MABODIGADI… DIAMOND ANAWAFUNIKA JAY Z, DRAKE ?

KUJITENGEN­EZEA hesh­ima kwa watu maarufu ni jambo lenye umuhimu mkubwa. Ndio maana zamani tulikuwa tunaona baadhi ya wasanii Bongo wa­najaribu kujionesha wakiwa kwenye magari au nyumba za kifahari katika video zao hata kama kiuhalisia ha­wana.  

 

 

Walichokuwa wanajaribu kukipeleka kwa hadhira ni ule utofauti kwamba yeye ni msanii. Yeye ni tofuati tu na watu wa kawaida. Ni kioo cha jamii hivyo lazima ajitengenezee mazingira ya kuonekana tofauti na watu wa kawaida, huo ndio ustaa. Hii ndio maana waswahili waliibuka na ule msemo wa umaridadi unaficha umasikini.

 

Hata kama huna lakini kama umejitengenezea mazingira ya kuonesha unacho, kila mtu atakuheshimu. Atakupa ile hadhi ya wenye nacho hata kama huna.

Hili halipo Bongo tu ndio maana wasanii maarufu duniani hususan Marekani ambako kuna wasanii wengi maarufu, wamejitengenezea heshima fulani ambayo inawatofautisha na watu wa kawaida. Msanii kama Rick Ross, unapokwenda nyumbani kwake ni kama vile Ikulu.

 

Huwezi kumfikia kirahisi. Utakutana na ulinzi mzito wa askari wa getini, utakutana na ulinzi binafsi wa bodigadi wake ambaye hutembea naye kila anapokuwa na mizunguko. Akiwa kwenye shoo, akiwa kwenye mizunguko yake binafsi.

 

Msanii ‘anaji-brand’ kwenye jamii. Haonekani hovyo hovyo. Akionekana sehemu unakuwa na hamu naye, sio msanii kila siku upo klabu. Msanii upo kijiweni unacheza bao na masela kila siku, ni tatizo. Ndio maana nasema msanii lazima uwe na muonekano tofauti.

 

Kibongobongo, yupo mtoto wa Tandale, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, kwa kiasi kikubwa anaonekana kujua kujitengeneza. Anajua kutengeneza ‘image’ yake kwa hadhira.

Nimemfuatilia tangu anaanza harakati za muziki. Alianza akijua anataka kuwa nani, apite njia gani ili aweze kufikia pale mahali anapopataka.

 

Ndio maana aliona si vyema kufanya muziki peke yake. Lazima awe na menejimenti ambayo itakuwa inamsimamia yeye katika muziki wake, kupokea na kuandaa matamasha mbalimbali ya muziki kama ambavyo sasa hivi anatikisa na Tamasha la Wasafi Festival.

 

Diamond ni miongoni mwa wasanii wachache sana walioweza ‘ku-maintain’ suala la kuwa na ulinzi binafsi. Kabla yake, walifanya wasanii kama Mr Blue na Mr Nice ambao baadaye walichemka, kwa sasa wanatembea tu kawaida kama vile mimi ninavyotembea.

 

Kwa kujitengenezea brand hiyo, Diamond aliweka pia msimamo wa shoo zake kwa kuweka kiwango cha juu kwa shoo za nyumbani na kiwango cha juu zaidi kwa shoo zake za nje ya nchi. Ukienda na kiasi ambacho kiko chini ya utaratibu wake hafanyi shoo.

 

Hiyo imemfanya aweze kutengeneza heshima kubwa na wanaondaa matamasha mbalimbali kujua kwamba kama unamtaka Diamond ujipange. Diamond ana msafara wa uongozi, DJ, wapiga picha wake, walinzi binafsi na wapambe wengine. Yaani inabidi unapomualika ujue kabisa utabeba gharama za watu wasiopungua kama kumi hivi.

 

Kutembea na walinzi binafsi kuna faida japo wengine wanaona kama ni ufahari, wanaona kama ni kujionesha lakini kwa upande mwingine, kutembea na ulinzi kwa msanii mkubwa ni jambo lisiloepukika. Msanii mkubwa kama Diamond ambaye akaunti yake benki inasoma si chini ya shilingi Bilioni 7, anatembeaje kiboyaboya? Si ufahari bali kujilinda ni suala ambalo kila mmoja wetu anapaswa kujilinda kutokana na nafasi yake.

Diamond ameshafanya mambo mengi makubwa ambayo ilikuwa ni nadra kusikia yamefanywa na msanii kutoka Tanzania. Amefanya kolabo nyingi tu na wasanii wa Marekani, ameshakuwa na urafiki na wasanii wa Afrika Kusini, Nigeria na kwingineko hivyo ni dhahiri kwa sasa anaweza kujishindanisha na wasanii wakubwa kutokana na jinsi alivyojitengeneza.

 

Anavaa kama msanii Jay Z, anaishi kwenye mjengo wa gharama kama vile wanavyoishi mastaa kibao wa Marekani. Diamond ana walinzi binafsi wengi kuliko hata wasanii wa Marekani kiasi cha mimi kujiuliza kwamba, anaweza kuwafunika Drake na Jay Z kwa ulinzi?

Jay Z alikuwa akilindwa na mlinzi mmoja, marehemu Norman Oosterbroek kama vile ilivyokuwa kwa Diamond na Mwarabu Fighter ambaye kwa sasa wameshaachana naye. Jay Z taarifa zinaonesha kwamba baada ya kuachana na Norman alipata mlinzi mwingine binafsi ambaye ndiye anatajwa kumlinda mpaka sasa.

 

Diamond kwa sasa kwenye msafara wake wowote anakuwa na ‘timu’ ya mabaunsa waliovalia suti kali wasiopungua watano. Drake vivyo hivyo anatembea na bodigadi mmoja, wasanii wengine wengi tu wa Marekani nao wametajwa kutembea na mlinzi mmoja je, anawafunika Jay Z, Drake na wasanii wengine wengi wa Marekani? Tutafakari pamoja na tupate majibu yetu binafsi

Makala: Erick Evarist

Toa comment