The House of Favourite Newspapers

Mafuta ya Nguruwe Yaiponza Simba

0

Na Sweetbert Lukonge | CHAMPIONI|GPL
KLABU ya Simba huenda ikajikuta ikiingia matatani kwa mara nyingine tena na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya juzi Jumamosi, mmoja wa wanachama wake kukamatwa akifanya vitendo vinavyoashiria ushirikina katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe FA dhidi ya Azam FC.
Kabla ya mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mwanachama maarufu wa klabu hiyo ambaye amekuwa akifanya vituko mara kwa mara uwanjani, Ngade Ngalambe, aliingia uwanjani huku akiwa amebeba chupa ya bia na kwenda moja kwa moja katika goli la upande wa Kaskazini kisha akaanza kumwaga kimiminika kilichokuwa ndani ya chupa hiyo.
Baada ya kumaliza kufanya zoezi hilo, ndipo alipokamatwa na walinzi wa uwanja huo na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi na baada ya muda aliachiwa na kuendelea na majukumu yake mengine ambayo inadaiwa alikuwa amekabidhiwa na uongozi wa klabu hiyo kuyafanya.
Hata hivyo, baada ya tukio hilo, Championi Jumatatu lilimtafuta Ngade ili kujua ni kitu gani alichokuwa akikimwaga katika goli hilo, alipopatikana na kuulizwa kuhusiana na tukio hilo alikataa kusema chochote.
Lakini mmoja kati ya watu wa karibu na Ngade, aliliambia Championi Jumatatu kuwa: “Yale yalikuwa ni mafuta ya nguruwe ambayo alipewa akayamwage golini ili kuvunja nguvu zote za uchawi kama Azam walikuwa wameturoga.
“Hata hivyo, kwa sasa hawezi kusema chochote kwani viongozi wamezuia asiseme.”
Kwa mujibu wa Kanuni ya 42 ya michuano hiyo inayozungumzia udhibiti wa klabu, kifungu cha 1 na 2,  kitendo hicho alichokifanya Ngade ni kosa na kinaweza kuisababishia Simba kupigwa faini ya Sh 500,000, huku mhusika mkuu akiadhibiwa kwa kufungiwa kuingia uwanjani kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu na kisichozidi miezi 12.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas kuzungumzia adhabu itakayowakumba Simba na Ngade kutokana na tukio hilo, alisema: “Tunaendelea kulifanyia uchunguzi suala hilo na endapo itabainika basi kanuni zipo wazi, hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya Simba na aliyefanya kitendo hicho.”

Leave A Reply