The House of Favourite Newspapers

Wanajeshi DRC wahukumiwa kifo kwa kukimbia vita

0

Mahakama ya kijeshi katika mji wa Goma huko Kivu Kaskazini Mashariki mwa Congo imewahukumu kifo maafisa nane wa jeshi la Congo, FARDC kwa tuhuma za kukimbia vita na kutoheshimu sheria za kijeshi.

Miongoni mwao ni Kanali Shamba mkuu wa kikosi cha makomando pamoja na msaadizi wake.

Mwendesha mashtaka amesema makamanda hao walishindwa kuwajibika kwenye uwanja wa mapigano karibu na mji wa Sake wilayani Masisi eneo lililo magharibi mwa mji wa Goma ambalo M23 inaendelea kuchukua udhibiti wa vijiji.

Wakili wa makamanda hao Bwito Jean Richard wa jeshi tiifu kwa serikali amesema mahakama imefanya makosa kutoa adhabu ya kifo kwa wanajeshi hao ambao walikuwa wamejitolea kulipigania taifa.

Hata hivyo amekata rufaa na kuonya Mahakama kuwa makini kwa kuwa hatua za mahakama zaweza kuwapelekea wanajeshi wengi kutoenda vitani.

Lakini baadhi ya wachambuzi wamesema hatua hii itawazuia wanajeshi kukimbia mapigano kila mara na kuwaacha waasi kuchukuwa vijiji.

Katika hukumu hiyo wanajeshi watatu, kapteni mmoja na maluteni wawili waliachiliwa huru na mahakama kwa madai ya kutokuwa na hatia.

Makamanda hao walipewa adhabu ya kifo kwa mujibu wa sheria ya nchi hiyo. Wakati huohuo Mkuu wa mahakama ameomba pande husika kukata rufaa katika kipindi cha siku tano.

Leave A Reply