The House of Favourite Newspapers

Madhara ya maambukizi katika via vya uzazi (pid) kwa mwanamke

MAAMBUKIZI katika via vya uzazi kwa kawaida hujulikana kama PID, kitaalamu kirefu chake ni Pelvic Inflammatory Disease, kwa Kiswahili maana yake ni maambukizi ya magonjwa katika via vya uzazi.

PID, ni maambuki yanayoathiri viungo vya uzazi vya mwanamke na hutokana na mchanganyiko mbalimbali wa magonjwa ya zinaa, hasa yaliyosababishwa na bakteria wa Pangusa (Chlamydia-ugonjwa huu tutaujadili siku zijazo) au kisonono.

Ugonjwa wa PID unapokaa muda mrefu bila kutibiwa, unaweza kusababisha uharibifu mkubwa usiobadilika katika mfumo wa uzazi wa mwanamke, hasa katika mfuko wa kizazi (uterus), vifuko vya mayai (Ovaries) na mirija ya mayai (fallopian tubes).

Ugonjwa huu unapokaa muda mrefu mwilini bila kutibiwa humfanya mwanamke kupatwa na ugumba. Wanawake wengi wamekuwa wakisumbuka na ugonjwa huu.

Ugonjwa wa kisonono pamoja na pangusa (Chlamydia) ndio vyanzo vikuu vya maambukizi katika via vya uzazi wa mwanamke.

Mwili wa mawanamke unapokuwa na afya kamili, mlango wa kizazi huwa na nguvu ya kuzuia bakteria wasiweze kuingia katika viungo vya ndani vya uzazi kutoka ukeni.

Hata hivyo, wakati mlango wa kizazi unapokuwa wazi na kuruhusu magonjwa ya zinaa kuingia, hasa kisonono na pangusa, mlango wa kizazi hupata maambukizi na kisha hupoteza uwezo wake, hivyo kuruhusu maambukizi na bakteria kuingia na kufika juu kwenye viungo vya uzazi.

Hapa kuna mambo ambayo huwafanya wanawake kupatwa na tatizo hili kwa urahisi, mambo hayo ni: Moja, kuwa na wapenzi wengi ama kutoka nje ya ndoa, pili; kuanza mambo ya mapenzi mapema hasa chini ya miaka 20, tatu; kupiga bomba ukeni kwaweza kusaidia vimelea kuingia ndani na kusababisha maambukizi katika viungo vya uzazi.

DALILI ZA MAAMBUKIZI

PID ikianza kuonyesha dalili zaweza kuwa kama ifuatavyo; maumivu ya tumbo chini ya kitovu, kutokwa na uchafu ukeni, hasa wenye rangi ya njano unaoelekea kuwa kijani kwa mbali ukiwa na harufu mbaya, kuhisi maumivu ama hali ya kuungua wakati wa kukojoa.

Dalili nyingine ni kuwa na homa, kuhisi kichefuchefu ama kutapika, maumivu wakati wa tendo la ndoa ama kutokwa na damu wakati wa tendo la ndoa, kupata hedhi mara mbili ndani ya mwezi mmoja.

Kadri inavyoonyesha kuwa huna dalili zozote za PID, ni vyema kila mara kwenda katika zahanati ama hospitali ili kupata vipimo kuweza kukuhakikishia kuwa uko salama, na hauna maambukizi yoyote ya zinaa.

Wanawake wadogo chini ya umri wa miaka 20, mara nyingi wanapatwa na janga la maambukizi haya kwa urahisi, na inafaa wapate vipimo angalau mara moja kwa mwaka.

Mwanamke unapoona dalili zozote tofauti, usisite kufika hospitalini ili kufanya uchunguzi na kuhakiki tatizo lako. Hakuna kipimo maalumu cha PID, lakini hata hivyo, daktari anaweza kupima maambukizi kwa kuchukua vitu vinavyotoka ukeni, ama mkojo.

Itandelea wiki ijayo.

 

Na Mtaalam Wetu, Mandai

Simu; + 255 716 300 200

Comments are closed.