The House of Favourite Newspapers

Lwandamina amfungia kazi Ibrahim Ajibu

0
Kocha wa Yanga hiyo, Mzambia, George Lwandamina.

KIUNGO mshambuliaji mpya wa Yanga, Ibrahim Ajibu, jana alitambulishwa na kuanza mazoezi ya pamoja na wenzake chini ya Kocha wa timu hiyo, Mzambia, George Lwandamina. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Ajibu kuanza mazoezi katika kikosi cha Yanga chini ya Lwandamina.

Timu hiyo, ilianza mazoezi hayo kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara itakayoanza mwezi Agosti, mwaka huu. Timu hiyo, ilianza mazoezi yake ya kujifua jana asubuhi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ikianza na nyota 15 pekee wapya na wa zamani. Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema tayari amepokea programu ya mazoezi ya msimu mpya wa ligi kuu watakayofanya kila siku asubuhi na jioni.

Kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga, Ibrahim Ajibu.

 

Saleh alisema, asubuhi watakuwa gym wakifanya mazoezi ya kuongeza fiziki kabla ya jioni kufanya mazoezi ya uwanjani kwa ajili ya kulainisha mwili. Aliongeza kuwa, programu hiyo ya mazoezi wataifanya kwa siku 14 sawa na wiki mbili, lengo likiwa ni kurudisha fitinesi ya wachezaji wake waliokuwa kwenye likizo ya mwezi mmoja. “Kocha tayari amenikabidhi ripoti ambayo tayari nimewapatia wachezaji kwa ajili ya kuifuata kwa asubuhi kuanzia gym kwa ajili ya kutengeneza fiziki na jioni tunahamia uwanjani. “Tunafanya mazoezi ya uwanjani kwa lengo la kutengeneza muunganiko wa wachezaji wapya

tuliowasajili, pia kuufahamu mfumo ambao kocha anautumia kwenye mechi,” alisema Saleh. Katika hatua nyingine, meneja huyo kabla ya mazoezi aliwatambulisha wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo, wakiongozwa na Ajibu, Pius Busitwa na Abdallah Shaibu ‘Ninja’. Wachezaji waliohudhuria mazoezi ya jana ni Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Said Makapu, Vincent Andrew ‘Dante’, Geoffrey Mwashiuya, Amissi Tambwe, Pato Ngonyani, Yusuf Mhilu, Emmanuel Martin, Juma Abdul, Said Mussa na Maka Edward ambao ni U20 waliopandishwa kwenye timu kubwa, mwingine ni Mcameroon, Fernando Bongnyang anayeichezea Cotton Sports ya nchini humo anayefanya majaribio Jangwani.

Stori: Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge | Championi


 

Leave A Reply