The House of Favourite Newspapers

Lukuvi Afuta Hati Yenye Mgogoro wa Miaka 14

0

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ameamuru kuondolewa katika daftari hati ya kitalu namba 153 na eneo hilo kupatiwa wananchi 74 waliokuwa katika mgogoro katika kata ya Mhandu, Nyamagana mkoani Mwanza.

 

 

Akitoa uamuzi huo jana wilayani hapa wakati wa ziara yake kwa ajili ya kutatua mgogoro wa eneo hilo uliodumu kwa takriban miaka 14, Lukuvi alisema hati ya mtu anayedaiwa mmiliki wa eneo hilo anayetambulika kwa jina la Abdallah Maliki, ilitakiwa kufutwa muda mrefu kwa kuwa hajalipia kodi ya pango la ardhi kwa miaka 15.

 

 

“Hati miliki ikaondolewe katika daftari la hati na jaji amethibitisha katika uamuzi wake kuwa wamiliki wa asili katika eneo hili hawakulipwa fidia,” alisema Lukuvi.

 

 

Waziri aliongeza kuwa kutokana na uamuzi huo, sasa wananchi wa eneo hilo watatakiwa kupimiwa kulingana na ukubwa wa eneo analomiliki na kila mmiliki atatakiwa kulipa tozo ya mbele asilimia 2.5 kufidia gharama ambayo mmiliki wa awali alishindwa kulipa kodi ya pango.

 

 

“Huyu mtu ameshindwa kuendeleza kwa wakati na hajalipa kodi kwa miaka 15. Sasa wananchi wapimiwe na kupatiwa eneo bila fidia. Huwezi kupewa eneo una hati watu 70 wanajenga miaka 15 wewe una hati umekaa nayo tu,” alisema Lukuvi.

 

 

Kwa mujibu wa Lukuvi, serikali itahakikisha inalinda hati ya mmiliki wa ardhi huku mmiliki akitakiwa kulinda eneo lake na kusisitiza kuwa hati ya ardhi ni dhamana na ndiyo inayotoa usalama wa mmiliki.

 

 

“Mtu hajaonekana halafu atoe kibali cha kuvunja nyumba. Sheria hairuhusu umilikishaji juu ya hati nyingine ndiyo maana nimeamua kuifuta kwanza hati hii ndiyo hati nyingine isajiliwe,” alisema.

 

 

Pia aliagiza eneo lingine kitalu Na. 154 linalokaliwa na wananchi 40 na kumilikiwa na Abdulkarim Mbaga, mmiliki wake apelekewe ilani ya siku 90 kabla ya hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi ya eneo lake.

 

 

Akiwasilisha mgogoro huo mbele ya Waziri, mwakilishi wa wananchi wa Kata ya Mhandu Sokoni, Kazimiri Shimbi, alisema muda mrefu wananchi wa eneo hilo wamekuwa katika mgogoro wa ardhi wakishtakiwa na mtu wasiyemjua jambo lililosababisha kushindwa kurasimishiwa makazi katika eneo hilo kwa madai ya kuvamia eneo.

 

 

Kwa mujibu wa Shimbi, wananchi hao mara kadhaa wamekuwa wakishinda kesi mahakamani dhidi ya mdai.

Leave A Reply