The House of Favourite Newspapers

Mabosi Yanga Wanasa Mafaili Ya Waarabu

 

YANGA haitaki utani hata kidogo! Ndivyo utakavyoweza kusema kwa timu hiyo baada ya kunasa mafaili ya wapinzani wao Pyramids FC ya jijini Cairo, Misri.

 

Hiyo ni baada ya droo ya Caf iliyochezeshwa juzi usiku huko Misri ambayo Yanga haikuwa na mwakilishi yeyote katika droo hiyo ambapo imepangwa kucheza na Pyramids kwenye Hatua ya Mtoano ya Kombe la Shirikisho.

Yanga itacheza michuano hiyo ya Shirikisho baada ya kuondolewa na Zesco United ya Zambia kwenye Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alisema kuwa tayari wameanza kuweka mikakati ya ushindi wa mechi ya nyumbani itakayochezwa Oktoba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Mwakalebela alisema tayari wanafuatilia kwa ukaribu wapinzani wao hao katika kuelekea mchezo wa nyumbani, ni timu changa iliyoanzishwa mwaka 2008 na msimu uliopita wa ligi walimaliza wakiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo.

 

Aliongeza kuwa pia timu hiyo wameifuatilia kwenye michezo ya Shirikisho waliyocheza ambao wameonekana hatari nyumbani na ugenini huku wakipanga kutafuta video za mechi zao kwa ajili ya kumpatia kocha wao, Mkongomani, Mwinyi Zahera.

 

“Pyramids tunafahamu ni timu iliyoanzishwa mwaka 2008 na msimu uliopita walimaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Misri na kupata nafasi hiyo kushiriki Shirikisho.

 

“Kingine ni timu yenye utajiri mkubwa, mapema mwaka huu tunafahamu ilinunuliwa na matajiri kutoka Uarabuni, lakini hilo halitufanyi Yanga tuwaogope, tunafahamu hii ni mara yao ya kwanza kushiriki michuano ya kimataifa.

 

“Kwani tuna uzoefu wa michuano hii mikubwa hasa kukutana na Waarabu, miaka ya hivi karibuni tulicheza na timu kutoka Misri ambazo ni kubwa kama vile Al Ahly na Zamalek, kiukweli tulijitahidi kutoa ushindani mkubwa.

 

“Pia tumepanga kumpatia video za mechi zao za mwisho za Pyramids kocha wetu kwa ajili ya kuwasoma zaidi,” alisema Mwakalebela.

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.