The House of Favourite Newspapers

Simba Yaitafuna Azam, Yabeba Ngao ya Jamii

MPAKA mashabiki wa Yanga jana walilazimika kumtaja japo kimoyomoyo. Sharif Eldin Shiboub. Mnyama kwelikweli. Kiungo huyo mshambuliaji wa Simba, raia wa Sudan alikuwa staa wa mchezo wakati timu yake ikiifunga Azam Fc mabao 4-2 katika mechi ya Ngao ya Jamii, Uwanja wa Taifa. Alitumbukiza mabao mawili mwenyewe ndani ya dakika 45 za kwanza na kugeuka mwiba kwa Azam.

 

Alitumia vizuri umbo lake, alionyesha umahiri wake kwenye fiziki,alisukuma mashambulizi ya akili na kutoa pasi za maana. Lakini komesha ni bichwa lake ambalo lilitumbukiza mabao mawili ya kinyama na kumfanya awe gumzo kwa mashabiki waliokuwa uwanjani na hata kwenye vibanda umiza uswahilini. Shiboub ambaye ana weusi wa kuvutia pengine kuliko wakazi wote wa Dar es Salaam,alitawala kwenye mitandao ya kijamii huku mashabiki wakimwambia kwamba ; “Huna deni. Tumekukubali.”

MCHEZO WENYEWE Licha Simba kuanza kulishambulia lango la Azam dakika ya 2 John Bocco alikosa bao la wazi la kichwa kutokana na pasi safi ya Hassan Dilunga kama ilivyokuwa kwa fundi mwenyewe Shiboub alipojikuta ndani ya 18 huku wakipenyezeana pasi fupifupi na Meddie Kagere na shuti lake kupanguliwa na Abalora.

 

Azam waliamka na kwa kufanya shambulizi kali la kushtukiza katika dakika 7 kupitia Shabaan Chilunda aliyekosa bao la wazi akiwa na Beno Kakolanya kutokana na ‘kuchopu’ mpira ambao ulitoka nje.

Azam walifanya tena shambulizi kali katika dakika ya 13 kupitia Chilunda aliyefunga bao la kuongoza kwa shuti kali kufuatia pasi mpenyezo ya Mvuyekure akiwa katikati ya mabeki wa Simba lakini bao hilo lilidumu kwa dakika tatu kabla ya Shiboub kufanya yake kwa kichwa kwa mpira uliokuwa umetemwa na Abalora aliyepangua shuti la Hassan Dilunga.

 

Bao hilo liliwaamsha Simba kwa kuendelea kuliandama lango la Azam ambapo Kagere ‘MK 14 au Terminator’ alikosa bao kwa shuti lake kuokolewa na kipa wa Azam licha ya pasi tamu kutoka kwa Kanda.

Lakini dakika ya 22, Shiboub yuleyule aliifungia Simba bao la pili kwa kichwa tena lakini safari hii akiunganisha mpira wa faulo uliokuwa umepigwa na Tshabalala baada ya Dilunga kuchezewa faulo na Wadada ambaye ni raia wa Uganda.

 

Katika dakika 27, Simba walilazimika kufanya mabadiliko ambapo walimtoa Bocco ambaye aliumia na kuingia Claytous Chama. Azam walizinduka tena katika dakika ya 31 kupitia Domayo kwa kushindwa
kuunganisha pasi fupi kutoka kwa Chilunda aliyekuwa akicheza soka la kulipwa Hispania. Matokeo hayo yalidumu dakika 45 za kwanza kwa Simba kuwa mbele kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili,Simba walifanya mabadiliko tena kwa kumtoa Kanda na nafasi yake kuchukuliwa na Miraji Athuman dakika 77 kabla ya dakika 79 Kagere kukosa bao kwa shuti lake kupaa juu. Azam wakaanzisha shambulizi la haraka ambapo wakapata bao la pili la kideo kupitia kwa Domayo aliyeunganisha krosi ya Chirwa dakika ya 78.

 

Dakika ya 82 Simba wakamtoa Shiboub na kuingia Fraga, wakafanya shambulizi la kushtukiza ambapo walifunga bao la nne kupitia Francis Kahata ambaye alishangilia kwa staili ya aina yake.

Baada ya mchezo huo Kocha wa Simba,Patrick Aussems alisema ; “Hii mechi tulikuwa tunaitumia kama kipimo cha mechi yetu ya kimataifa, tumecheza mpira mkubwa sana na tulitaka kuwaonyesha kwamba Simba haishikiki.

 

 

Ndio timu bora.” Shiboub alisema; “Ilikuwa mechi nzuri sana na nashukuru nimewapa raha wanaSimba, mambo mazuri yanakuja.”

 

Huku Chilunda akisisitiza kwamba haikuwa bahati yao lakini walipiga mpira mzuri. Simba:Kakolanya, Kapombe,Tshabalala, Nyoni,Wawa, Mkude, Kanda/Miraji,Shiboub/ Fraga,Kagere,Bocco na Dilunga/Kahata. Azam: Abalora,Wadada, Kangwa/Masai,Yaku b,Domayo,Mvuyekur e,Sureboy,Chilunda/ Kipwagile,Ella/Chirwa na Mahundi/Abdallah Masoud.

Comments are closed.