The House of Favourite Newspapers

Machozi! Watoto Walia Baba Yao Kufia Mikononi mwa Polisi -Video

MACHOZI! Hivyo ndiyo unavyoweza kusema kufuatia watoto wa dereva wa bodaboda, Thobias Joseph a.k.a Mchuwau, mkazi wa Temeke-Mikoroshini jijini Dar, kuangua kilio wakidai baba yao kufia mikononi mwa polisi baada ya kutuhumiwa kuwa mwizi wa simu.

 

Tukio hilo la kuhuzunisha lilijiri Oktoba 7, mwaka huu maeneo hayo ambapo ilisemekana kuwa Thobias na wenzake wawili walikamatwa na polisi wa Kituo cha Chang’ombe wakituhumiwa kuiba simu ya askari.

 

Katika msiba huo, watoto walioachwa na marehemu huyo, Joseph (8) na Maria (11), waliwatoa machozi waombolezaji kwa jinsi walivyokuwa wakimlilia baba yao aliyefia mikononi mwa polisi ambapo wengi wamekuwa wakiona jeshi hilo kama sehemu ya usalama.

 

Kuhusiana na tukio hilo, ilidaiwa msibani hapo kuwa, baada baba wa watoto hao na wenzake kutiwa mbaroni, walihojiwa ili waeleze ilipo simu hiyo ambapo baada ya mahojiano ilisemekana kuwa Thobias ndiye aliyeonekana kuhusika, ndipo akaanza kupewa kipigo.

 

Akizungumza na Risasi Jumamosi, mmoja wa vijana waliokamatwa wakiwa na Thomas aliyejitambulisha kwa jina la Onesmo Ayubu maarufu kama Mbogasaba alisema;

“Tulipokamatwa tuliingizwa mahabusu na baada ya muda tukatolewa na kupelekwa kwenye chumba fulani kwa ajili ya kuhojiwa, ambapo mwenzetu alionekana kama alihusika zaidi kwenye tukio hilo hivyo walianza kumpiga kwa marungu.

 

“Wakati akiendelea kupigwa, sisi wengine tulirudishwa mahabusu na kumuacha mwenzetu.”

Kwa upande wa mke wa marehemu, Amina Abdallah (30) alielezea alivyoachana na mume wake saa chache kabla ya mkasa huo.

 

“Siku ya tukio, mume wangu kama kawaida yake asubuhi alidamkia kwenye kazi yake ya bodaboda na kwa kuwa si mbali na hapa nyumbani, kulipopambazuka nilimtuma mwanangu Joseph akachukue pesa kwa ajili ya matumizi, na kweli alifanya hivyo.

 

“Nikiwa ninasubiria, ghafla rafiki zake walikuja na kuniambia mume wangu amekamatwa na polisi akituhumiwa kuiba simu na amepelekwa Kituo cha Chang’ombe.

“Niliwasiliana na ndugu zake ambao tuliongozana hadi hapo kituoni na kumuulizia ambapo kwanza walituambia hawana taarifa zake.

 

“Tulipozidi kuwauliza na kuwasisitiza kuwa amefikishwa kituoni hapo akiwa na wenzake, mmoja wa maafande alitutoa chemba na kutuambia mume wangu alikimbizwa Hospitali ya Muhimbili kutokana na hali yake kuwa mbaya.

“Tulijipanga na kuelekea Muhimbili ambapo tulipofika tuliulizia mapokezi na kuwatajia jina la mume wangu na kuwaambia alifikishwa hapo na polisi ambapo walituambia tukaanze kumuangalia mochwari.

 

“Kweli tulipofika mochwari tuliukuta mwili wa mume wangu, ukweli iliniuma sana.

“Mume wangu ameniachia watoto wawili hawa pamoja na mama yake ambaye ni bibi kizee mwenye umri wa miaka zaidi ya mia moja, sasa sijui nitawaleaje?” Alisema mke wa marehemu huku akilia.

 

Baada ya kuzungumza na mke wa marehemu, wanahabari wetu walizungumza na Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mkwinda uliopo eneo hilo, Salehe Lwimbo ambaye alisema anasikitishwa na mwananchi wake huyo kufa kifo hicho kwa sababu siku zote alizoishi mtaani hapo zaidi ya miaka 30, hajawahi kumsikia katika matukio ya uhalifu.

 

“Ukweli huyu marehemu amezaliwa hapa mtaani namuona na hata siku moja sikuwahi kumsikia wala kupata kesi yake ya uhalifu, lakini ndiyo hivyo tena, maisha yana siri nyingi, huwezi kujua,” alisema mjumbe huyo.

 

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Kamishna Msaidizi (ACP) Amon Kakwale alisema;

“Hilo tukio limenifikia na hao wanaosema huyo marehemu amefia mikononi mwa polisi, huo ni uzushi, hakuna kitu kama hicho.

 

“Ukweli ni kwamba huyo Thomas alikwapua simu ya askari na kukimbia, katika harakati za kukimbia ndipo wananchi wengine nao wakaanza kumuunganishia.

“Wakati anaendelea kukimbia, wananchi walifanikiwa kumkamata na kumshushia kipigo mpaka walipofika polisi na kumuokoa ambao walimleta Kituo cha Chang’ombe na kumfungulia kesi ya wizi.

 

“Kwa kuwa alifikishwa akiwa taaban, baada ya kupigwa na hao wananchi, polisi kama kawaida yetu baada ya kumfungulia kesi, tulichukua jukumu la kumpeleka hospitali ili akapate matibabu ndipo akaaga dunia, huo ndiyo ukweli.

 

Marehemu alizikwa Jumatano iliyopita katika Makaburi ya Chang’ombe-Unubini maarufu kama Maduka-Mawili, Temeke jijini Dar.

STORI: Richard Bukos na Khadija Bakari

Comments are closed.