The House of Favourite Newspapers

Maghembe, Lwenge Wang’oka Baraza la Mawaziri

0
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

RAIS John Magufuli amefanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri kwa kuwahamisha baadhi yao kwenda wizara nyingine, kuwapandisha baadhi ya manaibu waziri kuwa mawaziri kamili, kuwaingiza wapya na kuwaacha baadhi yao nje ya Baraza hilo.

 

Mabadiliko hayo aliyoyafanya jana Ikulu jijini Dar es Salaam, pia yameongeza wizara kutoka 19 za awali kwa kuzigawanya baadhi ya wizara hizo na kufanya jumla ya wizara zote kuwa 21.

 

Mabadiliko hayo pia yameongeza idadi ya mawaziri kutoka 19 hadi 21 na manaibu waziri kutoka 16 hadi 21. Wizara ambazo zimegawanywa ni ile iliyokuwa ya Nishati na Madini ambayo kwa mabadiliko aliyoyafanya Rais Magufuli jana sasa kutakuwa na Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini.

 

Wizara nyingine iliyogawanywa ni iliyokuwa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo sasa kutakuwa na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, aliyekuwa Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki amehamishiwa kwenye Wizara mpya ya Madini akisaidiwa na Naibu Waziri Stanslaus Nyongo, wakati Wizara ya Nishati amepewa Dk Medard Kalemani akisaidiwa na Naibu Waziri Subira Mgalu.

 

Waziri Kairuki anaingia katika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kukabidhiwa wizara hiyo ambayo imekuwa ikitajwa kuwa yenye changamoto nyingi kuliko wizara nyingine yoyote huku mawaziri wengi waliopita katika wizara hiyo wakipatwa na misukosuko.

 

Wizara nyingine mpya ni ile ya Kilimo ambayo itakuwa chini ya Dk Charles Tizeba na Naibu Waziri wake ni Dk Mary Mwanjelwa, wakati Wizara Mifugo na Uvuvi iko chini ya Luhaga Mpina akisaidiwa na Naibu Waziri Abdallah Ulega.

 

Ukiondoa ongezeko la wizara, kupanda kwa Naibu Mawaziri kuwa mawaziri kamili na kuteuliwa kwa sura mpya katika nafasi ya Naibu Mawaziri, Rais pia aliwaacha mawaziri wawili na Naibu Waziri mmoja.

Mawaziri waliokumbwa na balaa hilo ni Gerson Lwenge aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji na Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe na Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura.

 

Mlolongo wa Mawaziri kung’oka Rais Magufuli alianza kulifanyia marekebisho Baraza lake la Mawaziri tangu mwezi Mei mwaka jana, alipotengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kutokana na Waziri huyo kuingia bungeni na kujibu maswali akiwa amelewa na nafasi yake kuchukuliwa na Waziri Mwigulu Nchemba.

 

Baadaye alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na nafasi hiyo kumteua Dk Harrison Mwakyembe. Naye aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliondolewa kwenye nafasi hiyo kutokana na sakata la biashara ya madini kuonesha nchi kuibiwa kiwango kikubwa cha madini.

 

Jinamizi hilo liliendelea kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani ambao waliondolewa baada ya matokeo ya uchunguzi wa kamati mbili za Rais na moja ya Bunge zilizoundwa kuchunguza biashara ya madini nchini kubainisha mawaziri hao kuhusika kwa nchi kuibiwa mapato halisi.

 

Wachache watoa maoni yao Akizungumzia uteuzi wake, Ndugulile aliahidi kutumia uwezo wake wote katika kuihudumia Sekta ya Afya. Ndugulile ambaye kitaaluma ni mtaalamu wa afya alisema atahakikisha anachangia kikamilifu katika kuimarisha ubora wa huduma na utendaji katika sekta hiyo.

 

Alisema; “Namshukuru Rais kwa uteuzi huu na kuwa sijafurahi kwa sababu ya kupata cheo ila ni kuwa na wakati mzuri zaidi katika utekelezaji wa majukumu ambayo kimsingi yataongeza chachu katika maendeleo ya sekta hii ya afya.” Kwa upande wake Mpina alisema kuwa atahakikisha anaitumikia wizara hiyo kwa nguvu na akili zake zote.

 

Alisema, atahakikisha kuwa anajipanga zaidi katika kukabiliana na kero kadhaa ambazo zimedumu kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Alisema moja ya changamoto yake itakuwa ni kukabiliana na suala la uvuvi haramu na kumaliza migogoro inayosababishwa na wafugaji.

