The House of Favourite Newspapers

Haji Manara Afunguka Mazito Baada ya Kuondoka Simba – Video

0

ALIYEKUWA msemaji wa Simba, Haji Manara  leo Agosti 4, 2021 amedai kuwa ilimladhimu kulala kwenye kochi wakati kikosi cha timu hiyo kiliposafiri nchini Afrika Kusini kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Manara alidai sababu kubwa ya kulala kwenye kochi ni kutokana na kutopewa kipaumbele na mabosi wa timu hiyo.

 

“Nimefanya kazi ya kujitolea kwenye hii klabu mpaka kufikia hatua ya kusafiri kwa gharama zangu mwenyewe bila hata kupewa na uongozi, chochote kitu hii ni kuonyesha kabisa ni jinsi gani uongozi wa sasa umekuwa ukinifanyia vitu vya kinyama na nisivyotarajia” alisema.

 

Katika hatua nyingine Manara alidai kuwa hata safari za nje ya nchi pindi Simba inaposafiri amekuwa akitumia fedha zake binafsi kwa sababu ya kutowekwa kwenye orodha ya viongozi wanaosafiri na timu.

 

“Sina mkataba kwa miaka sita watu wanakuja wanapewa mikataba mie naachwa, sina promotion, laki saba hiyo hiyo imesimama kama mbuyu tangu 2015, nilikubali kwa sababu ni Simba yangu. Naipenda hii klabu namwachia nani?”

 

“Wakati Senzo anakuja kwa mara ya kwanza, alinifuata na kuniambia amepewa kazi ya kunifukuza Mimi kazi, lakini Senzo alihoji kwanini nimfukuze bila sababu?”

 

“Kifupi walimleta Senzo ili atekeleze matakwa ya wakubwa ila Senzo alisimama imara sana, alipinga kufanya kitu bila kukichunguza na ndicho kilichomuondoa Simba.”

 

“Simba inacheza nje ya Dar, msemaji wa timu sikatiwi tiketi. Naenda kwa kujitegemea nauli na hoteli. Hadi mechi za nje ya nchi. Nilishawahi kwenda South Africa kwa nauli yangu klabu ilishindwa kunilipia hata hotel, Nikalala kwenye kochi.”

 

“Shida zote nilizopata na Simba, hawa watu hawaniheshimu, hawana mkataba na mimi. Majungu yote wananifanyia sasa leo wananipa jungu jipya la kuhujumu yani mimi nikahujumu Simba? Nahujumu vipi naenda kwenye camp ya Yanga? Nawaambiaje?”

 

“Kuna siku Mohammed Dewji ‘MO’ alininipigia simu akaniambia watu wananilalamikia kuwa wewe umekuwa maarufu kunizidi mimi. Nikamwambia mie nitafanyeje? Nitawazuia watu? Kwani najipa mwenyewe umaarufu? Akaniambia watu wanasema tukutoe nikamwambia nitoeni”

 

“Kwa nini leo sipo Simba? Sababu ni mbili, biashara na umaarufu. Haji ameathirika na hayo mambo mawili. Ndiyo maana unasikia inarudiwa mara nyingi kwamba hakuna mtu mkubwa zaidi ya klabu, lini mimi nimesema ni mkubwa kuliko klabu?”

Leave A Reply