The House of Favourite Newspapers

Maganga Aanika Hali ya Ruge, Magufuli Achangia Mil. 46 za Matibabu

RAIS  John Magufuli ametoa Dola 20,000 (Sh. Mil. 46) kuchangia matibabu ya Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba,  ambaye yupo nje ya nchi kwa ajili ya matibabu kwa miezi kadhaa sasa.

 

Hayo yamesemwa na Meneja wa Vipindi na Maudhui wa Clouds Media, Sebastian Maganga,  wakati akizungumzia hali ya Ruge kwenye kipindi cha Clouds 360 leo, Jumanne, Novemba 20, 2018 na kwamba hali ya Ruge inaendelea vizuri huku akiwataka Watanzania kumuombea katika sala zao.

 

Amesema kuwa kuanzia mwezi Mei hadi Juni mwaka huu, afya ya Ruge ilikuwa mbaya,  jambo ambalo lilipelekea ofisi impumzishe kwa muda ili akaendelee na matibabu.

 

“Ni kweli mengi yamezungumzwa lakini ukweli halisi ni huu…   Katikati mwezi wa tano kulelekea mwezi wa sita hali ya mkurugenzi haikuwa nzuri na akatuomba kupata muda kidogo ili ashughulikie afya yake na tuliona hili litakuwa dogo tu na tukatoa baraka zote.

 

“Lakini ripoti za kitabibu zikasema muda wa kupumzika ni mdogo hivyo akaongezewa muda na katikati ya mwezi wa sita na wa saba alirejea na kasi ya kawaida kwenye kazi na wiki mbili tatu tukawa naye na hapo ndiyo tulikuwa tunakaribia kuanza Tigo Fiesta Morogoro.

 

“Akatuambia anabidi aelekee kwenye taratibu za kimatibabu na nikiri bado changamoto hizo zipo na madaktari wanakiri kiongozi wetu ni mpambanaji na bado anahitaji muda wa kupumzika na ni kweli hizo changanoto zilikuwepo,“ amesema Sebastian Maganga aliyengeza kwamba taarifa za kuugua kwa Ruge zilimfikia Rais Magufuli, jambo ambalo lilimuumiza na kumfanya achangie mfuko wa afya.

 

“Tunamshukuru Rais Magufuli kutokana na yeye mara baada ya kupata taarifa hizi alinyoosha mkono kwetu na kutuambia changamoto za kiafya ni kubwa na la awali ambalo anataka kulifanya ni kuchangia mfuko wa kiafya na changamoto zisiwe gharama za kimatibabu na kutoa Dola elfu 20,000,” amesema Maganga na akimshukuru Rais Magufuli kwa upendo aliouonyesha kuchangia matibabu hayo.

Taarifa hiyo, imekuja baada ya sintofahamu iliyokuwepo kwa takribani wiki mbili kuhusu afya ya Ruge Mutahaba.

BREAKING: Baraza la Maulid ya Kitaifa, Tanga

Comments are closed.