The House of Favourite Newspapers

Lundenga: Najivunia Kutengeneza Mastaa!

0

KWA takriban miaka 26 sasa tangu mwaka 1994, Shindano la Miss Tanzania limechangia kukuza utamaduni, utalii na uwekezaji kwenye urembo na mitindo nchini, hivyo kutoa ajira.

 

Achana na hayo, shindano hili limewapa fursa warembo kujitambua na tunawaona wakifanya vizuri kwenye nyanja mbalimbali ndani na nje ya nchi.

 

Washindi na washiriki wengi wa Miss Tanzania, wanapata fursa ya kushiriki harambee za kupata fedha kwa ajili ya watu wasiojiweza. Itoshe kusema wanakuwa watumishi wa jamii. Hata hivyo, huwezi kuzungumzia Shindano la Miss Tanzania bila kumtaja mtu aitwaye Hashim Lundenga ‘Uncle’.

 

IJUMAA limefanya mahojiano maalum (exclusive) na Lundenga, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency Limited iliyokuwa ikiratibu shindano la Miss Tanzania, kabla ya kustaafu mwaka 2018 na kumuachia kijiti Miss Tanzania 1998, Basila Mwanukuzi.

 

Katika mahojiano na Lundenga, mbali na kueleza shindano hilo lilivyopita kwenye changamoto nyingi, pia anajivunia kutengeneza warembo mastaa wengi Bongo na sasa ameamua kupumzika kwani amezeeka (bila kutaja umri alionao);

 

IJUMAA: Wazo la kuanzisha Miss Tanzania, ulilipata wapi?

LUNDENGA: Nakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 1990, nilikuwa ninasafiri sana kwenda Nairobi (Kenya) kwa sababu wanangu walikuwa wanasoma huko. Nikiwa kule nilikuwa ninashuhudia mashindano ya urembo na watu wakawa wanakwenda kushiriki Miss World.

 

Nilifanya utafiti juu ya urembo na mashindano yake ndipo nikaamua kuanzisha Miss Tanzania.

Historia ya Miss Tanzania ni ndefu kidogo. Shindano hili lilipigwa marufuku hapa nchini mwaka 1968 wakati wa mfumo wa chama kimoja. Umoja wa Vijana wa Chama cha Tanganyika African National Union (Tanu) ulilisitisha kwa kisingizio kuwa yalikuwa yanaharibu utamaduni wa Kitanzania hasa kimavazi.

 

Mwaka 1993 niliandaa muswada wa kuanzisha upya Miss Tanzania, lakini kwa mwaka huo sikufanikiwa kupata kibali. Nilipata kibali mwaka 1994 Miss Tanzania ikaanza rasmi. Kwa kipindi hicho hatukufanikiwa kushiriki Miss World hadi mwaka 1997.

 

IJUMAA:

Unaizungumziaje Miss Tanzania ya zamani ukilinganisha na hii ya sasa?

LUNDENGA: Ya zamani ni ya zamani na ya sasa ni ya sasa. Sivyo sitaki kuonekana ninajipendelea na kuwaponda wenzangu.

IJUMAA: Uongozi wako ulikumbwa na skendo za hapa na pale. Miongoni mwazo ni kuwa zawadi za washindi zilikuwa hazitolewi kama ilivyotakiwa, je, unalizungumziaje hilo?

 

LUNDENGA: Tangu nilipoanzisha Miss Tanzania, ni mwaka mmoja tu ambao nilikutana na tatizo hilo. Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1997 kule Mwanza. Nakumbuka washiriki hawakupata zawadi kwa wakati kwa sababu hazikutosheleza. Si kwamba tuliwanyima zawadi ndiyo maana tuliporudi tu Dar, tulikaa kama kamati na tukawakabidhi zawadi zao.

 

IJUMAA: Skendo nyingine iliyovuma zaidi ni ile ya washiriki kutoa rushwa ya ngono kwa viongozi au wadau wa Miss Tanzania ili washinde, hii ilikuwa na ukweli kiasi gani?

 

LUNDENGA: Kwanza niifute hiyo fikra kwenye vichwa vya watu ambao wanafikiri hivyo, labda kwa sababu hawajui utaratibu jinsi ulivyo na sheria zetu, washiriki walikuwa wanakaa wenyewe kambini, hakuna mwanaume aliyekuwa anasogelea eneo la kambi, sasa ni saa ngapi mtu atafanya uchafu wa namna hiyo? Hakukuwa na kitu kama hicho kabisa.

