The House of Favourite Newspapers

Lulu Aibua Balaa Gerezani, Mastaa ni Vilio Tu

0
Staa ‘grade one’ wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ (katikati). Picha na Maktaba.

 

Habari kubwa iliyojiri mapema wiki hii ni kuhusu hukumu ya kifungo cha miaka miwili jela inayomhusu staa ‘grade one’ wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ kufuatia kesi iliyokuwa ikimkabili ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa mwigizaji mwenzake, marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’.

TUJIUNGE GEREZA LA SEGEREA

 

Mara baada ya hukumu hiyo, mapokezi ya Lulu yalidaiwa kuzua balaa katika Gereza la Segerea jijini Dar kwa wafungwa wenzake ambao walipigwa na butwaa kusikia staa huyo ameingia gerezani hapo.

 

Kwa mujibu wa shuhuda wetu ambaye alikuwa mahabusu siku ya Jumatatu wakati ‘difenda’ lililombeba Lulu mara baada ya hukumu hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, mrembo huyo aliibua tafrani kutokana na kila mfungwa kutaka kumuona kwa mara nyingine.

ALISHASOTA SEGEREA

Ikumbukwe kuwa, Lulu alirejeshwa kwenye gereza hilo kwa mara nyingine baada ya kukaa hapo kwa zaidi ya miezi nane alipokuwa mahabusu mara tu baada ya kutokea kwa kifo cha Kanumba kabla ya baadaye kuachiwa kwa dhamana. Shuhuda huyo alieleza kwamba, wakati akiingizwa gerezani hapo, wafungwa hao waliacha shughuli zao kwa muda wakitaka kumuona na kumshangaa Lulu kabla ya kuamriwa kuendelea na shughuli zao.

 

“Lulu ni staa mkubwa, kama ambavyo huwa watu wanamshangaa anapokuwa mitaani au kwenye shughuli mbalimbali za hadhara, ndivyo ilivyokuwa gerezani, lakini walitulia baada ya kuamriwa kuendelea na majukumu yao na Lulu kuingizwa sehemu aliyotakiwa kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kuwepo kwake gerezani hao,” kilitiririka chanzo hicho.

 

NENO LA KAJALA

Akizungumza na gazeti hili mara baada ya hukumu hiyo, staa mwenzake wa sinema za Kibongo, Kajala Masanja ‘Kay’ aliyewahi kukaa naye mahabusu gerezani hapo alisema kuwa, anamhurumia Lulu kwenda mahali hapo kwa namna maisha ya gerezani yalivyo. “Jamani hakuna kitu kibaya kwa mwanadamu kama kunyimwa uhuru kama ilivyo kukaa gereza.

Hakika Lulu amekwenda pabaya, ninamsikitikia mno kwa sababu mimi napajua Segerea,” alisema Kajala aliyekaa Segerea kwa zaidi ya mwaka mmoja alipokuwa akikabiliwa na kesi ya kuuza nyumba iliyowekewa kizuizi na Takukuru baada ya mumewe, Faraji Agostino kukabiliwa na kesi ya utakatishaji wa fedha.

 

MASTAA WAMLILIA

 

Mastaa wengine waliomlilia Lulu baada ya kupigwa mvua mbili gerezani ni pamoja na Snura Mushi ambaye alisema amesikitishwa sana na hali iliyomkuta muigizaji huyo. “Hili siyo tukio la kufurahisha, lakini ndiyo hivyo hatuwezi kushindana na sheria, iliyobaki ni kumuombea tu kwa Mwenyezi Mungu ampe wepesi wa kila jambo,” alisema.

 

Kwa upande wake, Shamsa alisema; “Lulu ni mdogo wangu, msichana mwenzangu na msanii mwenzangu, katika maisha kila jambo lina changamoto zake, lakini kila kitu kitapita, tunamuombe Mungu ampe wepesi,
tutaendelea kumpa kampani, tutakuwa tunaenda kumtembelea mara kwa mara,” alisema.

 

Mahsen Awadh maarufu kama Dk Cheni naye alionyesha masikitiko yake kwa tukio lililomkuta msanii mwenzake, na kusema jambo hilo siyo dogo, ingawa wapo watakaofurahi na kuhuzunika. “Hili siyo jambo la kufurahia, hakuna mtu anayeijua kesho yake, haya ni mapito na yote tumwachie Mwenyezi Mungu,” alisema.

 

Mastaa wengine waliotoa maneno ya huzuni kufuatia hukumu hiyo ni Wastara Juma, Wema Sepetu na wengineo kibao. Wakati huohuo, msanii Hamisa Mabeto ambaye amezaa na mpenzi wa Lulu, aliwashangaza wengi kwa kuongoza maombi baada ya kuandika katika akaunti yake ya Instagram maneno ya kumfariji Lulu, akimuomba Mungu kumsimamia na kumtia nguvu. “Mwenyezi Mungu ampe nguvu mama yako na mdogo wako Iki katika kipindi hiki, sijui kama nitaweza kumuona bila kutoa machozi, haya yote ni mapito tu,” aliandika Mobeto.

 

TUMEFIKAJE HAPA?

Kifo cha Kanumba kilitokea Aprili 7, 2012, nyumbani kwake, SinzaVatican jijini Dar na mazishi yake kufanyika kwenye Makaburi ya Kinondoni. Lulu ndiye mtu wa mwisho aliyekuwa na marehemu chumbani kwake na ndiye aliyewaita watu wengine baadaye. Wakati tukienda mitamboni, Wakili wa msanii huyo Peter Kibatala aliyekuwa akimtetea, alisema atakata rufaa Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu hiyo.

NA MWANDISHI WETU | RISASI JUMAMOSI

Leave A Reply