The House of Favourite Newspapers

Mabilionea wasio na huruma – 80

0

PADRI Silvanio na Sista Mariastela wanasakwa kwa udi na uvumba, wakiaminika kuwa ni watawa feki waliofanya utapeli ili kuyanasa mabilioni ya urithi ya Dk Viola na Vanessa. Wakiwa wanatafutwa Dar es Salaam, wanafanikiwa kuruka kwa ndege kupitia Nairobi, lakini mkuu wa Interpol Nairobi anapewa taarifa juu ya kusakwa kwao na ndege yao tu ilipotua jijini humo ikazingirwa na polisi. Je, watafanikiwa kuwakamata? Je, ni nini kilichojificha nyuma ya pazia kwa watawa hao?

SONGA NAYO…

NDEGE namba PQ 290ATL tayari ilishakanyaga ardhi ya Kenya na baadaye kusimama, askari zaidi ya mia moja kila mmoja akiwa na silaha wakaizunguka, magari ya zimamoto pia yalionekana kuizunguka ndege hiyo, kikosi kilikuwa kamili kupambana na mtu yeyote aliyekuwa mbele yao.
Kipaza sauti ndani ya uwanja wa ndege kikasikika, sauti ikiamuru watu wote waliokuwa ndani ya ndege namba PQ 290 ATL iliyokuwa ikitokea jijini Dar es Salaam washuke haraka sana.
“Tunaomba abiria wote walioko ndani ya ndege iliyowasili muda mfupi uliopita washuke haraka iwezenavyo,” sauti iliendelea kutangaza huku macho na silaha za askari wote mia moja vikiwa tayari kwa lolote, kwa takribani dakika tatu nzima mambo yalikuwa ni yaleyale hakukuonekana dalili ya mtu kushuka wala mlango wa ndege kufunguliwa.
“Hebu atangaze kwa mara ya mwisho, tuone kama hawatafungua mlango na kutoka wenyewe, basi tutalazimika kuingia kwa nguvu na kuwakamata, hawawezi kutufanya wajinga,” John Kamau aliongea kwa sauti akionyesha hasira zake waziwazi, mara kadhaa alipokuwa na kazi ngumu kama hiyo iliyokuwa mbele yake hakuwa mtu wa mzaha, alitaka kulinda na kutunza heshima yake.
Pamoja na kutoa nafasi akiwataka askari wake kuwa watulivu akiamini kwamba pengine watu waliokuwa ndani ya ndege hiyo wangejitokeza wenyewe, haikuwa hivyo mpaka dakika kumi na tano baadaye, ndipo Kamishina John Kamau akatoa amri akiwataka askari kuisogelea ndege hiyo na kuamuru ifunguliwe ili waingie ndani kwa ajili ya upekuzi.
Chini ya kamishina John Kamau kwa kuonyesha kibali maalum alichokuwa nacho, rubani akaamriwa kufungua ndege na kuruhusu polisi kuingia ndani. Askari zaidi ya kumi wakiwa na silaha za moto wakazama ndani na kuanza kufanya upekuzi sehemu zote za ndege bila kuona dalili ya mtu.
“Mh!”
“Vipi?”
“Bosi hii ndiyo ndege yenyewe kweli?”
“Hakika.”
“Hakuna mtu yeyote humu ndani.”
“Mnasemaje?”
“Tumeingia ndani na kufanya upekuzi kwa inavyoonekana ndege ilikuja na rubani tu peke yake.”
“Siyo rahisi.”
“Tunachokueleza ni ukweli tupu.”
Kamishina John Kamau hakuwa tayari kuelewa alichokisikia kutoka kwa askari wake, akawataka wafanye tena upekuzi wakihakikisha wanaangalia sehemu zote ndani ya ndege hiyo kwani ni ndege ambayo alipewa namba na kupewa taarifa kwamba ndani yake ilikuwa imebeba wahalifu.
Askari wakaingia tena na kuanza kukagua na walipotoka jibu lao lilikuwa lilelile, ndani ya ndege hapakuwa na mtu yeyote.
“Nahitaji kufanya mahojiano na rubani wa ndege hiyo,” John Kamau aliongea akionyesha hasira za waziwazi.
Haraka rubani akaitwa na kuingizwa kwenye chumba maalum kisha kuanza kuhojiwa akitakiwa kueleza ukweli na kueleza ni wapi aliwaacha abiria aliotoka nao jijini Dar es Salaam wakiwa safirini kuja nchini Kenya kisha Dubai.
Rubani akaingizwa kwenye chumba maalum ambako alimkuta Kamishina John Kamau ambaye alimpokea na bila hata salamu akamtaka kueleza ni kitu gani kilitokea mpaka kutua ndani ya Uwanja wa Jomo Kenyatta peke yake wakati ndege hiyo ilikuwa imekodiwa na watawa wawili waliokuwa wakisafiri kutoka Dar kuja Kenya na baadaye Dubai.
“Ni kweli ilikuwa hivyo lakini dakika tano kabla ndege haijaondoka abiria hao waliingia ndani ya uwanja na kunieleza kwamba wasingeweza kupanda tena ndege hiyo wakiogopa ugaidi na kuniambia kwamba wao wangetumia njia ya barabara na mimi nitangulie na tungekutana huku.”
“Duh!” John Kamau alihisi akili ikichanganyika, hakuwa tayari kusikia alichokuwa akiambiwa na rubani wa ndege.
“Kamishina huo ndiyo ukweli.”
“Baada ya kukueleza hivyo walielekea wapi?”
“Niliwashuhudia wakitembea kutoka nje kwa kutumia mlango wa VIP baadaye sikufahamu kilichoendelea.”
“Una uhakika?”
“Nina uhakika asilimia mia moja, nilichoeleza ndicho kilichotokea.”
“Wametoroka tena!”
“Kiongozi inavyoonekana hawa watawa ni watu hatari mno.”
“Si watu wa kuchezea, wanafikiria mbele zaidi.”
“Kwa hiyo?”
“Hatuna jinsi zaidi ya kuwasiliana na Kamishina Hussein Rajab na kumweleza mambo yalivyokuwa.
Kamishina John Kamau akiwa na kundi la polisi wote wakatembea na kutoka nje ya Uwanja wa Jomo Kenyata kurejea ofisini akiwa na maswali mengi juu ya watawa wawili hatari, gari lilipoegeshwa tu akawa mtu wa kwanza kushuka haraka akatembea kuingia ofisini kwake akanyanyua simu kisha kupiga namba ya Kamishina Hussein Rajab ili kumpa taarifa.
“Ngriii! Ngriii! Ngriii.” Simu ilisikika ikiita na muda mfupi tu baadaye ikapokelewa na sauti iliyosikika upande wa pili John Kamau aliifahamu vizuri, ilikuwa ni ya rafiki yake wa siku nyingi na mpelelezi mwenzake Kamishina Hussein Rajab.
