The House of Favourite Newspapers

Maambukizi Kwenye Mfuko Wa Kizazi (Pelvic Inflamatory Disease)

pelvic-inflamatory-diseaseMAAMBUKIZI haya ni ya vijidudu katika via vya uzazi ambapo wadudu hupanda kutoka kwenye utupu wa mwanamke na kuingia kwenye viungo vya uzazi kama vile mji wa mimba, mirija na tezi za mayai na hupitia kwenye shingo ya kizazi, kitaalamu maambukizi haya huitwa Pelvic Inflamatory Disease (PID).

Asilimia 85 ya maambukizi katika via vya uzazi huwapata wanawake ambao wapo katika uhusiano wa kimapenzi, ugonjwa huu humpata mtu aliyewahi kuathirika na maambukizi ya magonjwa ya zinaa, pia kwa asilimia kubwa husababishwa na vimelea vya kisonono au Gonorrhea na Chlamydia.

Ugonjwa huu huweza kusababisha tatizo la kutopata mimba (infertility), kati ya wanawake nane waliougua ugonjwa huu, mwanamke mmoja huweza kupata ugumba, mara nyingi huathiri zaidi vijana.

Mara baada ya mgonjwa kuambukizwa magonjwa ya zinaa na kutotibiwa, vimelea hawa hupanda katika mfuko wa kizazi na hatimaye kufikia katika mirija ya uzazi, wanapokuwa katika mfuko wa kizazi, kinga ya mwili huamka kupambana nao. Kemikali mbalimbali hutolewa kutokana na mpambano huo na ikiwa

ugonjwa umekaa kwa muda mrefu basi kemikali hizi zinazotolewa huharibu kuta za mfuko wa kizazi na kusababisha michomo na maumivu makali kwenye ukuta wa uzazi, mirija ya mayai na viungo vingine vilivyo kwenye uzazi na hivyo kusababisha kuwa vigumu kwa mimba kutungwa au kukua katika kuta hizo.

Kwa sababu ugonjwa huu ni matokeo ya kutotibiwa kwa magonjwa ya zinaa(sexually transmitted infections) basi njia zinazomuweka mtu hatarini ni kushiriki tendo la ndoa na mtu aliyeathirika na vimelea hivyo.

Mambo yafuatayo yanaweza kumweka mwanamke hatarini zaidi, kupata na kutotibiwa kwa magonjwa ya zinaa, kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja, kuwa na mpenzi mwenye wapenzi wengi, kuwa na historia ya ugonjwa huu kabla ya sasa, kujisafisha kwenye uke  kwa maji au vidole, kutumia uzazi wa mpango hasa kwa kuwekewa vifaa kama kitanzi kwenye kizazi.

JINSI YA KUJIKINGA

Njia pekee ya kujikinga ni kuacha kufanya ngono zembe, ngono kwenye mdomo na njia ya haja kubwa.

Endapo umepata mpenzi ni vema mkapima na kuangalia kama mmoja ana maambukizi ya ugonjwa huu atibiwe kwanza au tumia kondomu unaposhiriki tendo la ndoa. Pia punguza mtandao kwa kuwa na mpenzi mmoja tu mwaminifu aliyepima.

 DALILI

Mwanamke anaweza asijitambue kwamba ana ugonjwa huu kwa sababu anaweza asiwe na dalili kwani huwa zinajionesha kidogo sana na hivyo kwa kuchukuliwa historia na daktari pamoja na uchunguzi wa awali (physical examination) na vipimo vingine unaweza kujulikana kama mgonjwa ameathirika na ugonjwa huu.

Ikiwa dalili zipo basi unaweza kuwa na dalili zifuatazo; maumivu ya tumbo chini ya kitovu, homa (lakini hutokea kwa mtu mwenye maambukizi ya awali, ugonjwa ukiwa sugu mgonjwa huwa hapati dalili hii), uchafu usio wa kawaida kutoka ukeni na hutoa harufu mbaya, maumivu au kutokwa damu wakati wa tendo la ndoa, hisia za kuungua wakati wa kukojoa, kutokwa na damu nyingi isiyo ya kawaida katikati ya kipindi cha hedhi.

VIPIMO NA MATIBABU

Yapo matibabu ya ugonjwa huu na huwa vizuri endapo ugonjwa utatibiwa mapema. Mara utakapoanza matibabu dalili zinaweza kutoweka lakini unatakiwa kumaliza dozi uliyopewa. Madhara yanayosababishwa na ugonjwa huu kwenye kizazi huwa hayaondoki na mtu anapochelewa matibabu madhara yanaendelea kuwa makubwa.

Madhara makubwa yatokanayo na ugonjwa huu ni kufanyika kwa makovu nje na ndani ya kizazi yanayosababisha kuziba kwa mirija ya uzazi, mimba kutunga nje ya kizazi (ectopic pregnancy), ugumba (infetility) na maumivu sugu au yasiyoisha ya tumbo chini ya kitovu.

Ukigundulika kuwa una vijidudu vilivyoshambulia ukuta wa tumbo la kizazi baada ya kupimwa damu kama vile full blood picture ambapo kama mgonjwa ana maambukizi, basi chembechembe nyeupe za damu zitaonekana kuongezeka. Vipo vipimo vingi kama vile cha Ultra Sound au ESR  nk. Matibabu yake kwa mwanamke ambaye aliwekewa kitanzi (LUCD) na ana maambukizi, itabidi kitolewe.

Itabidi apatiwe dawa za kuua wadudu (antibiotics) mchanganyiko wa dawa aina tatu na atazitumia kwa muda wa wiki mbili. Lakini mama huyo ni lazima amwambie mwenzi wake tatizo hilo la maambukizi ili naye akatibiwe, vinginevyo wakijamiiana bila huyo kutibiwa ugonjwa utajirudia.

 Tiba nyingine ni ya upasuaji (surgery) kwa ajili ya kumulika mirija na kuchukua vipimo, kitaalamu huitwa laparoslopy hasa kama ugonjwa unajirudia au kutumia dawa bila kupona au kutokana na kuwepo viuvimbe vidogo kwenye kizazi au kama mgonjwa hashiki mimba.

Comments are closed.