The House of Favourite Newspapers

Mabilionea Wasio na Huruma 82

0

GARI walilopanda limekutwa na polisi likiwaka moto, ndani yake kukiwa hakuna watu na msako mkali sasa unaendelea porini kuwatafuta Padri Silvanio na Sista Mariastela ambao wameuza kila kitu nchini Tanzania na sasa wanatoroka kwenda kusikojulikana. Watawa hawa wawili walirithi utajiri wa dola bilioni mbili ulioachwa na Dk. Viola na nduguye Vanessa, ambao walidungwa sindano ya sumu baada ya kuhukumiwa kifo.

Mpelelezi Denis Crapton amegundua kuwa Padri Silvanio na Sista Mariastela walioko nchini Tanzania ni feki, si waliotakiwa kurithi utajiri huo, mara moja amerejea nchini Tanzania kuwasaka watu hao kwa kushirikiana na Polisi wa Kimataifa (Interpol), amebaki jijini Dar es Salaam akisubiri askari warejee kutoka kwenye msako.

Padri Silvanio na Sista Mariastela wamo ndani ya kichaka, Padri akiwaza juu ya kilichofanyika kwa kushirikiana na Muisrael Yousef Emmanuel, kuwatorosha kutoka chumba cha kudungia sindano ya sumu, umeme ulipokatika ghafla! Akiwa katika mawazo hayo alishtukia mbwa wakibweka nje ya kichaka walichojificha.
Je, nini kitaendelea? Watakamatwa?SONGA NAYO…

GHAFLA mbwa wakakivamia kichaka hadi ndani na kuwauma Dk. Viola na Vanessa mavazi yao kisha kuanza kuwavuta kuelekea nje ya kichaka, walikuwa mbwa wakubwa wenye nguvu nyingi. Wakakutana uso kwa uso na mitutu ya bunduki ambayo iliwalenga usoni mwao huku wakitetemeka na jasho jingi kuwatoka ingawa hali ya hewa ilikuwa ya ubaridi.

Lala chini! Lala chini!” askari waliamrisha na wakalala chini kifudifudi, pingu zikachukuliwa na kuifunga mikono yao kwa nyuma.
“Ninyi ni akina nani?”
“Padri Silvanio na Sista Mariastela!”
“Twendeni makao makuu, mtajieleza hukohuko mbele.”

Wakanyanyuliwa na kuanza kusukumwa kwenda mbele na kuendelea kutembea hivyo kwa zaidi ya saa tatu, ndipo wakafika mahali palipokuwa na barabara, wakapiga simu polisi Kibaha na gari ikafika baada ya saa moja na kuwachukua hadi Kituo cha Polisi cha Kati jijini Dar es Salaam ambako timu nzima ya viongozi wa jeshi la polisi na usalama wa taifa walikusanyika, kila mmoja akiwa na hamu ya kusikia hao waliojiita Padri Silvanio na Sista Mariastela walikuwa ni akina nani hasa kama kweli watawa halisi waliuawa nchini Columbia na kutupwa kisimani.

Waliketishwa mbele ya jopo la askari, Denis Crapton akiwa katikati yao, yeye pia hamu yake kubwa ilikuwa ni ile ambayo watu wengi walikuwa nayo, alikaa kimya akisubiri wapewe nafasi ya kuongea. Muda ulipofika aliyejitambulisha kwa jina la Padri Silvanio alipewa nafasi ya kuanza kuzungumza.

Alichokifanya mwanzo na kilichowashangaza watu wote kabla hajaongea ilikuwa ni kuzungusha mkono wake nyuma ya shingo kisha kuanza kubandua kitu kichwani mwake, kumbe alikuwa amevaa sura ya bandia iliyobanduka kadiri mkono wake ulivyokwenda mbele, ilipomalizika, sura ya mzee Jonathan Magafu ikajitokeza!
“Mh! Huyu si ni Jonathan Magafu aliyedungwa sindano ya sumu na kufa?”
“Ni kweli mimi ndiye, sikufa, ni mchezo ulichezwa, maiti za watu wengine ziliwekwa kwenye kitanda cha kifo umeme ulipozimika ghafla!”

“Duh! Na huyu?”
Aliyeonekana kuwa sista Mariastela akazungusha mkono nyuma ya shingo yake kama alivyofanya mwenzake na kuanza kubandua sura ya bandia, alipomaliza sura ya Andrew Kisanji ikajitokeza, kila mtu ndani ya ukumbi wa mkutano akabaki mdomo wazi kugundua kuwa kumbe Dk. Viola na nduguye Vanessa walikuwa hai, walichokifanya ni kubadilisha sura na kurejea nchini Tanzania katika sura na vitambulisho vya watawa Padri Silvanio na Sista Mariastela.

