The House of Favourite Newspapers

Majaliwa Awasimamisha Kazi Watumishi Wanane Ulanga

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa, amewasimamisha kazi watumishi wanane  wa halmashauri ya wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro na kuagiza wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya sh. bilioni tatu za mapato ya ndani.
Amesema watumishi wa umma wana wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu.
“Nawasihi nyote muache kufanya kazi kwa mazoea, mbadilike na kuenenda sawa na matakwa na maelekezo ya serikali ya awamu ya tano na anayejiona hatoshi ajiondoe,” alisema.
Aliwasimamisha kazi watumishi hao jana (Jumatatu, Septemba 16, 2019) wakati akizungumza na watumishi na madiwani  wa halmashauri hiyo kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo uliopo mjini Mahenge.
Watumishi hao kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Yusuph Semguruka, ambaye kwa sasa amehamishiwa TAMISEMI, Rajabu Siriwa (mweka hazina), Stanley Nyange, Johnson Mwenyembole, Isack Mwansokope, Said Majaliwa, Charles Steven na Hezron Lopa.
Pia alitumia kikao hicho kumrejesha kazini na kumpandisha kuwa mkuu wa Idara ya Ukaguzi wa Ndani, Augustine Mwaria, ambaye awali alikuwa akikaimu nafasi na kuibua ubadhirifu huo ambapo matokeo yake alisimamishwa kazi.
Akisisitiza suala hilo aliwataka watumishi hao wazingatie sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi  na kujiepusha na vitendo vya wizi kwa sababu wanaoathirika baada ya wao kuchukuliwa hatua za kisheria ni wenza wao na watoto.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya,  alisema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto ya ubadhirifu wa fedha za umma,  hali inayosababisha kuwepo kwa mpasuko kati ya watumishi na baraza na madiwani.
Alisema watumishi wanaotekeleza majukumu yao ipasavyo wanaandamwa.
IMETOLEWA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

Comments are closed.