The House of Favourite Newspapers

MAKAMBO, AJIBU WAFICHWA KISA MECHI YA SIMBA FEB 16

Heritier Makambo

WACHEZAJI wote wa Yanga wakiwemo Ibrahim Ajibu na Heritier Makambo hawataonekana mitaani wala kwenye makazi yao mpaka mechi na Simba itakayopigwa Februari 16, mwaka huu ipite.

 

Kocha Mwinyi Zahera amesisitiza kuwa hatavunja kambi ya pamoja ya wachezaji wake hadi atakapomaliza michezo yake mitano ya Ligi Kuu Bara ambayo anaamini ndiyo itampa ubingwa.

 

Mechi hizo tano ambazo Yanga watazicheza za mfululizo ni dhidi ya Coastal Union(Tanga) watakaocheza Februari 3, Februari 6 na Singida United (Singida), Februari 10 na JKT Tanzania (Tanga), Februari 16 na Simba (Dar) kabla ya kumalizia na Mbao FC Februari 20 huko Mwanza.

Yanga, iliingia kambini juzi Jumatatu asubuhi kwenye Hoteli ya Nefaland, Manzese jijini Dar es Salaam baada ya mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini wakati wakijiandaa na mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Biashara United utakaopigwa leo Taifa.

 

Akizugumza na Spoti Xtra linalotoka kila Alhamisi na Jumapili, Zahera alisema; “Timu imeingia kambini Jumanne asubuhi kwa ajili ya mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Biashara United hii ni tofauti na siku nyingine ambazo tumekuwa tukiingia kambini tulikuwa tukiingia siku moja kabla ya mechi.

 

“Hayo ni mabadiliko ya haraka niliyoyafanya katika kuhakikisha nafanikisha malengo yangu ya kutwaa ubingwa wa ligi na Kombe la FA, huo ni mwanzo nimepanga baada ya mchezo huo sitavunja kambi hadi tutakapomaliza michezo yetu hii mitano ya ligi iliyokuwepo mbele yetu ukiwemo wa Simba.

 

“Sitaivunja kambi kutokana na mfululizo wa michezo yetu inayoongozana timu ikicheza mechi na kupumzika siku moja kabla ya kucheza mchezo mwingine, hivyo ni lazima wachezaji wangu wakae pamoja kambini ili wapate muda mzuri kula na kupumzika ili nifanikishe malengo yangu ya ubingwa,” alisema Zahera huku akisisitiza kuwa mechi ya Simba ni muhimu na ataicheza kiumakini kwavile ana wachezaji wengi wa kuamua matokeo.

STORI NA WILBERT MOLANDI

Comments are closed.