The House of Favourite Newspapers

MABADILIKO NA ATHARI KWENYE MZUNGUKO WA HEDHI

TATIZO la mabadiliko yasiyo ya kawaida katika mzunguko wa hedhi huwapata wanawake wengi walio katika umri wa kuzaa na wale waliomaliza majukumu yao ya uzazi, lakini hawajafunga hedhi. 

 

Tatizo linapojitokeza huleta athari nyingi kwa mwanamke kwa kumfanya ashindwe kupangilia mipango yake kama kupata ujauzito au kutopata.

 

JINSI TATIZO LINAVYOTOKEA

Mwanamke hulalamika kutofahamu vizuri siku zake, hajui anaingia lini, yaani damu inaweza tu kutoka na inachukua muda mrefu hata zaidi ya siku saba ikiwa nyingi au matonematone. Mwanamke hushindwa kupangilia siku za kupata mimba, tatizo huanza taratibu na mwishowe huchukua muda mrefu, mwanamke mwingine hujikuta anaingia hata mara mbili kwa mwezi.

CHANZO CHA TATIZO

Asilimia kubwa ya tatizo hili husababishwa na kuvurugika kwa mfumo wa homoni mwilini, hasa homoni au vichocheo vinavyoendesha na kudhibiti hedhi na uzazi kwa jumla. Uwepo wa uvimbe ndani ya kizazi au kwenye vifuko vya mayai pia ni tatizo.

 

Mabadiliko kwenye tabaka la ndani la kizazi, maambukizi sugu ya kizazi na kuharibika kwa mimba ni miongoni mwa matatizo haya yanayochangia siku za hedhi zitoke bila mpangilio. Maambukizi ya kizazi hasa ‘Pelvic Inflammatory Diseases (PID)’, uvimbe kama mayoma au fibroid navyo huchangia kusababisha tatizo hili.

 

Matumizi ya baadhi ya madawa bila ushauri wa kitaalam na hata dawa za uzazi wa mpango endapo zitatumika kiholela bila ushauri wa wataalam wa afya. Kwa wengine, mfano, sindano au vipandikizi na hata vidonge vya kudhibiti mimba, huweza kuvuruga homoni na kusababisha matatizo haya.

 

DALILI ZA TATIZO NA ATHARI ZAKE

Mwanamke mwenye tatizo hili hulalamika kutokufahamu mwenendo wa mzunguko wake, hulalamika damu kutoka muda mrefu au siku chache sana chini ya siku tatu, wakati mwingine hapati kabisa. Anaweza kuwa na maumivu ya tumbo chini ya kitovu, maumivu wakati wa hedhi, maumivu wakati wa kujamiiana na hata damu kutoka mabonge au nyingi na nyepesi. Pia ataelezea ni muda mrefu anatafuta mtoto, lakini hapati. Wengine hujikuta wakipata mimba bila kupangilia.

 

Athari za hali hii ni mwanamke kupoteza uwezo wa kuzaa, kupoteza uwezo wa kufurahia tendo la ndoa, kutumia muda mwingi kujitibu au gharama kubwa kwenye matibabu. Mwanamke pia hujikuta inamlazimu kutolewa kizazi kutokana na hali yake kiafya kuwa mbaya na kizazi kuharibika kabisa.

NINI CHA KUFANYA?

Tatizo hili humuathiri mwanamke kwa kiasi kikubwa hasa pale damu inapotoka kwa muda mrefu kwa zaidi ya siku saba au asipopata kabisa hedhi katika umri wake kama unamruhusu. Pia mwanamke hatakuwa vizuri anapopata maumivu wakati wa hedhi au anapotafuta mtoto halafu hapati ujauzito.

 

Uchunguzi hufanyika kwenye kliniki za madaktari bingwa wa magonjwa ya kina mama na afya ya uzazi katika hospitali za mikoa, vipimo mbalimbali vitafanyika kadiri daktari atakavyoona inafaa. Vipimo pia vitazingatia mahitaji ya mwanamke kama yupo tayari kushika ujauzito kwa kipindi hicho.

 

Kwa hiyo katika upimaji atachunguzwa na mfumo wake wa uzazi. Baadhi ya vipimo utakavyo-lazimika kupima ni ultrasound, damu kuangalia homoni, uchunguzi wa ukeni na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa. Uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na kizazi chenyewe vitazingatiwa.

USHAURI

Ni vema mwanamke mwenye matatizo haya akazingatia ushauri wa daktari wake ili aweze kupona na kufanikiwa malengo yake ya kupata ujauzito. Baada ya uchunguzi wa kina ndipo utaratibu wa matibabu unaanza.

 

Mwanamke ambaye ameshafikia ukomo wa kuzaa, yaani zaidi ya miaka arobaini na tano na ana matatizo haya, basi azingatie sana uchunguzi na tiba au ushauri mwingine atakaopewa na daktari wake. Matatizo haya huchunguzwa na kutibiwa katika kliniki za madaktari bingwa wa magonjwa ya kina mama na afya ya uzazi.

Comments are closed.