The House of Favourite Newspapers

MAKONDA: TUNDU LISSU AFIKISHIWE MIREMBE – VIDEO

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,  amesema Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu,  bado hajapona vizuri licha ya kuanza ziara zake Barani Ulaya huku akimtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai,  kumfikisha katika Hospitali ya Mirembe iliyopo Dodoma pindi tu atakaporejea nchini kwa ajili ya matibabu zaidi.

 

Makonda amesema hayo leo wakati akizungumza kwenye mkutano maalum na wadau wa madini ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais John Magufuli katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

 

Pamoja na kusifia utendaji kazi mzuri wa Rais Magufuli katika nyanja mbalimbali, Makonda aligusia na kuponda kauli alizotoa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, wiki iliyopita akihojiwa na shirika la habari la Uingereza BBC.

 

Makonda alisema kuna Watanzania ambao hawana utaifa na kwamba hawaoni mema yanayofanywa katika nchi yao hususan juhudi anazochukua Rais Magufuli.

 

“Nilimuona yule mtangazaji (wa BBC) kama Mtanzania anayeitetea Tanzania huku Lissu akibwabwaja hata alipoulizwa hata kuhusu mazuri ya Rais Magufuli… Hivyo nikajua kichwani bado hayupo vizuri, nimuombe Spika Job Ndugai, akirudi Lissu ampeleke (Hospitali ya Wagonjwa wa Akili) Mirembe,” alisema Makonda.

 

Mkuu huyo wa mkoa alisifia juhudi zinazofanywa na serikali hivi sasa katika kufumbua matatizo ya umeme na mafuta kwa ajili ya matumzi ya kawaida na katika maendeleo ya viwanda, ambapo aliutaja mradi wa Stiegler’s Gorge katika Mto Rufiji kuwa ndiyo unaotegemewa kulimaliza tatizo la umeme.

 

Katika mkutano huo, washiriki mbalimbali  katika sekta ya madini, wakiwemo wachimbaji wakubwa na wadogo na wadau mbalimbali, walitoa maombi,  na kueleza matatizo na  dukuduku zao kuhusiana na shughuli hiyo mbele ya Rais Magufuli ambaye aliwataka  kumweleza waziwazi matatizo yao badala ya wao kusubiri kauli kutoka kwake.

 

Hadi tunakwenda mitamboni mkutano ulikuwa unaendelea kwa hamasa kubwa ambapo Rais Magufuli alikuwa anazijibu hoja mbalimbali za wadau na nyingine kuahidi kuzitafutia ufumbuzi mara moja.

 

FUATILIA MJADALA HUO HAPA

Comments are closed.