiga Kura – Video

0

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema mpaka sasa, sheria zilizopo haziruhusu Mtanzania aliyeko nje na nchi kuweza kupiga kura.

Hayo yamesemwa mapema leo Juni 2, 2020 na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa NEC, Emmanuel Kawishe kupitia kipindi cha Front Page kinachorushwa na +255GlobalRadio.

Akijibu swali lililoulizwa na Mtanzania aliyeko Falme za Kiarabu, Kawishe alisema sheria zilizopo haziruhusu Watanzania kupiga kura wakiwa nje ya nchi hivyo kwa kuwa suala hilo limekuwa likilalamikiwa, pengine huko mbeleni linaweza kufanyiwa kazi.

 

“Mpaka sasa sheria yetu inasema mtu atapiga kura pale alipojiandikisha. Hivyo kwa wenzetu waliopo nje sheria haijatamka. Kwa kuwa ni malalamiko ya muda mrefu, labda huko baadaye sheria itarekebishwa lakini kwa uchaguzi huu tutaendelea na sheria hii tuliyonayo,” alisema Kawishe.

Akizungumzia kuhusu wasimamizi wa uchaguzi kuteuliwa na Rais ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi na kutoa tafsiri kwamba huenda wakapendelea chama hicho tawala, Kawishe alisema wasimamizi hao hula kiapo maalum kinachowaongoza kutenda haki.

“Kuna fomu namba 6 ya kiapo cha siri au fomu namba 7 ya kiapo cha kujitoa kuwa na chama cha siasa hivyo utaona ni jinsi gani ni vigumu kupendelea na wanaokiuka huwa tunawaondoa mara moja,” alisema na kuongeza.
“Rais huwa anawateua majaji, mbona huwa hawalalimiki kwamba ameteuliwa na mwenyekiti wa CCM.

Hata wanaolalamikia kwenye vituo vya kupigia kura, kwenye kila kituo cha kupigia kura kuna wakala. Mawakala wote wana haki sawa, akiingia kituoni kuna fomu anasaini kujiridhisha kwamba amekagua masunduku yote hayana kitu chochote.”

Kawishe pia alisema kwa hapa nchini watu wamekuwa wakitoa malalamiko mengi wakidhani kwamba ni Tanzania pekee inayotumia mfumo wa wakurugenzi kusimamia uchaguzi akasema ni jambo la kawaida na kuna nchi zinatumia mamea.

 

“Mimi nimeenda Uingereza, wanaosimamia uchaguzi ni mamea hivyo kikubwa ni utaratibu wa jinsi ya kusimamia tu sheria. Rais anawateua majaji, mbona huwa hawalalimiki kwamba ameteuliwa na mwenyekiti wa CCM,” alisema Kawishe.

Kawishe alimalizia kwa kuwataka viongozi wa siasa kudumisha umoja na mshikamano katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

“Kwa niaba ya Tume niwaombe viongozi wa siasa Tanzania ni yetu wote. Tunaomba ushirikiano, tume itatenda haki kwa watu wote,” alisema.

Kuyapata mahojiano zaidi na kusikiliza vipindi vingine live, itafute 255GlobalRadio kwa kupakua App ya Global Publishers kwenye simu janja.

Leave A Reply