“Nimenyoosha mikono! Sina tena ubishi, ninyi ni Dk. Viola na Vanessa?” Denis Crapton aliongea akiwa ameshika mikono kichwani.
“Ni sisi Denis, tusamehe!”

“Hamstahili kusamehewa hata kidogo, wauaji wakubwa!”
“Tunahitaji msamaha!”
“Haiwezekani!” alikataa Denis Crapton akipiga juu ya meza kuonyesha hasira aliyokuwa nayo.

“Kilitokea nini pale chumba cha kudungiwa sindano ya sumu baada ya umeme kukatika?”
“Miili mingine iliwekwa juu ya vitanda, sisi tukavishwa sura tulizozibandua na kutokea mlango wa nyuma!”
“Nani alifanya mipango yote hiyo?”
“Yousef Emmanuel!”
“Ni nani huyo?”

“Raia wa Israel, binadamu mwenye akili nyingi kuliko, ndiye aliyesaidia sisi kuepuka kifo siku ile kisha kutusafirisha kwa hati bandia za kusafiria hadi Nairobi ambako tulipanda ndege na kuelekea Bogota, Columbia.”
“Huko kilitokea nini?”

“Tayari alishawatafuta watawa katika Mji wa Santa Marta, akatengeneza sura zilizofanana nao, kisha kutuvisha sisi sura hizo, tukiwa Bogota tuliendelea na safari hadi Santa Marta walikoishi watawa hao, tukazivua sura zao tulipoingia Santa Marta, kisha kwenda kwenye Parokia yao tukijifanya watu tuliokuwa tukifatuta yatima na wajane wa kuwasaidia, wakatukaribisha vizuri ndani ya nyumba yao, humo ndimo tuliwaua na kuwatupa kisimani, baada ya hapo tukazivaa tena nyuso zao watu wakawa wanaona kama vile Padri Silvanio na Sista Mariastela bado wapo kumbe walishakufa!”
“Halafu kikafuata nini?”

“Yousef akatupigia simu kuwa Denis Crapton alikuwa ametuma watu wa kuja kuwaua watawa hao sababu yeye pia aliutaka utajiri huo!”
“Alijuaje?”

“Alikuwa na uwezo wa kuingia kwenye simu ya mtu kwa kutumia teknolojia na kujua kila kitu alichowasiliana!”
“Ikawaje?”
“Watu wale walipokuja tuliwapokea mimi na mwenzangu, usiku Yousef Emmanuel alikuja kutuchukua kwa gari yake, baada ya sisi kuondoka watu hao walichoma nyumba kwa lengo la kuwaua watawa ambao wakati huo tulikuwa ni sisi!”
“Mkaelekea wapi?”

“Tukaeleka Bogota, baadaye Los Angeles tukitumia hati ya kusafiria za Padri Silvanio na Sista Mariastela, kisha kuunganisha hadi jijini Dar es Salaam ambako tulirithishwa utajiri wetu, ukarejea tena mikononi mwetu, tukaendelea kufaidi maisha bila mtu yeyote kugundua, mioyoni tukifahamu lazima huyu angerejea tena!”
“Huyu nani?”

“Denis Crapton, aliutaka utajiri wetu kwa nguvu, kwa kutumia vyanzo vyetu tulisikia juu ya upelelezi alioufanya huko Santa Marta na kugundua kuwa mifupa iliyokuwa ndani ya kisima ni ya watawa wawili, hapo ndipo tukaona hapakuwa na njia, bora tuuze kila kitu na kutoroka.”
“Ninyi wanawake ni wajanja sana, dunia haijawahi kushuhudia binadamu mwenye akili nyingi kama ninyi!”
“Tunaomba tusamehewe kwa yote tuliyotenda!”

“Wawekeni mahabusu, adhabu yao ya kifo iko palepale, kesho wafikishwe mahakamani!” mkuu wa jeshi la polisi nchini Tanzania aliamuru, Dk. Viola na Vanessa wakiwa na sura za wazee wa Kijapani wakashushwa hadi ghorofa ya chini ambako walitupwa mahabusu huku wakilia machozi kama watoto wadogo, Denis Crapton akajisikia mshindi, utajiri wa dola bilioni mbili ulikuwa katika safari ya kurejea mikononi mwake.

JE, nini kitaendelea? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.

Leave A Reply