The House of Favourite Newspapers

Mahakama Yaamuru Wadeni Watatu wa Exim Kukamatwa

0

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania (Idara ya Biashara) jijini Dar es Salaam imeagiza kukamatwa kwa wadeni watatu wa benki ya Exim Tanzania kwa kushindwa kutekeleza hukumu ya kulipa deni lenye thamani ya Tsh 674.4m/ – na zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 2.

 

Kwa mujibu wa hati ya kukamatwa kwa wadeni hao iliyotolewa na mahakama hiyo katika kesi ya kibiashara nambari 95 ya mwaka 2015, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Justine Masejo ameagizwa kuwakamata wadeni hao watatu ambao ni Chimanbhai Marghabai Patel, Pratik Chimanbhai Patel na Sonia Pratik Patel.

 

Kwa mujibu wa hati hiyo iliyosainiwa mnamo Septemba 13, 2021 na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, inasema watatu hao walihukumiwa katika kesi hiyo tarehe 16 Septemba, 2016, kuilipa Benki ya Exim Tanzania Limited kiasi cha fedha Tsh 674,440,547.55 na Dola za Kimarekani 2,024,094.14 pamoja na riba na gharama ya kesi hiyo.

 

Hata hivyo licha ya hukumu hiyo kutolewa, pesa hizo bado hazijalipwa kwa benki hiyo. Aidha, ni kufuatia ucheleweshaji huo, ndipo mahakama hiyo iliamuru kukamatwa kwa watatu hao isipokuwa tu iwapo wangelipa deni hilo na kuongeza kuwa watatu hao wangepaswa kufikishwa mahakamani haraka iwezekenavyo.

 

“Unaagizwa kurudisha hati hii mnamo tarehe 27 Oktoba, 2021, sambamba na uthibitisho unaoonesha siku na namna ambavyo hati hii imetekelezwa au sababu zilizosababisha kushindwa kutekelezwa kwake,” ilisomeka sehemu ya hati hiyo.

NA MWANDISHI WETU

Leave A Reply