The House of Favourite Newspapers

Madaraka Matamu, Lakini Machungu Kwa Mugabe na Laurent Gbagbo

0
Aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe.

MWAKA 1789 ulikuwa wa kihistoria kwa Ufaransa na dunia kwa ujumla kutokana na mapinduzi makubwa yaliyotikisa nchi hiyo. Mapinduzi hayo yalikuwa ya kumuondoa madarakani Mfalme Louis wa XVI ambaye alianza kulewa madaraka akila na kusaza pamoja na mkewe, Marie Antoinette.

 

Wakati wananchi wa Ufaransa wakipiga kelele kuhusu hali ngumu ya maisha na matatizo mengine mengi, Mfalme Loius hakupenda kusikia la mtu. Aliendelea kutumbua maisha na wapambe wake wa karibu hawakupenda kumwambia ukweli wakihofia kitumbua chao kisiingie mchanga. Hivyo wakauchuna. Siku moja mke wake akiwa kwenye kasri lao kubwa, aliona barabara imefurika wananchi waliokuwa wanaandamana kuelekea Ikulu.

 

Alipouliza kuna nini, aliambiwa wananchi hao wamekuwa wakilalamikia matatizo lukuki kwa muda mrefu, lakini wakawa hawasikilizwi. Kwa majigambo akasema, “hamna keki muwape”.

Laurent Koudou Gbagbo akiwa mikononi mwa Mwanajeshi.

Kauli hiyo iliudhi wananchi wengi wakiwemo walinzi wake na kuanzia hapo hali ya nchi ikawa tete. Walinzi watiifu kwa mfalme walipambana vikali na waandamanaji kwa silaha za moto, lakini walipobaini wanaua watu wasio na hatia, walitupa silaha zao chini. Hatua hiyo ilienda pamoja na kuuungana na waandamanaji kumkabili mfalme ambaye alikiona cha moto.

 

Ikulu ilikuwa chungu. Ilipofika mwaka 1793 mfalme alikufa kifo cha aibu. Hatupendi kuingia kwa undani kwenye hili, lakini itoshe kusema, madaraka ni mazuri, lakini machungu. Ninasema hivi kwa sababu viongozi wanapoingia madarakani huapa kulinda na kuitetea katiba ya nchi kwa kuzingatia pia ukomo wa uongozi. Hata hivyo, kinachosikitisha ni kwamba wengi wao huenda tofauti na viapo vyao na mwisho hujikuta wakiishia pabaya kiuongozi.

 

Mfano mzuri na wa hivi karibuni unamhusu aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe. Alipoingia madarakani wananchi wengi walimfurahia na kumpenda. Lakini alipotakiwa kuondoka madarakani kwa kuzingatia katiba na taratibu za nchi, alibadilika na hakupenda kabisa kusikia suala hilo. Kwa sababu hiyo aliendelea kung’ang’ania madaraka licha ya kuongoza nchi kuanzia mwaka 1980 na mwisho w

 

ake ameondolewa kwa aibu, kwa maandamano na kuzomewa hata na watoto wadogo. Alipotangaza kuachia madaraka, nderemo na vifijo vilitawala nchi ya Zimbabwe huku wananchi wakionekana ‘kugongeana tano’ na wanajeshi.

 

Uongozi wa aina hii ya Mugabe si mzuri kwani hautoi taswira njema katika kutetea mfumo wa utawala bora na demokrasia kwa ujumla wake. Mugabe alitakiwa awe mlezi wa kutetea utawala bora kwa kuruhusu uongozi wa kuachana madaraka kwa njia za kidemokrasia badala ya kutumia mabavu. Kwa kuonesha udhaifu huo, Mugabe aliyeheshimika Afrika ameondoka kwa aibu ambapo nderemo na vifijo vilitawala baada ya kuachia ngazi. Ifahamike pia kwamba tatizo hili la ulafi wa madaraka lilisababisha kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi ambaye aliingia madarakani mwaka 1969 auawe.

 

Gaddafi kama viongozi wa mwanzo mwanzo barani Afrika, alilewa madaraka na kumpofusha macho na kushindwa kusoma alama za nyakati. Pamoja na mazuri mengi aliyofanya Libya, lakini ulafi wa madaraka na kutopenda kuruhusu uongozi wa kuachiana uligharimu maisha yake. Wakati mmoja
alipotembelea Uganda na kufungua msikiti mkubwa, Gaddafi alitamani yeye, Rais Yoweri Museven na Mugabe waongoze milele.

 

Hiyo ilikuwa ndoto yake ingawa haikutimia kwake wala Mugabe. Kazi ibaki kwa Rais Museveni kuanza kujipima kwa kusoma upepo unavyokwenda. Tunafahamu kuwa aliingia madarakani mwaka 1986, lakini hadi leo hii anaendelea kupiga jaramba na haonekani kuondoka madarakani leo wala kesho.

 

Swali ni je, tamaa ya madaraka itamponza? Je, atakubali yamkute yanayowakuta wakongwe wenzake kama Mugabe au atasoma maandishi ukutani? Kwa ushauri tu ni kwamba ingependeza kama angekaa pembeni mapema kabla mambo hayajamuendea mrama kama wenzake.

 

Asikubali kusubiri hadi mafuriko yamsombe kama ilivyotokea kwa aliyekuwa Rais wa Guinea, Yahya Jammeh ambaye pia aliondoka madarakani kwa aibu. Suala jingine ambalo linasumbua viongozi wa Afrika ni pamoja na kuchezea katiba.

 

Kwa sasa suala hili linaonekana ni jambo la kawaida na lisiloogopeka tena. Angalia yaliyotokea Burundi na yanayoendelea kutokea Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC). Kimsingi yanasikitisha wapenzi wa demokrasia. Pamoja na nchi hizo kuongozwa na vijana, lakini wamekuwa mfano mbaya kwa kuchezea katiba halali za nchi ili wasiondoke madarakani. Utamaduni huu si mzuri hata kidogo.

 

Ni lazima viongozi wenyewe wabadilike na kuhakikisha wanaheshimu katiba za nchi zao. Kama katiba inawaruhusu kuongoza vipindi viwili viwili waache kujiongezea muda kinyemela kwani kwa kufanya hivyo ni chanzo cha vurugu zisizo na msingi. Viongozi wanaofanya hivyo wajaribu kujifunza kutoka Tanzania kwa sababu imejitahidi kuheshimu katiba tangu Mwalimu Julius Nyerere aondoke madarakani. Ingawa yapo majaribu ya hapa na pale, lakini viongozi husika wamejaribu kuyakwepa ili kuhakikisha taifa haliingizwi kwenye matatizo yasiyo na ulazima. Kwa maoni na ushauri wasiliana nasi kwa namba 0718 981221

Leave A Reply