The House of Favourite Newspapers

Mabosi Yanga Kuwajadili Makambo, Ndemla

0

KAMATI ya Utendaji ya Yanga leo Jumatatu inatarajiwa kukutana kwa ajili ya kupitia ripoti ya usajili ambayo Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji Luc Eymael, ameikabidhi mapema kwa ajili ya kuanza mikakati ya kukisuka kikosi hicho katika kujiandaa na msimu mpya.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu kocha huyo akabidhi ripoti hiyo kabla ya kurejea nyumbani kwao kwenda kufunga ndoa na mchumba wake mara baada ya ligi kusimamishwa kupisha Virusi vya Corona.

 

Majina manne hadi hivi sasa yapo kwenye orodha ya usajili mpya wa kikosi hicho ambayo ni Heritier Makambo anayekipiga Horoya ya Guinea na Tusile Kisinda anayeichezea AS Vita, pamoja na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ (Azam FC) na Said Ndemla (Simba).

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu na kuthibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, kamati hiyo inatarajiwa kukutana kwa mara ya kwanza leo kwa ajili ya kupitia ripoti ya kocha aliyoiacha wakati ligi ikiwa imesimama.

 

Mwakalebela alisema kuwa mengi yanazungumzwa kuhusiana na usajili huku baadhi ya majina yakitajwa, lakini kila kitu kitajulikana baada ya kikao hicho cha utendaji.

 

Aliongeza kuwa ni ngumu kutaja majina ya wachezaji ambao wametajwa kwenye usajili wa kocha bila kikao kufanyika na kupitia ripoti hiyo ambayo itatoa mwongozo katika usajili huo mpya.

 

“Kila kitu kitajulikana baada ya kikao chetu cha kesho (leo).

 

Katika kikao hicho, mengi yatajadiliwa tofauti na hilo la usajili ambalo linasubiriwa na mashabiki wengi wa Yanga wanaotamani kuona timu yao inasukwa vema.

 

“Hivyo, wasubirie kila kitu kitakwenda sawa, kikubwa Wanayanga wanatakiwa wawe wavumilivu katika kipindi hiki ambacho uongozi kwa kushirikiana na kocha wanaweka mipango sawa katika kuisuka Yanga mpya ya ubingwa msimu ujao,” alisema Mwakalebela.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply