The House of Favourite Newspapers

MALARIA YAPUNGUA KWA ASILIMIA 7. 3 NCHINI

MAAMBUKIZI  ya  viashiria vya ugonjwa wa  Malaria  Nchini Tanzania yamepungua  kwa Watoto chini ya miaka mitano  kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015 na kufikia asilimia 7.3   kwa Mwaka 2017 hii ni kuzigatia harakati zinazofanywa na  Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Mashirika ya Marekani (USAID) pamoja na shirika la WHO kuhakikisha wanautokomeza ugonjwa huo.

Akizindua  takwimu zilizo tolewa na Ofisi ya Takwimu ya Tanzania   leo Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema siku ya leo kupitia maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa Mkoani Kigoma, atazindua rasmi Matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya Malaria kwa Mwaka 2017.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu,  Albina Chuwa, alithibitisha         matokeo ya sasa ya utafiti huu, yanaonesha kuwa kiwango cha malaria kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano Nchini Tanzania kimeshuka kwa zaidi ya nusu kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3. Hii ni kwa kutumia kipimo cha haraka cha utambuzi wa vimelea (mRDT).

Waziri Ummy alisema utafiti huo unaonesha mikoa yenye kiwango kikubwa cha watoto wenye malaria ni, Kigoma (asilimia 24.4), Geita (asilimia 17.3), Kagera (asilimia 15.4) na Tabora (asilimia 14.8) ambapo mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Njombe, Songwe na Dodoma ina kiwango kidogo cha maambukizi chini ya asilimia moja.

“Takwimu hizi, zinaonesha kupungua kwa kiwango cha malaria kwa kiasi kikubwa, na hii ni habari njema kwetu sote na inaonesha ni jinsi gani Serikali yenu ipo tayari kutoa kipaumbele katika kuhakikisha kuwa malaria inadhibitiwa na hatimaye tuweze kuitokomeza kabisa ili kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa, tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja katika kufikia malengo tuliyojiwekea ili jamii, hasa watoto chini ya umri wa miaka mitano na wanawake wajawazito ambao ndio waathirika wakubwa wa ugonjwa wa malaria waweze kuepukana na ugonjwa huu,” alisema Waziri Mwalimu.

 

Alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana, lakini bado kuna changamoto, ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi ili kwapamoja tuweze kufikia malengo ya kutokomeza malaria nchini.

 

 Changamoto hizo ni pamoja na wanajamii kutotumia vyandarua ipasavyo katika kujikinga na ugonjwa wa malaria, kuwepo kwa mitazamo potofu juu ya afua za kupambana na malaria; mfano dhana ya kuwa viuatilifu-ukoko za kunyunyizia ukutani zinaleta kunguni na viroboto na kuwa vyandarua vinapunguza nguvu za kiume ni dhana potofu ambazo hazina ukweli wowote. Vilevile, Jamii kutoshiriki kikamilifu katika kutunza mazingira na kuharibu mazalia ya Mbu.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwakilishi wa Shirika la Misaada na Maendeleo la Marekani (USAID), Andy Karas, alisema kwa zaidi ya miaka 12 USAID imekuwa ikifanya kazi pamoja na serikali kupitia Wizara ya Afya kwa ajili ya kupambana na Malaria.

 

Alisema watoto wengi walio hai leo ni kwa juhudi za serikali, kwa kushirikiana na Mfuko wa Rais wa Marekani wa  kupambana na Malaria   kwa muda wote wameweza kusambaza vyandarua zaidi ya milioni 10 na kununua viuwadudu zaidi ya milioni 20 na kupuliza dawa ya mbu kwenye maeneo hatarishi  vile vile wameweza kushirikiana na  ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kufanya takwimu mbalimbali juu ya kupungua kwa ugonjwa wa Malaria.

 

Nae  Balozi wa  Uswizi, Florence Tinguell, aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kwa juhudi kubwa walizozifanya katika kuhakikisha wanatokomeza Malaria. Kwa zaidi ya miaka 50 Ubalozi wa Uswizi umekuwa ukifadhili tafiti za malaria ambazo zimekuwa zikifanywa na taasisi ya Ifakara Health Institute.

 

Hata hivyo mjumbe wa  kamati ya Bunge ya kupambana na Malaria ( TAPAMA) na Mbunge wa Viti  maalumu Mkoa wa Iringa,  Rose Tweve, alisema  wao kama wabunge wanatoa wito kwa wananchi wote kuwa jukumu la kupambana na Malaria na mapambano dhidi ya Malaria ni la wananchi  na wasiiachie serikali peke yake na kuomba nguvu kubwa ielekezwe kwenye kinga na wahudumu wa Afya  na wakina mama  kufika hospitali kwa wakati ili kuweza kupatiwa kinga ya Malaria.

Comments are closed.