MAMA AMWAGIWA PETROLI, ACHOMWA MOTO HADI KUFA

MaMa mmoja ajulikanaye kwa majina ya Lucia Keraka mwenye umri wa miaka 34, mkazi wa Kijiji cha Kerende wilayani Tarime, Mkoa wa Mara amefariki dunia baada ya kumwagiwa petroli kisha kulipuliwa kwa moto na mwanamke mwenzake. Mauaji hayo yametokea Alhamisi iliyopita kutokana na kile kilichodaiwa ni wivu wa mapenzi. Inadaiwa kuwa, mtuhumiwa aitwaye Joyce au mama Pili alikuwa akihisi marehemu anatembea na mume wake na ndipo alipofanya tukio hilo la kinyama.

Shuhuda mmoja wa tukio hilo ambaye aliomba jina lake kuhifadhiwa alisema mama Pili alikuwa akimlalamikia marehemu mara kwa mara kutembea na mumewe na akadai ‘atamuonyesha cha mtema kuni’, ndipo siku hiyo ya tukio (Alhamisi wiki iliyopita) nje kidogo na nyumbani kwake, alipomwagia petroli na kumchoma moto na marehemu kuungua vibaya mwili wake.

“Mama Pili ilikuwa ni kawaida yake kulalamika tena hadharani kwamba Lucia anatembea na mume wake na alidai aliwahi kuwafuma mara nyingi wakiwa wawili tu sehemu mbalimbali,” alisema shuhuda huyo. Lucia baada ya kuunguzwa alikimbizwa hospitali ya wilaya baada ya kupata PF 3, hata hivyo, alifariki dunia kabla ya kupewa matibabu ya kutosha. Imeelezwa kuwa mara Joyce alipopata taarifa kuwa mbaya wake

amefariki dunia alitoweka na kuna habari ambazo hazijathibitishwa zinazodai kwamba amekimbilia nchini Kenya kukwepa mkono wa sheria. Mama mwingine ambaye anafanya biashara ya vitumbua aliyeomba jina lake kuhifadhiwa alisema siku moja alishuhudia marehemu Lucia akibanwa na mama Pili kwa madai kwamba anatembea na mumewe na kwamba anamsababishia matatizo ya malezi “Ugomvi huo ulitokea mbele yangu na ulikuwa mkubwa ikabidi watu kuingilia na kuwaamulia lakini mama Pili alidai kwamba hawezi kumuacha hivihivi ni lazima amkomeshe,” alidai mama huyo. Gazeti la Uwazi lilifika ofisi ya Polisi ya Nyangoto ambapo polisi wa hapo walithibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini wakasema msemaji wao ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa.

Uwazi lilichapa mwendo hadi Ofisi ya Kijiji cha Kerende na kuzungumza na Mwenyekiti wa Kijiji, Mniko Mgabe Cheki ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Kusema kwali alichokifanya mama huyo ni ukatili mkubwa sana. Kuchukua hatua ya kumwagia mwenzako petroli na kumlipua kwa moto ni unyama mkubwa, watu sasa wamegeuka na kuwa na roho za kinyama,” alisema kwa masikitiko kiongozi huyo wa kijiji. Naye kaka wa marehemu aliyejitambulisha kwa majina ya Keraka Keraka alithibitisha dada yake Lucia kufariki dunia kwa kulipuliwa kwa mafuta ya petroli.

“Tukio hilo limetokea na naiomba serikali ichukue hatua kali juu ya mtuhumiwa. Isilifumbie macho licha ya kwamba mtuhumiwa ametokomea kusikojulikana lakini serikali ina mikono mirefu. Naomba apatikane ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema kaka huyo. Aliongeza kuwa katika vijiji vingi wilayani kwao hapo vitendo vya kikatili vimekithiri, hivyo sheria ichukue mkondo wake kwani ni kawaida watu kukamatwa wakiwa wametenda makosa na baadaye kuwaona mitaani wakitamba.

Mwanakijiji mwingine aliyezungumza kwa sharti la jina lake kutoandikwa gazetini alisema kijijini hapo hakuna usalama na vituo vingi vya polisi wilayani humo wamewekeza nguvu zao kulinda migodi ya dhahabu badala ya raia na akamuomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kutembelea wilaya hiyo ya Tarime ili akasikilize kero zao.


Loading...

Toa comment