The House of Favourite Newspapers

Mfungwa Aliyesamehewa na JPM Afariki Kimiujiza Akijiandaa Kwenda Ikulu

Kulia ni Maziku enzi za uhai wake.

  

MACHOZI yametawala kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha maajabu cha mfungwa aliyeachiwa huru hivi karibuni kwa msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’, Maziko Juma Masanja (62), Uwazi lina habari kamili.

Masanja alikuwa miongoni mwa wafungwa 1,812 walioachiwa huru na Rais Magufuli katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 56 ya Uhuru zilizofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri

mjini Dodoma, Desemba 9, mwaka jana ambapo alikutwa na umauti wakati akijiandaa kwenda Ikulu ya Magogoni, Dar kwa ajili ya kumshukuru rais kwa msamaha huo.

Alikuwa akitumikia kifungo cha maisha baada ya kufungwa mwaka 1980 kufuatia kukutwa na hatia katika kesi ya mauaji ya mgoni wake, tukio alilolitenda mwaka 1977.

Ndugu wa marehemu wakiwa na jeneza lenye mwili baada ya kuutoa kwenye chumba cha kuhifadha maiti.

KIFO CHAKE

Habari zenye kuumiza mioyo zilieleza kuwa, kifo cha Masanja kilikuwa cha ghafla kwani kilitokana na kugongwa na bodaboda kimaajabu eneo la Ubungo jijini Dar kwani dakika chache tu alikuwa na mwenyeji wake na kitendo cha kufumba na kufumbua akawa amepoteza maisha, hivyo kushangaza wengi.

 

SIMULIZI YA NYUMA

“Masanja alikuwa ni mkazi wa Kijiji cha Bupandwamhela, Sengerema jijini Mwanza.

“Alikamatwa mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 21 kisha akahukumiwa kifungo cha maisha mwaka 1980 akiwa na umri wa miaka 24.

“Masanja alikuwa anaishi na mkewe kijijini hapo. Siku ya tukio alionekana akiwa

kusafisha shamba lake.

Maziku enzi za uhai wake.

 

FUMANIZI

“Baada ya kumaliza kazi za shamba, alirudi nyumbani akiwa amechoka, lakini alipofika kwake akakuta mtoto wake mdogo wa kike akiwa ametelekezwa, kwani alikuwa analia.

“Alipotaka kuingia ndani, alishangaa kuona mwanaume akiwa amebeba stuli akitoka ndani kwake.

“Inaonekana mke wake alikuwa ameingiza mwanaume ndani ya nyumba yao.

“Yule mgoni alibeba ile stuli kwa ajili ya kujihami, kwani alipokutana na Masanja uso kwa uso, alimpiga nayo kichwani na kusababisha kuanguka.

“Yule mgoni alikimbia, lakini Masanja alijikusanya, akanyanyuka na kuanza kumkimbiza mgoni wake.

Moja ya nyaraka za kifungo chake gerezani.

“Alipomfikia, ndipo akamkatakata mapanga kisha baadaye alifariki dunia,” alisimulia mmoja wa ndugu wa Masanja aliyeomba hifadhi ya jina kwa maelezo kwamba si msemaji wa familia.

Msimuliaji huyo aliendelea kusimulia kuwa, baada ya tukio hilo, Masanja alikamatwa na kufungwa katika magereza mbalimbali nchini ikwemo Gereza la Butimba (Mwanza), Uyui (Tabora), Isanga (Dodoma) na Ukonga (Dar).

Aliendelea: “Mwaka 2001, Masanja alisumbuliwa sana na tatizo la kibofu cha mkojo, ikabidi ahamishiwe Gereza la Ukonga ili awe karibu na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Jeneza lenye mwili wa marehemu.

 

“Akiwa Ukonga, alikuwa akitembelewa mara kwa mara na Mchungaji wa Kanisa la Assembly of God lililopo Ubungo.

“Hata alipoachiwa huru kwa msamaha wa rais, alichukuliwa na mchungaji huyo na kuishi naye.

“Baada ya kutoka gerezani, Masanja alikwenda hadi kijijini kwao, Bupandwamhela na kukuta familia yake ilishasambaratika na wengine walishahama siku nyingi huku yule mtoto wake wa kile aliyemkuta analia siku ya tukio, akiwa ameolewa mkoani Tabora.

 

“Kutokana na kukosa sehemu ya kuishi kule kijijini Bupandwamhela, ilibidi Masanja arudi Dar kwa mchungaji wake.

“Januari 7, mwaka huu, Masanja baada ya kukaa kwa muda mrefu, aliamua kumtafuta rafiki yake ambaye anaishi Madale (nje kidogo ya Jiji la Dar), waliongozana na mchungaji hadi Madale kwa ajili ya kumtafuta rafiki yake huyo.

“Wakiwa wanarudi kutoka Madale, walipofika Ubungo kwa mchungaji huyo, mchungaji aliingia ndani, lakini Masanja hakuingia, akawa kama amesimama getini.

 

AJALI YA AJABU

“Dakika chache baadaye aliondoka na haukupita muda mrefu, mchungaji huyo alipigiwa simu na wasamaria wema kuwa Masanja amegongwa na bodaboda kiajabu maana hata haikuwa sehemu ya kugongwa na pikipiki haikuwa spidi hata kidogo.

“Mchungaji huyo alikwenda eneo la tukio na kustaajabu kumuona Masanja aliyeachana naye dakika chache akiwa chini huku mguu wake ukionekana kuumia zaidi.

 

MASANJA AKATA ROHO NJIANI

“Mchungaji huyo alimchukua Masanja akiwa hai na kumkimbiza Hospitali ya Sinza-Palestina (Hospitali ya Wilaya ya Ubungo), lakini wakiwa njiani, Masanja alikata roho, jambo lililozidi kumstaajabisha mchungaji huyo kwani hakuamini alichokuwa akikishuhudia ndani ya muda mfupi.

“Hivyo ndivyo kilivyokuwa kifo cha Masanja, kila mtu kilimshangaza na mchungaji huyo aamini kama Masanja angeingia ndani baada ya kurudi kutoka Madale, asingegongwa na pikipiki.“

 

SAFARI YA IKULU

Mtu mwingine aliyekuwa karibu na Masanja enzi za uhai wake aliyeomba hifadhi ya jina lake alimwambia mwandishi wetu kuwa, kuna wakati marehemu alijipanga kwenda Ikulu kumshukuru Magufuli hasa baada ya kuona wenzake kama vile Babu Seya na wanaye wameenda, lakini kabla ya kutimiza hilo, Mungu akamchukua. Marehemu Masanja alizikwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika Makaburi ya Madale jijini Dar.

 

Stori: IMELDA MTEMA, Dar

VIDEO; FUATILIA TUKIO HILO HAPA

Comments are closed.