Kartra

Rais Samia: Corona Imetupiga, Gharama Kubwa Hatuwezi – Video

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameitaka mamlaka zinazoshughulikia zoezi la sensa lililopangwa kufanyika mwakani 2022 kutumia gharama ndogo na kufanya zoezi hilo kwa ufanisi kwani Serikali haina pesa ya kubeba gharama kubwa.

 

Rais Samia amesema hayo leo Jumanne, Septemba 14, 2021 wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya uelimishaji na uhamasishaji kuhusu sensa ya mwaka 2022 inayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

“Suala la #Sensa linatambulika kwenye dini zetu zote mbili na viongozi wetu wa dini wameyasema hapa. Hii inadhihirisha #Sensa imekuwepo duniani kwa miaka mingi.

 

“Sensa ya kwanza hapa kwetu ilifanyika mwaka 1910 wakati wa Utawala wa Ujerumani, ili kufahamu nguvu kazi iliyopo nchini. Sensa ya kwanza ya Kisayansi ilifanyika mwaka 1967 baada ya nchi zetu mbili kupata uhuru na kuungana.

 

“Mjitahidi kutumia mbinu na nyenzo zote kuwafikia wananchi kote waliko na kwa rika zote, ikiwemo vipindi vya radio na televisheni, magazeti, wasanii wetu na wanamuziki, njia za TEHAMA kupitia mitandao ya kijamii, meseji za simu, n.k.

 

“Taarifa za Sensa zitatusaidia kufahamu ongezeko la idadi ya watu katika nchi na hali ya uhamiaji, mfano kutoka vijijini kuja mjini na wale wanaotoka nje ya nchi, pia kupima maendeleo yaliyofanyika tangu sensa ya mwisho.

 

“Zoezi hili mfanye kwa ufanisi ikiwemo kumaliza kwa wakati na kwa kutumia gharama ndogo, kama mnavyojua nchi yetu imepigwa na wimbi la corona kwa hiyo uwezo wa kubeba gharama umepungua. Ninaamini zoezi hili litafanyika kwa gharama ndogo na kukidhi matarajio.

“Ni imani yangu kuwa endapo mkakati huu utafanyika kikamilifu, basi wananchi watahamasika kuhesabiwa na kupata idadi kamili kwa ajili ya maendeleo yetu.

“Taarifa za #Sensa zinatumiwa pia na taasisi za Kimataifa, taasisi za kiraia, pia wawekezaji hutumia taarifa hizi kuamua ni aina gani ya biashara kuwekeza na wapi, watafiti wa ndani na nje ya nchi hutumia taarifa za sensa kwa ajili ya tafirifa,” amesema Rais Samia.

 


Toa comment