The House of Favourite Newspapers

Mama Mbaroni kwa Tuhuma za Kumchinja Mtoto Wake

0

Mkazi wa mji mdogo wa Ngaramtoni, wilayani Arumeru mkoani Arusha, Anna Maliaki (30) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa kumzaa, Godfrey Godson mwenye umri wa miezi 4 kwa kumchinja kwa kutenganisha kichwa na kiwiliwili.

 

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Salum Hamduni alisema tukio hilo limetokea katika mji huo na jeshi hilo linamshikilia mtuhumiwa huyo kwa upelelezi zaidi.

 

Alisema kuwa, jeshi hilo litamfikisha mahakamani kujibu shtaka hilo la mauaji, baada ya uchunguzi kukamilika, na mwili wa marehemu tayari umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.

 

“Tulipomhoji mwanamke huyo, alisema kuwa hakumbuki alichokifanya na alisema mwanawe bado yupo hai na kutaka aonyeshwe alipo, hata tulipomwambia amemuua alisema anamtaka mwanawe,” alisema askari polisi mmoja wa kituo cha Ngaramtoni.

 

Aidha, baadhi ya majirani walioshuhudia tukio hilo, walidai kuwa tukio hilo limetokea muda wa saa nne asubuhi katika nyumba ya mtuhumiwa huyo anayeishi na mumewe aliyejulikana kwa jina la Godson Mungaya.

 

Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo, Paulina Samweli, alisema kwamba baada ya mama huyo kutekeleza mauaji hayo, alitoka nje na kumwita jirani yake huyo ili ashuhudie alichokifanya na kukuta kichwa na kiwiliwili kikiwa barazani kimetenganishwa, huku kisu alichotumia kikiwa pembeni.

 

Alidai kuwa, baada ya kufika mtuhumiwa alidai hajui kitu kilichomchinja mwanawe, lakini mwilini maeneo ya miguuni na kwenye nguo zake mama huyo, zilikuwa zimetapakaa damu, huku kisu kikiwa pembeni ya kitanda.

 

Alisema kuwa, mtuhumiwa huyo alipofika kwake, alimwambia njoo kwangu na kumfuata kwa nyuma, lakini alitaka kukimbia nilimwambia huwezi kwenda mahali na kumfungia ndani na kuita watu waliomsaidia kumkamata.

 

“Nilishuhudia mtoto akiwa kichwa kimewekwa kando na kiwiliwili, nikamuuliza mtuhumiwa mtoto umemfanyaje, alijibu sijui mtoto amefanywa nini ila mimi naenda magereza mtoto wangu umtunze,” alisema.

 

Kwa upande wake shemeji wa mtuhumiwa huyo, Jerry Mungaya mkazi wa Ngaramtoni Juu, alisema alisikia watu wakipiga mayowe na alipotoka, alimkuta mume wa marehemu anavutana na mtuhumiwa na alipofika ndani, alikuta mwili wa marehemu na kisu kipo chini.

 

Alisema kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa na matatizo ya akili na mara zote wamekuwa wakiweka silaha mbali na nyumba hiyo, kwani kwa kipindi hiki alikuwa ametulia tofauti na mwanzoni.

 

Baadhi ya majirani wengine ambao pia ni ndugu na mume wa mtuhumiwa, walidai kwamba chanzo cha tukio hilo hakijulikani na hapakuwa na ugomvi wa kifamilia, ila walidai kwamba kuna wakati mtuhumiwa hukumbwa na matatizo ya akili.

STORI: Joseph Ngilisho, Arusha

Leave A Reply