The House of Favourite Newspapers

Maajabu Mtoto Mlemavu Bongo, Simulizi Yake Fundisho!

OMARY Jumanne ‘9’ ndiyo mtoto anayeonekana katika picha kubwa ukurasa wa mbele; usimchukulie poa kwa jinsi unavyomtafsiri; Uwazi lina maajabu yake na linakupa simulizi yenye mafunzo makubwa. 

 

Fatuma Athuman mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro ndiyo mama mzazi wa Omary ambaye amezungumza na mwandishi wetu na kumpa simulizi ya maisha ya mtoto huyo.

 

MSIKIE FATUMA

“Huyu mtoto ana maajabu mengi sana kwanza ana akili na ufahamu usiokuwa wa kawaida lakini kikubwa zaidi ana akili darasani, kwani hadi walimu wake wanamshangaa.

 

“Miaka tisa iliyopita nilibeba mimba kama wanawake wengine, sikufikiria kama ningeweza kuzaa mtoto mwenye ulemavu. “Nakumbuka niliposhikwa na uchungu nilikwenda Hospitali ya KCMC kwa ajili ya kujifungua, ilikuwa siku yenye matarajio ya furaha kwangu, mume wangu na familia kwa ujumla.

 

MTOTO MWENYE ULEMAVU AZALIWA

Fatuma anasimulia kuwa baada ya kujifungua na mtoto kuhifadhiwa, baadaye aliletewa na wauguzi kwa ajili ya kumnyonyesha hapo ndipo alipogundua jambo lililomhuzunisha.

 

“Nilimtazama mara mbilimbili nikawa najiuliza ni nini hiki ninachokiona mbele ya macho yangu? Mtoto wangu alikuwa hana miguu na mikono haikuwa imekamilika katika maumbile.”

 

Alisema Fatuma na kuacha ujumbe mzito kwamba hata kama ungekuwa wewe ndiyo mzazi na umekutana na mtoto tofauti na matarajio yako ungekuwa katika hali ya huzuni na kama huna imani unaweza kukufuru.

 

APIGA MOYO KONDE

Kutokana na hali ambayo haikuwezekana kubadilishika, Fatuma anasema alilazimika kumkubali mwanaye katika hali ya ulemavu aliyonayo na hivyo kuendelea kumlea kwa mapenzi yote.

 

“Hata niliporudi nyumbani niliona ni hali ya kawaida ingawa kuna baadhi ya watu walikuwa wakija kumtazama wanaonesha mshangao lakini mimi nilikuwa nimekubaliana na hali hiyo. “Nilijua alichonipa Mwenyezi Mungu kilikuwa chema katika maisha yangu na sikuwa na namna ya kupingana na mapenzi yake.”

 

MUME AINGIA MITINI

“Pengine kwa sababu ya ulemavu aliokuwa nao Omary, mume wangu hakuwa tayari kushirikiana nami katika malezi ya mtoto. “Ikabidi nianze kumlea mwenyewe kwa shida huku wasamaria wakinisaidia, nashukuru Mungu leo nahisi nimekuza,” alisema Fatuma na kuongeza kuwa hajui mahali alipo mumewe.

 

OMARY AFANYA MAAJABU SHULENI

Fatuma anasema kutokana na uwezo aliokuwa akiuonesha Omary katika suala zima la kusoma, msamaria mwema aljitokeza na kuahidi kugharamia masomo yake shuleni.

 

“Mwaka huu nilimuanzisha darasa la kwanza katika Shule ya St. Thimoth iliyopo Moshi mjini ambapo ada yote alikuwa akimlipia huyo mfadhili wake.

 

“Shuleni alionesha maajabu makubwa tofauti na wengi walivyokuwa wakimchukulia hapo mwanzo, aliweza kuandika vizuri kwa kutumia mkono wake wenye ulemavu, kusema kweli ana akili nyingi na anapenda sana kujisomea.

MFADHILI AISHIWA PUMZI

Kutokana na hali ya mambo kumwendea ndivyo sivyo, mfadhili aliyekuwa akimuwezesha Omary; Juni mwaka huu alishindwa kuendelea na ufadhili wake huo na hivyo kumfanya mtoto huyo kushindwa kuendelea na masomo.

 

FATUMA AFADHAIKA

“Nilianza kuona nyota ya mwanangu iking’aa, lakini ghafla matumaini yameanza kuyeyuka, mtu aliyekuwa akimsaidia amepata matatizo, uwezo wa kuendelea kumsomesha sina.

“Tangu mwezi wa sita Omary yupo hapa nyumbani, analilia shule lakini sina uwezo, amebaki anajisomea mwenyewe; kila mara anachukua madaftari yake anaandika na kusoma, uwezo wake unamstaajabisha kila mtu.”

 

FATUMA APATA KIGUGUMIZI SHULE ZA SERIKALI

Mwandishi wetu alipomuuliza Fatuma kwa nini asimpeleke Omary kwenye shule za kata ambazo elimu hutolewa bure alisema:

“Ni kweli serikali inatoa elimu bure lakini kutokana na hali ya huyu mtoto napata shida sana kumpeleka kwenye shule zisizokuwa na uangalizi maalumu. “Ndiyo maana nimekuwa nikihangaikia watu wa kumsaidia maana naona anaweza kuwa mtu wa kipekee katika nchi hii kutokana na uwezo wake wa kiakili.”

FUNZO KWA WAZAZI

Hata hivyo, simulizi ya Omary ni funzo kwa wazazi wengi ambao wamekuwa wakijisikia vibaya wanapozaa watoto wenye ulemavu.

“Ulemavu si ugonjwa, bali ni hali ya kimaumbile, mtoto anaweza kuwa mlemavu lakini akawa msaada mkubwa kwa jamii kuliko hata asiyekuwa mlemavu.

 

“Mimi nawashauri wazazi wenzangu inapotokea mtu amezaa mtoto mwenye ulemavu asimtelekeze, ampe haki zake kama mtoto kamili na amwendeleze kielimu,” alisema mzee Said mkazi wa Ilala jijini Dar ambaye naye ana mtoto mwenye ulemavu, alipozungumza na Uwazi kwa njia ya simu kuhusu malezi ya watoto walemavu.

 

WITO WA KUMSAIDIA OMARY

Kwa mtu yeyote ambaye ataguswa na simulizi ya maisha ya Omary na akatamani kuchangia chochote kuhakikisha ndoto za mtoto huyo zinatimia basi awasiliane na mama yake kwa namba za simu zifuatazo; 0763711720.

 

Ifahamike kuwa ulemavu wa Omary si kikwazo katika maisha na masomo kwani Muaustralia, Nicholas James “Nick” Vujicic ambaye hana mikono wala miguu ni miongoni mwa watu waliofanikiwa zaidi duniani.

Comments are closed.