The House of Favourite Newspapers

Mambo Kumi Usiyoyajua Kuhusu DK Mpango

0

DK Philip Isidor Mpango (63) ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango katika Serikali ya Awamu ya Tano jana akateuliwa na kupitishwa na Bunge kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaapishwa leo.

 

Jina lake lilipendekezwa na Rais Sumia Suluhu Hassan, akalipeleka bungeni, mara baada ya jina lake kutajwa bungeni na wabunge kupiga kura, Spika wa Bunge, Job Ndugai alitangaza kuwa Dk. Mpango alipata kura 363 ambazo ni sawa na asilimia mia moja kwa kuwa hakuna kura iliyoharibika.Kuna mambo 10 ambayo baadhi ya watu hawayajui kuhusu Dk. Mpango ambaye pia alikuwa mbunge wa Jimbo la Buhingwe, wilayani Kibondo, mkoa wa Kigoma, jimbo ambalo sasa ameliachia.

 

ASILI YAKE

Dk. Mpango ni mzaliwa wa Kigoma, alizaliwa kijiji cha Kasumo, ni mchumi mwenye shahada ya uzamivu ya uchumi na ana sifa lukuki. Mosi, kuanzia miaka ya 1990 hadi 2000, alifanya kazi akiwa mhadhiri mwandamizi wa uchumi katika kitivo cha Biashara cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

 

Alikuwa mwalimu akifundisha “Microeconomics”, “Macroeconomics” kwa mwaka wa pili na “Public Finance” kwa mwaka wa tatu na kozi za uzamili. Pili, Dk Mpango amewahi kuwa Mchumi Mwandamizi wa Benki ya Dunia, tatu amewahi kuwa Mkuu wa Kamati ya kumshauri Rais Jakaya Kikwete wakati huo kuhusu masuala ya uchumi.

 

Nne; Dk Mpango amewahi kuwa katibu binafsi (Katibu mnyeka) wa Rais Kikwete anayeshughulikia masuala ya uchumi, tano amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, kabla ya kuhamishiwa Tume ya Mipango, Ofisi ya Rais.

 

Nyadhifa hizi zote amezishika wakati wa utawala wa Kikwete.

 

Sita; hayati Rais Magufuli alipoingia madarakani, alimteua kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baada ya siku chache akateuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

 

Dk Mpango ni kiongozi mwenye msimamo thabiti na amewahi kufanya kazi ofisi ya Rais kwenye idara ya uchumi na baadhi ya watendaji ambao wamewahi kufanya kazi chini yake kwenye ofisi hiyo wanaeleza sifa ya saba kwamba ni mtu anayetaka waliomzunguka wazungumze kwa takwimu na ushahidi hasa katika masuala ya uchumi.

 

Msimamo huo pia aliuonyesha alipokuwa mtaalamu wa Benki ya Dunia. Nane; anatajwa kuwa hakuwa mwoga kuieleza ukweli Serikali pale ambako ilikuwa haifanyi vizuri.

 

Mathalan, wakati wasomi wengi wa uchumi wakiwa wanapiga kelele za kuisifia serikali juu ya ukuaji wa uchumi miaka ya mwanzoni ya 2000, Dk Mpango alieleza wazi kuwa lengo hilo la kukuza uchumi kwa asilimia 5.9 haliwezi kufikiwa kwa sababu katika miaka minne iliyopita, Serikali ilishindwa kulifikia.

 

Misimamo ya namna hii ni nadra kwa wasomi wa ngazi yake walio wengi, ambao hubakia kusifia kila kinachotendwa na Serikali ilimradi kwa kutegemea siku moja watateuliwa kushikilia nyadhifa kubwa.

 

Ushahidi wa msimamo wa Dk Mpango pia umeelezwa na baadhi ya wanafunzi wake aliowafundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wengine ni wahadhiri katika chuo hicho hivi sasa.

 

Tisa; mwanafunzi wake mmoja amenieleza kuwa kama kuna mwalimu ambaye wanafunzi wa uchumi walikuwa wanampenda na kumheshimu ni daktari huyu. Pia anasema kama kuna mwalimu ambaye walikuwa wanamuogopa kwa misimamo yake ni huyu.

 

Nimeambiwa wakati wote alitaka wanafunzi wake waenende na miiko ya kitaaluma na hakuchelewa kuwa rafiki wa yeyote pale anapofanya vizuri.

 

Kumi; Dk Mpango ni kiongozi mwenye dira na maono mapana, ni mtendaji anayeweza kusimamia jambo alilokabidhiwa na likafanikiwa.

 

Alipoteuliwa kuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, ndani ya mwezi mmoja ukusanyaji wa mapato wa taasisi hiyo ulivunja rekodi. Kwa mara ya kwanza TRA ilikusanya zaidi ya Sh1.4 trilioni kwa mkupuo. Aliyekuwa Rais, hayati Magufuli alijitokeza na kumpongeza kwa hatua hiyo na muda mfupi baadaye akamkabidhi Wizara ya Fedha kuwa waziri.

 

Ubobezi na ujuzi wake kwa uchumi wa chini na juu wa wananchi na kujua matatizo na hatua za kuchukua ni kigezo tosha kitakachomsaidia daktari huyu kuchukua hatua za kiuchumi za kulivusha Taifa hadi kuwa katika daraja la uchumi wa kati.

 

Mahali kote alikopita amechukuliwa kama mtendaji hodari, mweledi na anayejitambua katika majukumu yake.

 

Jambo dogo ambalo linaweza kumsumbua kwake ni uzoefu wa masuala ya siasa. Watu wake wa karibu wameniambia kuwa kiongozi huyu hata siku moja hakuwahi kuwa na ndoto za kuwa mwanasiasa wala hakuwahi kutamani na kufikiria nyadhifa za kisiasa.

 

Anayo kazi ya kufanya kujigeuza kisaikolojia na kiakili kukubaliana na hali ya sasa kwamba yeye ni mwanasiasa lakini akabaki katika misingi yake ya taaluma na kusimamia.

STORI: ELVAN STAMBULI, RISASI

Leave A Reply