“Hallow.”
“Ndiyo John niambie, umefanikiwa kuwakamata wahalifu?”
“Hapana.”
“Kwa nini? Ndege haijafika?”
“Ndege imefika lakini baada ya upekuzi wetu ndani ya ndege hawakuwemo.”
“Hawakuwemo? John unanitania au?”
“Huo ni ukweli ndege imewasili ikiwa na rubani tu, hakukuwa na abiria yeyote ndani na baada ya kuongea na rubani ametueleza kwamba watawa hao waliingia ndani ya uwanja dakika tano kabla ndege haijaondoka na kumweleza rubani kwamba kwa kuwa wanahofia masuala ya ugaidi basi yeye rubani atangulie na wao wangetumia gari na wangekutana Kenya.”
“Duh! Kwa mara nyingine tena wamefanikiwa,” Kamishina Hussein alijikuta akitamka kwa sauti, tumaini alilokuwa nalo juu ya kuwakamata wahalifu hao wawili watawa lilikuwa limetoweka, taa nyekundu ikawaka kichwani mwake, akionyesha masikitiko, akamshukuru John Kamau kisha kukata simu na kumgekia mwanasheria Denis Crapton aliyekuwa ofisini kwake.
“Tumechelewa.”
“Unamaanisha nini?”
“Lazima tutambue kwamba tunadili na watu hatari kuliko, ambao akili zao zinafikiria zaidi.”
“Kamishina mbona sikuelewi?”
“Kifupi ni kwamba Padri Silvanio na Sista Mariastela hawakusafiri na ndege kama tulivyokuwa tukifahamu.”
“Lakini waliingia ndani ya uwanja?”
“Ni kweli kwa jinsi nilivyoelezwa na Kamishina Kamau waliingia na kutoka wakiacha taarifa kwamba waliogopa kusafiri na ndege, hivyo wangesafiri na gari na kumwambia rubani kwamba wangekutana Kenya.”
“Mungu wangu!” Denis Crapton alisema akishika mikono kichwani.
Taarifa aliyokuwa ameipata ilikuwa imemchanganya kabisa akili yake, akiwa hapo jasho jembamba lilionekana kumtoka pamoja na kwamba ndani ya ofisi ya Kamishina Hussein kulikuwa na kiyoyozi kikali.
“Sasa?”
“Haraka turejee uwanja wa ndege kuangalia kamera za CCTV ili kugundua walipotoka walipanda gari gani na namba, hiyo itatusaidia kulifuatilia.” Kamishina Hussein aliongea, tayari alishaufikia mlango na kuufungua, hakukuwa na muda wa kupoteza, walitaka wafike huko haraka iwezekanavyo.
Wakati anatoka ofisini alionekana kutumia simu ya upepo aliyokuwa nayo mkononi mwake akitoa maagizo kwa polisi wa barabara ili kuhakikisha anapata nafasi bila msongamano ili kuwahi uwanja wa ndege kwa shughuli maalum. Wakaingia kwenye lifti na kushuka mpaka chini ambako walikuta tayari gari likiwasubiri, haraka wakaingia na kumwamuru dereva aendeshe kwa kasi kuelekea uwanja wa ndege.
Dakika kumi na tano tu baadaye, tayari walishafika uwanja wa ndege, hapo wakashuka na kutembea moja kwa moja kuelekea ofisini kwa meneja wa uwanja, kama ilivyokuwa mwanzo wakajitambulisha tena, safari hii wakiomba kuonyeshwa kumbukumbu ya matukio yote yaliyonaswa kwenye CCTV kamera ili kuangalia Padri Silvanio na Sista Mariastela walipotoka hapo walichukuliwa na gari gani.
“Sawa Kamishina hakuna shida, jambo hilo ni rahisi mno, karibuni mketi nishughulikie.”
“Ahsante.” alisema Denis Crapton na wote wakatembea na kuketi kwenye viti vilivyokuwa ndani ya chumba hicho, mioyo yao ikionekana kwenda mbio kuliko kawaida, kama ingetokea daktari akawapima presha zao basi ni lazima angesema watu hao walikuwa na shinikizo la damu.
Wakiwa hapo hawakuchukua hata dakika kumi tayari meneja akarejea kisha kuwaita na kuwaingiza kwenye chumba kilichokuwa kando kidogo tu ambako waliketi na kuanza kuangalia matukio yote yaliyokuwa yametokea ndani ya uwanja siku hiyo. Macho yao yaliwashuhudia watawa wawili, mwanamke na mwanaume wakiingia ndani ya uwanja huo na baadaye kidogo kutoka kwa kutumia mlango maalum wa VIP kisha kutembea na kuelekea maegesho ambako walipanda gari aina ya Toyota Corola, haraka wakaisogeza picha ili kuona namba ya gari na kusomeka TZ L 203 ABO.
“Kazi imekwisha, gari hili ni lazima lifuatiliwe kwa karibu, tutawapigia polisi wa barabarani kuhakikisha wanalizuia wanapoliona,”
“Hiyo itasaidia?”
“Asilimia zote.” Kamishina Hussein Rajab aliongea haraka bila kupoteza muda akachukua simu yake ya upepo kisha kuanza kupiga kwa mkuu wa polisi wa barabarani akimpa maagizo na kumtaka ahakikishe gari hiyo haifiki mbali kwani iliaminika kubeba magaidi wawili waliojificha kwa mwamvuli wa watawa.
“Tunaelekea wapi sasa Kamishina?”
“Ofisini tusubiri matokeo.”
Akili zao zilishavurugika, mioyo yao ilijaa hasira na chuki juu ya watawa hao wawili hatari walioonekana kusumbua akili za wengi, ndani ya gari kila mtu alionekana kuwa kimya akijaribu kutafakari juu ya tatizo lililokuwa mbele yao, kilometa chache tu kabla hawajalifikia lango la kuingia makao makuu ya Interpol, simu ya kamishina iliita haraka akaipokea na kuiweka sikioni kusikiliza.
“Nasikiliza.”
“Kamishina taarifa tulizozipata gari TZL 203 ABO limeonekana Kibaha likipita kwa kasi na polisi wetu pamoja na polisi Kituo cha Chalinze wametoka kulifuatilia, tuna uhakika watazingirwa bila wao kufahamu na kufanya kazi ya kuwakamata iwe rahisi.
“Hakikisheni mnawakamata mara moja, nitakuwepo ofisini kwangu,” alijibu na kukata simu.

