The House of Favourite Newspapers

Makala Exclusive… Anjela Kampa Penzi Harmonize?

0

Ukipewa nafasi ya kutaja listi ya warembo wanaokimbiza kwa sasa kwenye gemu la muziki wa Bongo Fleva, huwezi kuacha kutaja jina la mwanadada Angelina George almaarufu Anjela.

Licha ya kuwa kwenye gemu kwa kipindi kifupi, lakini tayari amefanya maajabu ya kutosha huko mjini YouTube na hata kitaani.

 

Miongoni mwa ngoma kali alizofanya na zikampa jina kubwa akiwa zao la Konde Gang ni pamoja na Kama aliyoshirikiana na bosi wake, Harmonize na No Body iliyotoka miezi mitatu iliyopita, lakini mpaka sasa bado ipo namba kumi kwenye ngoma zinazotrendi YouTube.

Gazeti IJUMAA limeketi kitako na Anjella katika mahojiano maalum (exclusive interview) ambapo amefunguka mambo mengi usiyoyajua kutoka kwake, ikiwemo ile skendo matata inayomuandama ya kudaiwa kutoka kimapenzi na bosi wake huyo, Harmonize pamoja na jinsi anavyojisikia pale anaposhindanishwa kila mara na msanii mwenzake, Zuchu kutoka Lebo ya WCB.

 

IJUMAA: Hivi karibuni kulikuwa na maneno mengi kuwa umenunua viewers (watazamaji) kwenye YouTube na hii ni baada ya wimbo wako wa No Body kufikisha views wengi ndani ya muda mfupi, hili unaliongeleaje?

 

ANJELLA: Huwezi kuwakataza watu kuongea, walianza kuongea hivyo baada ya wimbo wangu wa No Body kufikisha watazamaji milioni moja kwenye YouTube ndani ya siku moja, lakini mbali na yote namuachia Mungu kwa sababu kazi nzuri siku zote hujiuza zenyewe.

 

IJUMAA: Ni kweli kwamba bila kiki muziki haukui?

 

ANJELLA: Siyo kweli, kama nilivyosema mwanzo kuwa kazi nzuri siku zote hujiuza zenyewe, sasa kama umefanya kazi nzuri inayoeleweka, kuna sababu gani ya kufanya kiki tena? Kwa hiyo binafsi naamini muziki mzuri unaweza kujiuza wenyewe bila kiki.

IJUMAA: Wewe ni msanii ambaye umepitia changamoto nyingi tangu ulipoanza tu kujulikana kwa watu, kipindi unatoka uliimba wimbo wa msanii mwenzako, Zuchu, lakini baadaye ukaandamwa sana mitandaoni kuwa umeimba vibaya, hii ilikuathiri kiasi gani?

 

ANJELLA: Haikuniathiri chochote, ila kitu ambacho nilijifunza ni kusikiliza maoni ya watu mbalimbali pia, kwa hiyo nilipoambiwa nimeimba wimbo wake vibaya, nikaona kuna kitu cha kufanyia kazi ili siku nyingine lisije kutokea jambo lingine kama hilo.

 

IJUMAA: Baada ya yale maneno, umewahi kukutana mahali popote na Zuchu?

 

ANJELLA: Hapana, sijawahi kukutana naye mahali popote.

 

IJUMAA: Ulipoambiwa maneno ya kashfa kuhusu ngoma yake, ilikukatisha tamaa ya kuendelea kumfuatilia?

 

ANJELLA: Hapana, Zuchu ni miongoni mwa wasanii ninaopenda sana kazi zao.

IJUMAA: Umewahi kutamani kufanya naye kolabo siku moja?

 

ANJELLA: Ndiyo, natamani sana, siku menejimenti yake na yangu zikikaa na kuelewana, basi naamini hakutakuwa na shida yoyote ile.

 

IJUMAA: Huwa unajisikiaje unaposhindanishwa naye?

 

ANJELLA: Mwanzoni ilikuwa inanikata sana, lakini siku hizi naona ni jambo la kawaida tu.

 

IJUMAA: Harmonize alisema kuwa yupo mbioni kukupeleka nchini India kwa ajili ya matibabu ya miguu, unaweza kutuambia taratibu za matibabu zimefikia wapi?

 

ANJELLA: Taratibu za matibabu yangu zinaendelea vizuri na mpango wa kwenda nchini India bado upo palepale ila kwa sasa nimeshaanza matibabu Muhimbili kisha baada ya hapo ndipo madaktari wataona kama kuna umuhimu wa mimi sasa kwenda India au la.

 

IJUMAA: Kipindi Harmonize na Kajala wakiwa kwenye uhusiano wa kimapenzi tuliona jinsi Kajala alivyokuwa anakusapoti kwenye muziki wako, vipi uhusiano wenu bado unaendelea kwa sasa?

 

ANJELLA: Mimi na Kajala hatujawahi kuwa karibu kabisa, ila alikuwa ananisapoti kipindi kile kwa sababu alikuwa ni sehemu ya familia ya Konde Gang, lakini kwa sasa hayupo tena, hivyo siwezi kusema kuwa nipo naye karibu.

 

IJUMAA: Vipi, lakini ukiachia ngoma mpya huwa unamcheki ili akusapoti?

ANJELLA: Hapana, sijawahi kumtumia.

 

IJUMAA: Kuna maneno yanaendelea kuwa hujui kupangilia vizuri mavazi yako na watu wanakwenda mbali zaidi kwa kukushauri kuwa ni bora utafute mbunifu wa mavazi (designer) ambaye atakuwa anakuvalisha vizuri ili uwe na muonekanao wa kisanii, wewe unayachukuliaje maoni yao?

 

ANJELLA: Kama nilivyosema mwanzo, mimi huwa napenda kufanyia kazi kila ushauri ninaoambiwa kwa sababu wao ndiyo wananiona. Pia naamini anayekuambia ukweli anakupenda kwa hiyo nipo nalifanyia kazi hilo.

 

IJUMAA: Kwani nani ambaye anakuvalisha kwa sasa?

ANJELLA: Yupo designer wangu naamini hata yeye ameliona hilo mitandaoni, hivyo atalifanyia kazi.

 

IJUMAA: Ni kweli kwamba umewahi kutoka kimapenzi na bosi wako, Harmonize?

 

Anjella: (anashtuka) Mimi? Ndiyo kwanza nasikia kwako jamani.

 

IJUMAA: Ndiyo inavyosemekana, wananzengo wanadai Harmonize hana huruma akaamua kupita na wewe pia…

 

IJUMAA: Hapana, siyo kweli kabisa, namheshimu sana Harmonize na hajawahi hata siku moja kunivunjia heshima.

 

IJUMAA: Unamzungumziaje Harmonize?

Anjella: Ni mtu ambaye ana upendo sana, anamjali na kumthamini kila mtu, nina mengi sana ya kumzungumiza ila najua siwezi kumaliza yote hapa, aliponitoa ni mbali mpaka hapa aliponifikisha, nasema kwangu ni ndoto iliyotimia, naomba Mungu aendelee kumpa maisha marefu.

Cc: @sifaelpaul

Leave A Reply