The House of Favourite Newspapers

Makonda Amtembelea Askofu Dkt Malasusa, Amhakikishia Viongozi Wa Kiroho Kumwombea Rais Samia

0

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) Taifa, Ndugu Paul Christian Makonda amemtembelea Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Mkuu Dkt. Alex Gehaz Malasusa, kwa lengo la kumsalimia na kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake kuliongoza kanisa hilo, kwa mara nyingine.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika leo Jumamosi, Disemba 2, 2023, Askofu Mkuu Dkt. Malasusa ambaye pia ni Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), amesema viongozi wa dini na kiroho wataendelea kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuwa na busara, where hekima anapoendelea kuliongoza taifa, kama ambavyo tayari ameonesha uimara, tangu alipobeba dhamana na Mamlaka ya Kiongozi Mkuu wa Nchi.

Mbali ya kumpongeza Ndugu Makonda kwa kuteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya NEC, Uenezi, Itikadi na Mafunzo na kumtakia heri anapotimiza wajibu huo, Baba Askofu Dkt. Malasusa ameongeza nasaha zake kwa kutoa wito kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kusimamia misingi yake, ikiwemo kuhakikisha Watanzania wote wanatendewa haki, kuwa sikio lao la wananchi wanyonge na kuwasemea changamoto zao mbalimbali kila inapojitokeza, ili zifanyiwe kazi na kubadili hali zao.

Kwa upande wake Ndugu Makonda, pamoja na kumshukuru Baba Askofu Dkt. Malasusa kwa ushirikiano wake na utayari wake na viongozi wenzake wa KKKT, muda wote kuendelea kuliombea taifa na Watanzania wote kuendelea kudumisha upendo, amani, utulivu na mshikamano bila kujali tofauti za kiitikadi, pia alitumia fursa hiyo kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake kuwa Mkuu wa KKKT, hivyo amemtakia kila la heri katika majukumu yake na kumuahidi ushirikiano wake na Chama Cha Mapinduzi, ambacho amepewa wajibu wa kuwa msemaji wake.

Ziara hiyo ya Ndugu Makonda ofisini kwa Askofu Dkt. Malasusa ni mwendelezo wa ziara zake za kuwatembelea viongozi mbalimbali wa dini na kiroho, kwa ajili ya kwenda kuwasalimia, kujitambulisha na kuwaomba ushirikiano wa kikazi.

Leave A Reply