The House of Favourite Newspapers

Lwakatare Arejea CUF, Atangaza Kutogombea Ubunge -Video

0

WABUNGE wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),akiwemo Wilfred Lwakatare wamekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF), huku Lwakatare akisisitiza ameenda kukipa chama nguvu na hatogombea ubunge.

 

Aidha, Lwakatare amesema msimamo wa CUF sio kupinga kila kitu yakiwemo mambo mema yanayotekelezwa na chama tawala na serikali iliyopo madarakani na kwamba wao wanaunga mkono mambo yote mazuri ya kimaendeleo na kukosoa utendaji usioridhisha.

 

Wakizungumza jana Mei 31, 2020 jijini Dar es Salaam kwenye ofisi za CUF eneo la Buguruni, Lwakatare alisema Chadema walishamfukuza na yupo bungeni kwa idhini ya Spika na kwamba hana deni na mtu na wala hadaiwi hivyo ameamua kurudi CUF kusaidia kukijenga.

Wilfred Lwakatare ni mbunge wa Bukoba Mjini kupitia Chadema, na Subrina Sungura ni mbunge wa Viti Maalum Kigoma (Chadema).

“ Siku kadhaa katika bunge hili lililobakiza siku 18 kumalizika, nilisimama bungeni na nikasema, sitagombea tena nafasi ya ubunge, kwa umri wangu nastaafu kugombea nitabaki kushauri na kusaidia masuala ya siasa ndani ya CUF kwa sasa, sina deni na mtu na wala sidaiwi,”alisema Lwakatare.

 

Alisema akiwa Chadema alikisaidia chama kwenye nafasi aliyokuwa nayo na alitumikia kwa uadilifu na kwamba kwa sasa ameamua kurudi CUF na kadi yake ya uanachama wa CUF namba 104 aliyokuwa nayo tangu enzi za Muasisi wa chama hicho, James Mapalala, bado anayo na ataendelea kuitumia.

 

“Ninaomba radhi sana kwa wanachama wa CUF, pale nilipokosea chama na nyie mnisamehe na mimi ninasamehe wote walionikosea ndani ya chama, naomba pia muwasamehe waliowahi kukikosea chama, tusigombanie vyeo, tujenge chama kwa sababu kushinda uchaguzi ujao ni suala la idadi ya kura, sasa tukiwa tumegawanyika hatuwezi kushinda,”alisema Lwakatare.

 

Aidha alisema hakuna sababu za msingi ziku zote kuwa mpinzani, na badala yake ni vyema kukubali mema yanayotendeka na kukosoa mabaya kwa lengo la kujenga.

 

Akizungumzia sababu za kukihama Chadema,Lwakatare alidai kushindwa kuvumilia siasa za kibabe. Mbunge mwingine aliyehamia CUF, ni aliyekuwa mbunge wa viti maalum, Kigoma (Chadema), Subrina Sungura ambaye alisema kwa kipindi chote alichokuwa Chadema hakuna na furaha na amechoka kubaguliwa.

Leave A Reply