The House of Favourite Newspapers

Madenti Vyuo Vikuu Wanavyoambukizwa UKIMWI

TUNAIMALIZIA ripoti yetu ya uchunguzi tuliyoianza wiki mbili zilizopita. Kama mnavyokumbuka, kwenye matoleo mawili yaliyopita tuliona jinsi ambavyo wanafunzi wa vyuo vikuu wanavyoambukizwa magonjwa ya zinaa ukiwemo Ukimwi na homa ya ini kutokana na mazingira yanayowazunguka.

 

Tuliuona sehemu ya ushuhuda wa yule mama ambaye alituelezea jinsi mume wake ambaye ni profesa anayefundisha moja ya vyuo vikuu vya hapa jijini Dar alivyomuambukiza virusi vya ugonjwa huo hatari huku akiendelea kutembea na wanafunzi wake tofautitofauti.

 

Kabla hatujaenda mbali zaidi, tumalizie ule uchunguzi wa kikosi chetu cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) kilipofika kwenye baa moja maarufu iliyopo karibu na moja ya chuo kikuu ili kujiridhisha jinsi wanafunzi hao wanavyojirahisi kwa kupenda starehe.

 

Tuliishia pale ambapo OFM ameahidiwa kulengeshwa kwa mmoja wa wanafunzi na mhudumu wa baa hiyo. Alipofika tu huyo mwanafunzi, akampeleka mezani kwa kamanda wa OFM. Kamanda akaanza kupiga naye stori:

 

OFM: Karibu sana mrembo kuwa huru na utumie chochote unachopenda.

MWANAFUNZI: Asante sana, mimi natumia red wine.

OFM: Dada mletee hiyo chupa kubwa…

 

Baada ya kuletewa kinywaji hicho, denti huyo hakuwa na hiyana tena. Baada ya kumuona kamanda wa OFM ni mtu mwenye mwili wake ambaye ameweka funguo ya gari mezani, alikunywa na kuwa tayari kulala na kamanda wa OFM kwa siku hiyo.

OFM: Kwa hiyo tutalala wote leo?

 

MWANAFUNZI: Hakuna neno lakini itabidi unipe kama shilingi elfu hamsini maana kesho nilikuwa na mpango wa kwenda kutengeneza nywele mpenzi.

OFM: Sawa lakini tatizo langu baby mimi huwa siinjoi na zana hivyo utanisaidiaje?

MWANAFUNZI: Mh! mbona mtihani huo, itabidi basi uongeze hela fanya laki nitakufurahisha mpenzi.

 

OFM: Nashukuru sana mpenzi hapa pesa siyo tatizo sema lingine.

Baada ya kubadilishana namba, kula na kunywa hadi usiku wa saa saba, kamanda huyo alilazimika kumrudisha katika hosteli zilizopo ndani ya chuo hicho na kumzuga kuwa atalala naye siku nyingine kwani siku hiyo hayuko sawa.

 

Mwanafunzi huyo alileta kipingamizi lakini kamanda wa OFM akajiongeza fasta baada ya kumsoma kwamba inaonekana hana pesa ya supu asubuhi, akalazimika kumuachia shilingi elfu kumi. Akakubali kwenda kulala.

 

Baada ya siku mbili kupita, kamanda mwingine wa OFM alikwenda kwenye baa ileile na kumlia mingo mwanafunzi yuleyule.

Kwa kuwa yule mhudumu alishafahamiana na kamanda wa kwanza, alimuomba amkutanishe yule mwanafunzi wa awali na yule kamanda wa pili.

 

Mambo yalikuwa yaleyale. Kamanda wa pili akatajiwa bei zilezile, akakubali. Kama hiyo haitoshi, mwanafunzi huyo akamkaribisha na rafiki yake na kumtambulisha masomo anayosomea chuoni hapo.

Mazungumzo yakaenda hivyo lakini kuna wakati yule mwanafunzi mwenyeji alikwenda uani, muda huohuo kamanda wa OFM akajaribu kumuomba namba yule denti mpya aliyetambulishwa.

 

Denti huyo mpya akatoa namba kiulaini na hapohapo akaanza kueleza shida zake kwa kamanda kupitia ujumbe mfupi.

Mazungumzo na vinywaji viliendelea hadi usiku mnene ndipo kamanda alipoamua kuwarudisha wawili hao hosteli moja chuoni hapo wanapoishi.

 

Baada ya kujiridhisha kwamba wanafunzi hao wapo tayari kuuza utu wao sababu ya fedha, OFM ililazimika kuhamia kwenye baadhi ya wanachuo ambao inasemekana wanatembea na yule profesa ambaye mkewe alithibitisha kwamba anaishi na virusi vya Ukimwi.

Kikosi kazi cha OFM kiliweza kufika kwenye nyumba aliyopangiwa na profesa huyo mmoja wa wanafunzi hao ambapo majirani zake walitoa ushirikiano kwa kutaja muda anaokuja profesa huyo na kuingia naye.

 

OFM waliweza kuweka mtego na kumnasa live profesa huyo akifika na gari lake kisha kuingia ndani.

Kama hiyo haitoshi, OFM pia iliingia mzigoni na kuwanasa wanawake wanne wengine wa profesa huyo na ambao nao ilibainika kuwa licha ya kushiriki penzi na profesa huyo ambaye ameathirika, nao kila mmoja ana mpenzi wake ambaye ni mwanafunzi chuoni hapo.

 

Bahati mbaya sana, wapenzi wao hao nao wana mahusiano na wanawake wengine chuoni hapo hivyo kufanya mtandao wa kuambukizana maradhi hayo kuwa mkubwa sana.

Pia ilibainika kuwa, ushawishi mkubwa wa hatari ni wakati wanafunzi hao wanapokaribia kipindi cha mitihani kwani hulazimika kutoa rushwa ya ngono kwa wanafunzi wenzao pamoja na wahadhiri wao ili waweze kufaulu.

 

“Ni hatari kaka, ikifika kipindi cha mitihani hawana namna, wanajirahisi sana kwa wahadhiri ili wawabebe kwenye mitihani, matokeo yake cheni ya maambukizi ya magonjwa ni kubwa mno,” mmoja wa wanafunzi wa chuo kikuu Huria, aliwaambia OFM.

Lakini pia kuna mwanafunzi mwingine ambaye alikuwa akitembea na mhadhiri mmoja ambaye ana maradhi ya ini.

 

Mhadhiri huyo nusura avunje ndoa na mkewe kutokana na kung’ang’aniwa na msichana huyo mwana chuo.

Hivi sasa mhadhiri huyo anatapa matibabu India na mwanafunzi huyo wa kike haijulikani alipo kwani ameshamaliza masomo.

 

STORI: Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Comments are closed.