Kartra

Harmonize Achafua Hali ya Hewa Marekani

 

STAA wa Bongo Fleva, Harmonize au Konde Boy Mjeshi anaendelea na ziara ya takriban miezi miwili katika majimbo mbalimbali ya nchini Marekani na tayari amefanya shoo kadhaa kwenye Miji ya Ohio na Arizona.

 

Lakini mbali na hilo, wikiendi iliyopita, Harmonize alichafua hali ya hewa baada ya kujilipua na pete, cheni na saa mpya; vyote vya madini ya almasi vikitajwa kuwa na thamani kubwa mno na kusababisha mjadala mkali kwa upande wa pili wa mahasimu wake.

Vitu hivyo vyote vimemfanya Konde Boy Mjeshi kuchafuka kwa almasi kuanzia shingoni, mikononi na kwenye vidole huku mwenye akitamba kutumia mamilioni ya pesa kwa ajili ya vitu hivyo.

 

Katika video ambayo ilimuonesha akiwa amevaa vitu hivyo akivisifia kuwa ni orijino kabisa, moja ya cheni hizo aliyoivaa shingoni inaonekana ikiwa na picha ya kichwa cha mtu ambacho machoni kinawakawaka mataa hivyo akiwa kwenye giza anaonekana yeye tu.

ISHU NI KUVAA MSALABA

Lakini kubwa lililojitokeza na kuibua tafrani ni kichwa hicho kilichopo kwenye cheni hiyo ambacho kinaonesha sura ya Yesu na lile taji la miiba ambalo alivalishwa na msalaba wakati ule alipokuwa akisulubiwa msalabani yapata miaka elfu mbili iliyopita.

 

Mjadala mkubwa umekuwa ni juu ya Harmonize kuvaa kwake cheni yenye msalaba bila kufahamu ni nini anamaanisha ilihali ni mtoto wa Kiislam na ni kinyume na imani ya dini yake.

 

Hoja kubwa imekuwa ni kwamba, Harmonize kuvaa msalaba anakubali kuwa Nabii Isa alisulubiwa wakati Waislam wanaamini Isa hakusulubiwa.

 

Wengine wanasema labda ana mpango wa kubadili dini na kuwa Mkristo au ni mihemko tu ya ujana huku baadhi ya wajuzi wa mambo ya imani wakisema msalaba hauna uhusiano wowote na mambo ya imani.

“Harmonize anakosea sana kuvaa misalaba. Siyo vyema kwa dini yake. Kama anapenda kuvaa misalaba namshauri abadilishe dini. Ni vyema kuheshimu dini yako na dini za wengine na daima tudumishe upendo licha ya tofauti za kiimani tulizonazo.”

 

“Sijaona kosa la Harmonize, mbona Wakristo wengi tu wanavaa kofia za Kiislam na pia wanasalimia asalaamu aleikumu na Wakristo wanaitikia aleikumu msalamu,” Yalisomekana baadhi ya maoni ya video ya Harmonize aliyoiachia kupitia Insta Story yake.

HARMONIZE ANAMUIGA DIAMOND?

Hata hivyo, suala kama hilo liliwahi kumkuta aliyekuwa bosi wa Harmonize, Diamond Platnumz ambaye naye amekuwa na kasumba ya kuvaa misalaba na kusababisha baadhi ya mashehe kumwambia anatoka nje ya mstari wa dini yake ya Kiislam.

 

Hata hivyo, katika majibu yake, Diamond amekuwa akijibu hachukulii cheni hiyo kama msalaba, bali ni alama ya jumlisha ambayo kwake ina maana kubwa ambayo ni siri yake.

“Cheni ninayovaa na watu kunidisi kwamba ni msalaba, kiukweli huwa ninashangaa sana kwa maana watu huzungumza kile ambacho hawakifahamu.

 

“Kwangu huo si msalaba, bali ni alama ya jumlisha ambayo ninaona haina tatizo lolote, kwani alama hiyo ina maana kubwa kwangu ambayo itabaki kuwa siri yangu!” alisema Diamond.

STORI; MWANDISHI WETU


Toa comment