 

IJUMAA: Kama kiongozi wa shindano kubwa kama hilo, ni changamoto gani ulizopitia?

LUNDENGA: Ni nyingi sana, lakini kubwa ni pale niliponyimwa kibali cha kuanzisha Miss Tanzania kutoka wizara husika, wakati huo ilikuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni, lakini nashukuru Mungu baadaye nilifanikiwa. Nyingine kubwa ilikuwa ni changamoto ya kipesa kwa sababu nilikuwa natoa pesa mfukoni mwangu na kwa wadau ambao niliwatafuta ili kuendesha Miss Tanzania.

 

IJUMAA: Unajivunia nini kwenye Miss Tanzania?

LUNDENGA: Kwanza ninajivunia kuwa mwanzilishi na msimamizi wa Miss Tanzania kwa kipindi chote hicho na nimetengeneza njia ambayo wengine wanaifuata. Pia najivunia kutengeneza mastaa wengi hapa nchini. Unaweza ukawataja washindi na washiriki wote wenye majina makubwa mjini.

 

Ni wengi sana, wapo akina Jacqueline Ntuyabaliwe (Jack Mengi), Nancy Sumari ambaye alifanya vizuri hadi Miss World Afrika, Irene Uwoya, Wema Sepetu, Jokate Mwegelo ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya (Kisarawe) na wengine wengi.

 

Wengine wenye majina waliopitia Miss Tanzania ni pamoja na Hoyce Temu, Millen Magese, Faraja Nyalandu, Richa Adhia, Nasreen Karim, Miriam Gerald, Sylvia Shally na Aunt Ezekiel.

Wengine ni Sylivia Bahame, Salha Israel, Briggite Alfred, Happiness Watimwanya, Lilian Kamazima na wengine kibao.

 

IJUMAA: Mwaka huu tunaambiwa Miss Tanzania imebadili mfumo wa upatikanaji wa washiriki na kuanzisha mfumo wa kutembea kanda zote kufanya usaili, je, mfumo huu unauonaje?

LUNDENGA: Inategemea na uongozi wenyewe jinsi walivyoamua. Kama wameona njia hiyo ni sawa kwao, basi waitumie japokuwa si kazi rahisi kutembea kanda zote; yaani mikoa yote ya Tanzania.

 

IJUMAA: Miss Tanzania imekupa mafanikio kiasi gani?

LUNDENGA: Kikubwa kutembea sehemu nyingi duniani na kujifunza. Nimetembea nchi kama China, India, Uingereza na nyingine nyingi. Hivyo imenisaidia kuijua dunia na vitu vingi ambavyo sikuvijua.

IJUMAA: Je, una familia ya watoto wangapi?

 

LUNDENGA: Nina mke na watoto sita. Kuna watoto ambao wapo Marekani ila mmoja yupo hapa (Tanzania) na anasoma Chuo Kikuu cha Dar (UDSM).

IJUMAA: Ulikuwa unadili na warembo, je, mkeo alikuwa anaichukuliaje kazi yako?

LUNDENGA: Ninamshukuru Mungu kwa sababu mke wangu alikuwa anaelewa kazi yangu. Pia ananiamini, hivyo haikuwa ngumu kwa upande wake kukubaliana na hali halisi.

 

IJUMAA: Baada ya kustaafu kuratibu Miss Tanzania, kwa sasa unajishughulisha na nini?

LUNDENGA: Nimezeeka sasa, umri umeenda na sidhani kama ninaweza kufanya tena kazi za kuajiriwa. Ninafanya kazi zangu binafsi na maisha yanaendelea.

IJUMAA: Unaishauri nini Kamati ya Miss Tanzania ya sasa?

 

LUNDENGA: Ninafurahi kwa sababu mtu aliyepokea kijiti changu alikuwa Miss Tanzania aliyepita kwenye mikono yangu (Basila Mwanukuzi). Ninampongeza kwa kazi nzuri anayofanya, ninamshauri asikate tamaa na Mwenyezi Mungu aendelee kumsimamia.

Makala: Happyness Masunga

Leave A Reply