Mali za Mugabe Kaa la Moto!

SIKU chache baada ya mazishi ya kihistoria ya rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe kufanyika; mali zake zimegeuka kaa la moto kwa warithi wake.

 

Vyombo vya habari vya magharibi na baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali hasa za Jumuiya ya Ulaya wametaka ufanyike uchunguzi wa mali zote alizoacha Mugabe kwa madai kuwa alizipata kwa njia ya kifisadi.

 

Shirika la Habari la AP (Associated Press) la nchini Uingereza limemtaja waziwazi mjane wa Mugabe, Grace Mugabe kuwa mtuhumiwa wa kwanza wa kile kinachodaiwa kuwa ni ufisadi wa mumewe. Grace ametajwa kuishi na kutumia fedha za umma atakavyo wakati mumewe alipokuwa madarakani na kwamba baada ya kifo cha Mugabe, muda wa yeye kukumbana na mkono wa dola umefika.

Grace ametajwa na baadhi ya vyombo vya magharibi kuwa mara kadhaa ametumia ndege ya rais kwenda nchi za Ulaya kufanya manunuzi ya bidhaa mbalimbali kwa ajili ya matumizi yake. Jarida maarufu la Forbes la nchini Marekani limewahi kumtuhumu Grace kutumia Pauni 60,000 (sawa na shilingi milioni 172) kwenye duka moja kununulia mavazi, mapambo na mahitaji yake mengine.

 

“Grace anasafiri duniani kote kununua nguo za gharama kutoka kwa wabunifu wa kimataifa, sisi huku tunakosa mahitaji ya kibinadamu na watoto wetu wanashindwa kwenda shule,” alisema Hazel Tokwe, mama wa watoto watatu, raia wa Zimbabwe alipohojiwa na Forbes mwaka 2017.

Kifo cha Mugabe ambaye inaaminika kuwa ufisadi wake haukuangaziwa na rais wa sasa wa nchi hiyo Emmerson Mnangagwa kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kulinda heshima ya Mugabe, kimeongeza msukumo kwa baadhi ya raia wa Zimbabwe ambao wamekuwa na kiu ya kuona mali zake zinachunguzwa na ikiwezekana zitaifishwe.

 

Tendai Biti, waziri wa zamani wa fedha wa nchi hiyo na kiongozi wa chama cha upinzani cha People’s Democratic Party (PDP) anasema: “Muda umefika wa mali za Mugabe kuchunguzwa. “Familia hii ina zaidi zaidi ya dola milioni 100 (sawa na shilingi milioni 229), hili sina shaka nalo hata kidogo lakini familia ya Mugabe ina akaunti katika nchi mbalimbali.

“Kwa mfano Afrika Kusini, China, Asia na Hong Kong; Mugabe ana mashamba makubwa 15 na mkewe amejitwalia karibu eneo lote la Mazowe (Mashonaland).”

 

Ingawa nia ya kuzifanyia uchunguzi mali za Mugabe imekua gumzo miongoni mwa Wazimbabwe walio wengi lakini serikali ya nchi hiyo imejizuia kusema chochote hadi hivi sasa ingawa ni wazi kuwa kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakimtazama Grace kama mtu ambaye alitumia madaraka yake vibaya na alimpotosha mumewe kwenye baadhi ya mambo.

Inaelezwa kuwa hata mapinduzi yaliyofanywa na jeshi la nchi hiyo kumuondoa madarakani Mugabe mwaka 2017, yalilenga kuzima harakati za Grace ambaye alikuwa anatajwa kutaka kukiteka chama tawala ZANU-PF ili awe rais baada ya mumewe, jambo ambalo vyombo vya usalama havikukubaliana nalo.

Pamoja na nchi ya Zimbabwe kukabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi, familia ya Mugabe imetajwa kuishi maisha ya anasa kupindukia kwa kile kinachodaiwa na wengi kuwa ni kujilimbikizia mali za umma

Stori: Richard Manyota na mitandao, Uwazi


Loading...

Toa comment