The House of Favourite Newspapers

Rais Samia Aruhusu Mikutano ya Hadhara kwa Vyama vya Siasa Nchini-(Picha +Video)

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi wa Vyama Vya Siasa kuhusiana na maamuzi ya Serikali ya kuruhusu kufanyika kwa Mikutano ya Hadhara kwa Vyama hivyo wakati wa Kikao kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 03 Januari, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Januari 3, 2023 ameondoa rasmi tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara na kuruhusu vyama vya siasa kuanza kufanya mikutano hiyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni

Rais Samia ametoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es salaam wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa nchini ambapo amesema ni haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na kuwataka kutumia nafasi hivyo kufanya siasa za kistaraabu na za kujenga badala ya kubomoa nchi

“Wajibu wenu vyama vya siasa ni kufuata sheria na kanuni zinavyosema, lakini kama waungwana na wastarabu niwaombe sana tunatoa ruhusa ya mikutano, twendeni tukafanye siasa za kistarabu, za kupevuka na kujenga na si kubomoa”

Aidha Rais Samia amesisitiza kuwa utaratibu wa kufanya mikutano hiyo utaendelea kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi ili kupata vibali huku akisema kwa hali ilivyo sasa vibali hivyo vitaruhusiwa

Sehemu ya Viongozi mbalimbali wa Vyama Vya Siasa 19 waliohudhuria Kikao kilichoitishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Ikulu Jijini Dar es Salaam Dar es Salaam tarehe 03 Januari, 2023.

“Ni haki kwa vyama vya siasa kuendesha mikutano yao ya hadhara, lakini ndugu zangu tuna wajibu, kwa serikali wajibu wetu ni kulinda mikutano ya vyama vya siasa, mnatupa taarifa kama sheria inavyosema, vyombo vinatoa ruhusa, wakiona kuna hatari hawatoi ruhusa, lakini kwa hatua tuliyofika ruhusa za kufanya mikutano zitatolewa”

Katika hatua nyingine Rais Samia amesema hivi karibuni ataunda kamati maalumu kwa ajili ya kushauri kuhusu marekebisho ya katiba mpya na njia bora ya kuliendea jambo hilo huku akisisitiza kuwa mchakato huo utakuwa wa kistaraabu ili kupata katiba bora ya watanzania.

Rais Samia akizungumza jambo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya Kikao na Viongozi wa Vyama vya Siasa Ikulu.
Rais Samia akiwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) George Simbachawene, Msajili wa Vyama vya Siasa  Jaji Francis Mutungi, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Mohammed Ally Ahmed pamoja na viongozi wa Vyama Vya Siasa mara baada ya Kikao Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 03 Januari, 2023.

Leave A Reply