 

Kwa upande wake Nyongo, alisema anamshukuru Rais kwa kumuamini na kumpa jukumu hilo kubwa. ‘Nimshukuru Rais kwa kunipa jukumu hili kubwa lililobeba maslahi ya umma, ninamuahidi nitafanya kazi uzalendo na ubunifu kwa kuzingatia sheria na kanuni, ni wizara nyeti iliyobeba maslahi ya taifa,” alisema Nyongo.

 

Naye Hasunga alisema ameupokea uteuzi huo kwa mikono miwili na anamshukuru Rais kwa kuona anaweza kulitumikia taifa katika wizara hiyo. “Ninamshukuru Rais kwa kuona ninaweza kuwatumikia wananchi katika wizara hii, ninaahidi nitajitahidi kufanya kazi kwa weledi kwa kuwa pia nafasi niliyopewa inaendana na taaluma yangu,” alisema Hasunga.

Wasomi waunga mkono

Baadhi ya wasomi waliozungumza na gazeti hili jana walisema kuwa mabadiliko ambayo Rais Magufuli ameyafanya yalikuwa ni ya lazima na muhimu. Sababu zilizotajwa na wasomi hao ni mtikisiko ulitokea kwenye sekta ya madini lakini pia ni kipindi ambacho Rais amekitumia kama cha mapumziko baada ya kutafakari utendaji wa timu aliyokuwa nayo kwa miaka miwili sasa tangu aingie madarakani.

 

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bashiru Ally alisema kuwa mabadiliko aliyoyafanya Rais ni ya kawaida kwa kuwa miaka miwili inamtosha kujua mwelekeo wa utendaji wa serikali yake katika kutekeleza Ilani ya Chama chake cha Mapinduzi (CCM) na matarajio binafsi aliyokuwa nayo kama Rais.

 

“Kuna Wizara ambazo ziliathirika kutokana na kujiuzulu kwa mawaziri baada ya kuundwa kwa kamati zilizochunguza biashara ya madini, hivyo kwa wizara nyeti kama ya Tamisemi, Nishati na Madini ilikuwa lazima zipate mawaziri, lakini pia kuzitenganisha Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo ni muhimu kwa sababu italeta ufanisi katika kuzisimamia,” alieleza Dk Bashiru.

 

Kwa kuwa lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuifanya Tanzania iwe ya viwanda, Dk Bashiru alisema kuwa lengo hilo si rahisi kulifikia kama hakuna msingi mzuri katika kilimo. Alisema kuzitenganisha Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni muhimu kwa maendeleo ya viwanda kwa kuwa kwenye kilimo kuna mazao muhimu kama vile korosho, pamba, kahawa, lakini pia mambo ya pembejeo, mbolea na ugani ambayo yote yanahitaji usimamizi wa karibu.

 

Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana alisema kuwa mabadiliko aliyoyafanya Rais yataleta udhibiti, ufuatiliaji na usimamizi bora hasa kwa Wizara za Madini, Nishati, Kilimo, Uvuvi na Ufugaji ambazo zimegawanywa na kuwa wizara zinazojitegemea.

 

Profesa Bana alisema kwa kuwa kwenye madini kulikuwa na matatizo mengi, anaamini Waziri Kairuki ataisimamia vyema Wizara hiyo kutokana na uzoefu aliokuwa nao wa kuwa kwenye Baraza la Mawaziri tangu serikali ya awamu ya nne.

 

Alisema Kairuki alifanya kazi nzuri katika kusimami zoezi la kuwaondoa watumishi waliokuwa na vyeti feki na watumishi hewa, hivyo kwa kutumia taaluma ya sheria aliyonayo na uzoefu wake anaamini hata kwenye Wizara ya Madini atasimamia vizuri.

 

“Pia Rais amefanya vizuri kuwapandisha Manaibu Mawaziri ambao wengi wao ni vijana. Ujue jambo hili litawapa moyo na nguvu, lakini pia vijana wana nguvu ya kufanya kazi, ni wepesi wa kutembea huku na huko katika kusimami wizara zao,” alieleza Profesa Bana.

 

Aidha Profesa Bana alisema kuwa Rais asiishie tu kufanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri, lakini pia aangalie watendaji wengine wa serikali ambao wanaonekana kupwaya kwenye nafasi zao kama vile Makatibu Wakuu na Wakurugenzi.

 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, wateule wote wataapishwa kesho saa 3:30 asubuhi, Ikulu jijini Dar es Salaam. Wakati huo huo; Rais John Magufuli amemteua Stephen Kagaigai kuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumzia uteuzi wa Kagaigai Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema anachukua nafasi ya Dk Thomas Kashilila ambaye alisema atapangiwa majukumu mengine. Kabla ya uteuzi huo Kagaigai alikuwa Kaimu Karani wa Baraza la Mawaziri.

Leave A Reply