***
Polisi Mkoa wa Kibaha walikuwa ndani ya magari maalum yasiyopungua kumi kila moja likiwa na askari watano wenye silaha za moto nao pia walikuwa wakifanya mawasiliano na polisi Mkoa wa Chalinze kuhakikisha wanafanikiwa kuliweka chini ya ulinzi gari namba TZL 203 ABO ambalo ndilo haswa walilitumia watawa wawili Padri Silvanio na Sista Mariastela wakielekea mpakani ambako wangeingia na kuvuka kuingia Kenya na hatimaye kuendelea na safari yao.
Kwa kutumia tochi, waliweza kufuatilia kwa makini gari lililowabeba watawa hao wawili hatari likizidi kutokomea, askari kutoka Kibaha wakiwa nyuma na askari kutoka Chalinze wakiwa mbele, tayari walikuwa wamewekwa katikati bila wao kufahamu.
Kilometa chache tu polisi wa Kibaha wakilifuatilia gari kwa kutumia tochi maalum, walishuhudia moshi mzito ukiibuka juu na walipozidi kusogea karibu zaidi walilishuhudia gari namba TZL 203 ABO likiteketea kwa moto.

JE, nini kimetokea? Kimetokea nini mpaka gari ambalo liliaminika kubeba watawa wawili Padri Silvanio na Sista Mariastela kuungua kwa moto? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.

Leave A Reply