The House of Favourite Newspapers

MAMA MLEMAVU AFANYIWA UKATILI!

AMA kweli watu wamekosa utu! Mama mmoja aliyetambulika kwa jina la Fatuma Hamis hivi karibuni alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kufanyiwa ukatili wa kutisha, Uwazi linakujuza.

Mama huyo ambaye ni mlemavu wa viungo aliyedai alitokea mkoani Morogoro na kuja Dar kwa ajili ya matibabu na kutafuta maisha alikutwa ametupwa kando ya barabara maeneo ya Sinza Kamanyola jijini Dar na kusababisha hali yake kuzidi kuwa mbaya kutokana na upepo pamoja na vumbi la barabarani hapo.

Shuhuda mmoja wa tukio hilo alisema alimshtukia mama huyo majira ya saa moja asubuhi akilia kuomba msaada na alipomsogelea alishangaa mama huyo kumuona akigalagala huku akilia kwa uchungu.

Aliendelea kusema kuwa kilichoshangaza zaidi ni kwamba pembeni mwa mama huyo kulikuwa na mizigo yake zikiwemo ndoo za maji, kibao cha kukunia nazi, jiko la mkaa, chetezo, vifaa vya kupikia vikiwemo, sufuria, mwiko, furushi la nguo na baiskeli ya walemavu.

Shuhuda huyo alisema baada ya kumkaribia alijaribu kumuuliza shida yake ndipo akamueleza kilichomsibu huku akizungumza kwa shida kutokana na hali ya kuumwa aliyokuwa nayo.

Kufuatia hali hiyo wananchi walianza kukusanyika eneo hilo na kupiga simu polisi ili wampe msaada zaidi wa kiusalama.

Uwazi lilifika eneo la tukio na kuwakuta wananchi hao wakiendelea kumsaidia mama huyo aliyekuwa akisema amezidiwa huku akionekana kama mwenye presha ambapo alikuwa akiomba apatiwe maji ya kunywa.

Akizungumza kwa shida na mwandishi wetu, mama huyo alisema ametokea mkoani Morogoro na alishuka Stendi Kuu ya Mkoa, Ubungo usiku hivyo asubuhi hiyo alichukua Bajaj impeleke Hospitali ya Sinza (Palestina).

Mama huyo aliendelea kusema kuwa, baada ya kufika eneo hilo dereva huyo wa Bajaj aliyesema hamkumbuki vizuri labda mpaka akimuona alimshusha kwa nguvu kwenye Bajaj na kukimbia.

“Nilipanda Bajaj pale Ubungo nikamwambia nataka kwenda Hospitali ya Sinza lakini tulipofika maeneo haya baada ya kushindwa kuelewana ndipo akanishusha na kunitupia nje vitu vyangu,” alisema mama huyo.

Baada ya Uwazi kuzungumza na mama huyo, polisi nao walifika eneo la tukio na kumchukua ambapo walimpeleka katika Kituo cha Polisi Urafiki.

Kutokana na hali ya kiafya ya mama huyo kutokuwa nzuri polisi hao waliamua kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu.

Gazeti hili lilifika hospitalini hapo kwa ajili ya kujua kilichoendelea kuhusu hali ya mama huyo lakini taarifa zilieleza kwamba baada ya polisi kumfikisha alipokelewa katika chumba cha wagonjwa wa dharura ambapo alitibiwa na kuruhusiwa.

Mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni halikuweza kumpata mama huyo azungumze zaidi kwani baada ya kuruhusiwa hospitalini hapo haijulikani alipokwenda.

STORI: RICHARD BUKOS, UWAZI

Comments are closed.