The House of Favourite Newspapers

MAFURIKO YASABABISHA VIFO VYA WATU TISA DAR – PICHA 15

MVUA kubwa zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita zimesababisha mafuriko aktika maeneo mbalimbali ya jiji huku watu kadhaa wakiripotiwa kufariki dunia kutokana na mvua hizo.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Lazaro Mambosasa amesema amepokea taarifa ya watu tisa kufariki dunia kutokana na mvua hizo huku wengine wakijeruhiwa.

Kamanda Mambosasa amesema vifo hivyo vimetokana na kuangukiwa na ukuta na wengine kusombwa na maji kutokana na mvua zilizonyesha kwa siku tatu mfululizo.

Mambosasa amesema mwili mmoja uliosombwa na mafuriko umekutwa ukielea majini kuelekea eneo la Jangwani.

Aidha, mamia ya wakazi wa jiji hilo wameripotiwa kupoteza makazi yao kutokana na maafa hayo huku wengine wakipoteza mali zao.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amefika katika eneo la Jangwani leo na kushuhudia hali halisi, na kisha kutoa agizo kwa wakuu wa shule kuwa wanafunzi wapumzike nyumbani kwa siku mbili, mpaka hali itakapokuwa nzuri.

 

 

Aidha, Makonda amewaomba wakazi waishio maeneo hayo kuchukua tahadhari na kuondoka maeneo hayo kwa kipindi hiki cha mvua ili kuepusha madhara makubwa zaidi kuwatokea.

Comments are closed.